Nov 13, 2022 02:21 UTC
  • Jumapili, 13 Novemba, 2022

Leo ni Jumapili tarehe 18 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 13 Novemba 2022 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 842 iliyopita alizaliwa Muhaqiq Hilli, Abul Qasim Jaafar bin Hassan, mmoja wa wanazuoni wakubwa na faqihi ya Kiislamu katika mji mashuhuri wa Hillah nchini Iraq. Muhaqiq Hilli alikuwa msomi aliyekuwa na nafasi ya juu na mtaalamu wa sheria za Kiislamu na alibobea pia katika fasihi na uandishi wa mashairi. Baada ya kukamilisha masomo ya awali na kukwea daraja za juu za kiroho, alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa zama zake. Kitabu muhimu zaidi cha Muhaqqiq al Hilli ni Sharaiul Islam fii Masaailil-Halal Wal-haraam'. Mwanazuoni huyo pia ameandika vitabu vya "Nafi', Ma'arij na Tanbih". Muhaqqiq al Hilli alifariki dunia mwaka 676 Hijria akiwa na umri wa miaka 74. ***

Muhaqiq Hilli

 

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita hayati Hafidh Assad alichukua hatamu za uongozi wa Syria baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1970 na baadaye akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Hafidh Assad alizaliwa mwaka 1930 na mwaka 1964 alichaguliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha jeshi la Syria. Miaka mitatu baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Hafidh Assad alifariki dunia mwezi Juni mwaka 2000 baada ya kuugua kwa muda mrefu. ***

Hafidh Assad

 

Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Ayatullah Sayyid Morteza Pasandideh kaka wa Imam Ruhullah Khomeini. Alisoma masomo ya awali ya kidini kwa maulama na wanazuoni wa mji wa Isfahan na kushiriki masomo ya elimuu ya juu ya kidini kwa maustadhi mashuhuri wa zama hizo. Baadaye alirejea katika mji wa Khomein na kujishuhulisha na ufundishaji wa fikihi, usuul na masomo mengine. Ayatullah Pasandideh anayejulikana kama alimu na mujahidi, kipindi fulani alibaidishwa kutokana na upinzani wake kwa utawala wa kifalme wa wakati huo wa Reza Khan na kusimama kwake kidete dhidi ya utawala huo. ***

Ayatullah Sayyid Morteza Pasandideh kaka wa Imam Ruhullah Khomeini.

 

Na miaka 7 iliyopita tarehe 13 Novemba saa tatu na dakika 16 usiku kwa wakati wa Ulaya ya Kati milipuko kadhaa ya kigaidi ilitokea katika vitongoji nambari 1, 10 na 11 ya jiji la Paris nchini Ufaransa na kuua watu 130 na kujeruhiwa wengine 368. Baadhi ya milipuko hiyo ilitokea karibu na uwanja wa michezo wa Stade de France ulioko kaskazini mwa jiji la Paris wakati wa mechi ya mpira wa miguu kati ya timu za taifa za Ufaransa na Ujerumani. Wakati huo huo watu wengine 87 waliuawa katika utekeji nyara uliofanyika katika ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Bataclan mjini Paris. Mashambulizi hayo yalihesabiwa kuwa makubwa zaidi kutokea nchini Ufaransa baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Siku moja baadaye kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuwa ndilo lililohusika na mashambulizi hayo. ***

Mashambulio ya kigaidi Paris Ufaransa

 

Tags