Nov 07, 2022 09:13 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (26)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 26 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitatupia jicho maudhui ya ukamilifu wa kiutu katika mada yetu ya Akhlaqi katika Familia kwa mtazamo wa dini tukufu ya Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Kama tulivyotangulia kueleza, katika sehemu iliyopita ya 25 tulianza kuzungumzia "Akhlaqi katika Familia" na tukabainisha kuwa, katika suala la kufunga ndoa na kuanzisha taasisi ya familia, ambayo ni moja ya nguzo kuu za mfumo na jamii yoyote ile, kuanzia mwanzo wake inapotaka kujengwa, inapasa nguzo za familia zisimamishwe juu ya msingi imara unaotokana na imani madhubuti za dini na za kiutu ili kuweza kuwa na jengo imara na madhubuti pia la familia hiyo.

Kuhusiana na suala hili, kuna nukta ambayo inapasa kuzingatiwa, nayo ni kwamba, mwanadamu ana hisia za kutaka awe na hali ya ukamilifu; na kila mara hupenda awe katika hali ya kupiga hatua mbele ili aweze kuyafikia yale yote anayotamani na anayoyatarajia. Uislamu, ambao unaichukulia ndoa kama ngazi au lifti ya kasi ya kumfikisha mtu kwenye vilele vya ukamilifu, unatuonyesha na kutubainishia wazi kigezo bora cha familia iliyo na kiu ya kuwa na ukamilifu wa kiutu na kuwataka watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu wamuelekee Mola aliye Mpaji wa ukamilifu kwa waja wake na kumwomba dua ifuatayo ya aya ya 74 ya Suratul-Furqan: "Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu."

Pamoja na hayo, ifahamike pia kwamba kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Uislamu, dua peke yake haitoshi; na kimsingi huwa na athari, pale mtu mwenyewe anapofanya jitihada pia za kuyafikia yale ayatakayo. Isitoshe, kutokana na maelezo ya aya hiyo inabainika wazi kuwa, kufunga ndoa na kuasisi familia inapasa kufanyike kwa lengo maalumu; na ni pale inapokuwa hivyo tu ndipo tunaweza kuwa na matumaini ya kupatikana mke, mume na watoto wa kumpa mtu heshima kutokana na familia hiyo, au kama inavyoeleza Qur'ani; wenye tabia, mwenendo na shakhsia za kuyapa kitulizo macho ya wanaowatizama, yaani kumpa mtu furaha na uchangamfu.

Nukta nyingine muhimu iliyomo katika aya ya 74 ya Suratul-Furqan ni kwamba, familia imetajwa kuwa ndio njia inayowezesha mtu kufikia upeo wa juu kabisa wa ukamilifu na inasema:  Na utujaalie (familia yetu) tuwe waongozi kwa wachamngu."

Moja ya vigezo muhimu vinavyompa ilhamu Muislamu, ambavyo Uislamu unavitaja kuwa mfano wa kuigwa, ni vya shakhsia na watu ambao baada ya kuivuka hatua ya kuukubali Uislamu na kuamini, wamefikia kilele cha ukamilifu wa kiutu, ambacho ni taqwa na uchamungu. Katika kubainisha sifa maalumu za watu hao, kuna aya na Hadithi nyingi katika mafundisho ya Uislamu asilia zinazotoa taswira ya hadhi kubwa na tukufu waliyonayo waja hao. Kwa maelezo haya mafupi, unatubainikia umuhimu na nafasi inayochangia dua hii; nayo ni kufahamu, tunapomwomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa waongozi na wa mbele katika taqwa na kumcha Yeye, huwa inatupasa tupige hatua kiasi gani kwa ajili ya kufikia malengo yenye utukufu mkubwa; na ni jukumu lenye uzito gani analibeba mabegani mwake mtu anayetaka kuwa na familia bora iliyo kigezo cha kupigiwa mfano. Inatosha kufahamu umuhimu wa lengo hili tukufu, tunapozingatia kwamba hata Mitume wa Mwenyezi Mungu nao pia walikuwa wakimwomba Mola awajaalie kuwa na wake na watoto wema, ili wawe ruwaza na kigezo kwa watu wengine.

