Nov 10, 2022 16:26 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (37)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 37 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia umuhimu wa kutumia akili na busara na hatari na madhara yanayoweza kuisibu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Bila shaka mpendwa msikilizaji ungali unakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba akili ina hadhi na nafasi maalumu katika utamaduni wa Uislamu unaoshajiisha elimu na kujifunza na pia ni kipimo muhimu sana kinachokubalika mbele ya Mwenyezi Mungu na viongozi wakuu wa dini kwa ajili ya kutathmini amali na utendaji wa watu. Katika utamaduni wa Uislamu, viongozi wateule wa dini ni hoja, ushahidi na mwongozo wa nje wa kumtambulisha mtu uongofu; na akili, ni hoja na nuru ya batini ya ndani ya nafsi ya kumwangazia njia ya uongofu.

Moja ya madhara hatarishi yanayoweza kuidhuru akili ni madhara ya upofu na ujahili. Ifahamike kuwa, kwa mtazamo wa uono wa kina wa Uislamu, ujahili haumaanishi ujinga tu wa kutojua kusoma na kuandika; kwa sababu si hasha uono finyu na wa kijuujuu wa mambo, kukosa basira na uwezo wa kupambanua baina ya haki na batili kukawaingiza maulamaa na wasomi wakubwa wakubwa kwenye tapo la majahili. Imam Ali (AS) amesema katika moja ya semi zake za hekima: "Si hasha mtu aliye alimu sana akaangamizwa na ujahili wake (wa akili na roho); na elimu na ujuzi wake visiwe na faida yoyote kwake". Nahjul-Balagha, Hekima ya 102

Qur'ani tukufu inawafananisha maulamaa na wasomi kama hao walioghariki kwenye dimbwi la upofu na ujahili na punda abebaye mzigo mkubwa wa vitabu, kubainisha kwamba elimu zao hazina faida yoyote kwao. Na ni kwa sababu hiyo pia, ndio maana katika aya ya 36 ya Suratul-Israa, Qur'ani inapinga kila aina ya ujinga na ujahili kwa kusema: "Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa."

Bwana Mtume Muhammad SAW amesema: "Mimi siuhofii umma wangu kusibiwa na ufakiri; ninachelea upofu na ujahili. Madhara ambayo ufakiri wa kifikra utausababishia umma wangu ni zaidi ya ufakiri wa kiuchumi." Awali-Llali 4/39

Kama tulivyobainisha pia ni kwamba, kwa mtazamo wa utamaduni wa Kiislamu, ujahili hauwahusu watu wasio na elimu yoyote tu, bali kuna watu wengi wanaoonekana wamesoma, lakini kwa sababu ya kutokuwa na basira, kwa kuwa na uono finyu na wa kijuujuu wa mambo, ufahamu potofu, taasubi, ukereketwa na fikra mgando, nao wanaingia kwenye kundi la majahili na wasiojua kitu. Lakini mbali na hayo, huwa kila mara wanachukua hatua zinazokidhi malengo na sera za kishetani na zilizo dhidi ya utu, za wenye nguvu za utajiri na madaraka.

Imam Ali (AS), ambaye katika zama zake, alitaabishwa zaidi na kundi la watu hao, alikuwa akiwaambia: "Nyinyi ni mishale iliyoko mikononi mwa shetani, ambayo anaitumia kutokana na nafsi zenu ovu ili kufikia malengo yake; na kupitia kwenu nyinyi anawatumbukiza watu kwenye lindi la mduwao, shaka na upotofu." Nahjul Balagha, Khutuba ya 125.

Isisahaulike pia kwamba, ujahili na upofu hauhusiani na Zama za Ujahilia au Enzi za Kati pekee, kwa kimombo Middle Ages, lakini hata katika zama hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia pia zinashuhudiwa na kuonekana kwa uwazi alama za upofu na ujahili.

Xavier Crement, mwandishi na mtaalamu wa saikolojia wa Marekani amelichambua na kulizungumzia suala hilo katika kitabu chake alichokiita "Basi Tena Uzuzu". Crement anaufafanua wigo wa uzuzu huo kuwa ni: "Uzuzu wa kijamii, uzuzu wa kiraia, uzuzu wa wafanyabiashara, uzuzu wa kujipa utakatifu, uzuzu wa kujifanya mtu wa irfani, uzuzu wa urasimu, uzuzu katika siasa, uzuzu katika vyombo vya habari, uzuzu wa madikteta, uzuzu katika familia, uzuzu katika ndoa na uzuzu katika dunia ya kusoma na kuandika."

Uislamu, ambao ni dini ya uelimishaji inapiga vita ujahili na madhihirisho yote ya uzuzu na upumbavu katika kila zama na mahala. Tatizo la msingi la watu majahili, ambao hawajijui kama wana ujinga na ujahili ni kwamba, kutokana na kudhani kuwa kile wanachokijua wao ndicho sahihi na chenye mantiki, basi huendelea kung'ang'ania kufuata imani na mitazamo yao potofu na ya kijahili na hawawi tayari kukubali kauli yoyote yenye hoja na burhani za kimantiki.

Imam Ali (AS) ameizungumzia hivi sifa hii ya watu hao: "majahili ni mithili ya jabali na jiwe gumu, ambalo maji hayapenyi ndani yake; na ni mithili ya mti mkavu ambao haunawirishi matawi na majani yake yakastawi; na mfano wa ardhi yabisi ambayo mimea haiwezi kuota juu yake". Ghurarul Hikam 1341/34

Naam, kutokana na ukaidi wa majahili na kutokubali kubdilika kwa namna yoyote ile ilifika hadi Mwenyezi Mungu Mtukufu, aliyetuma Mitume na akawapa ujumbe wa kuwaelimisha na kuwaelekeza watu kwenye uongofu, akamhutubu Mtume wake mteule kama aya ya 40 ya Suratu-Zukhruf inavyosema: Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza kuwaongoa vipofu na waliomo katika upotofu ulio wazi?

Hata kama katika historia, siku zote yamekuwepo makundi na matapo yenye sifa kama hizi, ambayo kwa sababu ya ujahili na upofu wao, kwa upande mmoja, yalisimama kukabiliana na viongozi wa dini; na kwa upande mwingine, yalionyesha uduni na udhalili mbele ya watawala majabari; lakini mfano hai wa watu na matapo kama hayo katika zama za sasa ni makundi ya ukufurishaji, ya Kiwahabi na Kidaesh yaliyoasisiwa na kulelewa na Uistikbari wa dunia; ambayo yamefikia kilele cha ujahili na utovu wa hisia, kwa kuwa tayari kufanya jinai ya aina yoyote ile. Na kwa kujidhihirisha na kujionyesha kwao kuwa ni Waislamu, tena wenye uchungu na walioshika dini barabara, wameweza kupanda mbegu za mifarakano, vita na umwagaji damu katika Ulimwengu wa Kiislamu; na kwa kufanya hivyo wakaweza kuwaridhisha na kuwapendezesha mabwana zao wa Kimarekani, wa Ulaya na wa Kizayuni.

Lakini kinyume na dhana ya kijahili waliyonayo wenyewe ya kuamini kuwa hatima na makazi yao akhera yatakuwa ni peponi, Qur'ani tukufu inaubainisha mwisho wao kama sehemu ya aya ya 97 ya Suratu-Israa inavyosema:  "Na tutawakusanya Siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu." Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji, niseme pia kwamba, sehemu ya 37 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 38 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/