Baada ya Nabii Ibrahim (as), mbeba bendera ya chuo cha fikra ya tauhidi, pamoja na mwanawe, Nabii Ismail (as) kukamilisha kazi ya kuliinua tena jengo la al Kaaba, alimuelekea Mola Mwenyezi na kumuomba dua hii ya aya ya 128 ya Suratul-Baqarah: " Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma ulio silimu kwako. Na utuonyeshe njia za ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu."  

Kwa hivyo katika familia iliyo kigezo na mfano wa kuiga, inatakiwa imani juu ya Mwenyezi Mungu itawale maisha ya watu wa familia hiyo. Katika hali kama hiyo, hisia za ubinafsi na umimi, ambazo ndio chanzo cha mitifuano mingi ya kifikra, ya kikauli na kitabia katika maisha ya ndoa hufifia, na badala yake utulivu maalumu ulionukizwa manukato na marashi ya upendo na huruma huipa hali maalumu ya furaha taasisi ya familia; na endapo itatokea watu kukosana, basi huwa tayari kirahisi kufidia makosa yao kwa kutubia na kuombana radhi.

Dua nyingine ambayo Nabii Ibrahim (as), -anayetajwa na Mwenyezi Mungu kama ruwaza na kigezo cha kufuatwa na wafuasi wa njia ya tauhidi,- alimuelekea kwa unyenyekevu Mola Mwenyezi na kumuomba, ni ile ya aya ya 40 ya Suratu-Ibrahim isemayo: "Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala, na katika dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu."  

Aya hii mpendwa msikilizaji imebeba ndani yake nukta kadhaa muhimu na za msingi: Moja ni kwamba, ili kuasisi familia bora, ambayo itakuwa mwongozi wa wachamungu, hatua yoyote chanya na athirifu inapasa ianze kuchukuliwa na akina baba, ambao ndio wenye jukumu kuu la kuongoza na kutoa muelekeo wenye malengo kwa familia. Ni kwa sababu hiyo, Nabii Ibrahim ameianza dua yake kwa kumwomba Mwenyezi Mungu: "Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala." Nukta nyingine ni kuwa, pamoja na kuandaa mipango na kufanya juhudi za kuasisi familia bora, tunatakiwa tuelekeze matumaini yetu kwa rehma za Mwenyezi Mungu na kumuomba Yeye Mola atupe auni na msaada wake katika kulea watoto wema, ili tuweze kuyafikia malengo matukufu tuliyoya kusudia. Hapa kuna mambo mawili muhimu ya kufanyiwa kazi ambayo yameashiriwa katika aya hii: moja ni kusimamisha Sala, ambayo ni dhihirisho la utajo wa Mwenyezi Mungu na jengine ni dua na kushtakia shida na haja zetu kwa Yeye Mola, ambako kunaimarisha mihimili ya kimaanawi ya familia na kuwa kinga na ngao ya kuikinga na madhara.

Ujumbe wa mwisho muhimu katika aya hii ni kwamba, familia bora inaweza kutoa mchango mkuu na athirifu katika malezi ya vizazi vijavyo vya familia na jamii yoyote ile. Na ni kwa sababu hiyo, Nabii Ibrahim (as) amemwomba Mwenyezi Mungu asimjaalie yeye tu, bali vizazi vyake vinavyofuatia pia, viwe ni vya wanaosimamisha Sala. Mtazamo wa aina hii unabainisha kuwa, familia safi, salama na thabiti haifikirii malezi ya kizazi cha zama zake tu, bali inajihisi kuwa na jukumu la vizazi vya zama za baada yake pia. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kwamba, sehemu ya 26 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 27 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/