Ijumaa tarehe 18 Novemba 2022
leo ni Ijumaa tarehe 23 Rabiuthani 1444 Hijria sawa na tarehe 18 Novemba 2022.
Katika siku kama ya leo miaka 235 iliyopita Louis Daguerre mchoraji, mvumbuzi na mtaalamu wa elimu wa fizikia wa Kifaransa alifariki dunia. Mwaka 1789 mtaalamu huyo alifanikiwa kuvumbua mambo kadhaa. Miongoni mwa uvumbuzi muhimu wa Louis Daguerre ni ule wa mwaka 1839 ambapo alifanikiwa kuvumbua camera ya kupigia picha na kwa kutumia camera hiyo akapiga picha ya kwanza iliyokuwa ikionekana vizuri.
Tarehe 23 Rabiuthani miaka 199 iliyopita alifariki dunia faqihi, mwanachuoni wa Hadithi na malenga mashuhuri wa Kiislamu, Allamah Ahmad Naraqi. Mwanazuoni huyo alizaliwa mwaka 1185 Hijria na kukulia katika mji wa Kashan katikati mwa Iran ambako alipata elimu kwa baba yake, Mullah Mahdi Naraqi. Miaka kadhaa baadaye alihamia katika mji mtakatifu wa Najaf, nchini Iraq na kupata elimu ya juu kwa maulamaa wakubwa wa mji huo. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vya "Miirajus Saada" na "Asrarur Hajj."
Siku kama ya leo miaka 183 iliyopita ilianza awamu ya pili ya mapambano ya wananchi wa Algeria wakiongozwa na Abdul Qadir bin Muhyiddin dhidi ya ukoloni wa Ufaransa. Ufaransa iliivamia Algeria mwaka 1830 ikiwa na nia ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Amir Abdul Qadir akiwa pamoja na wapiganaji elfu 50 alipambana na wakoloni wa Kifaransa hadi mwaka 1847. Lakini hatimaye jemedari huyo wa Algeria alishindwa na kukamatwa mateka. Karibu karne moja baadaye, baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wananchi wa Algeria walianzisha tena mapambano ya kupigania uhuru dhidi ya wakoloni wa Kifaransa na mwaka 1962 Algeria ilipata uhuru.
Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita ulitiwa saini mkataba wa Mfereji wa Panama kati ya Marekani na Jamhuri ya Panama. Kwa mujibu wa mkataba huo mfereji huo ulikodishwa milele kwa Marekani mkabala wa Panama kupewa dola milioni 10 taslimu na dola laki mbili na nusu kila mwaka. Baadaye wananchi wa Panama walianzisha mapambano ya kupinga mkataba huo na hatimaye wakailazimisha Marekani kutazama upya kipengee cha kukodishwa mfereji huo milele. Kwa msingi huo mwaka 1978 Jimmy Carter na Jenerali Omar Efraín Torrijos viongozi wa wakati huo wa Marekani na Panama walitia saini mkataba mpya ambao kwa mujibu wake mfereji wa Panama ulirejeshwa chini ya mamlaka kamili ya nchi hiyo mwishoni mwa mwaka 1999.
Miaka 66 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 18 Novemba mwaka 1956, nchi ya Morocco ilipatia uhuru. Kabla ya hapo ardhi hiyo ilikuwa chini ya tawala na mataifa mbalimbali. Hata hivyo kufuatia kuenea dini Tukufu ya Kiislamu katika maeneo mbalimbali duniani, yakiwemo maeneo ya kaskazini mwa Afrika, ardhi ya Morocco nayo ikawa miongoni mwa ardhi za utawala wa Kiislamu. Mwaka 1921 Ufaransa iliidhibiti Morocco hadi mwaka 1956 wakati nchi hiyo ilipojitangazia uhuru.
Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita alifariki dunia msomi na mwanafizikia wa Denmark, Niels Bohr, akiwa na umri wa miaka 82. Bohr alizaliwa mwaka 1885 na kuvutiwa mno na elimu ya hisabati. Msomi huyo alifanya uchunguzi na uhakiki mkubwa katika elimu hiyo. Niels Bohr pia alifanya uhakiki katika masuala ya atomu na mwaka 1945 alitunukiwa Tuzo ya Nobel katika medani ya fizikia kutokana na uvumbuzi wake katika masuala ya atomu.
Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita kanali Abdul Salam Arif alishika hatamu za uongozi nchini Iraq baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu. Ikulu ya Rais na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq zilishambuliwa kwa mabomu na kupelekea kuuawa Abdul Karim Qasim aliyekuwa Rais wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, Abdul Karim Qasim naye aliingia madarakani mwaka 1958 baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji yaliyohitimisha utawala wa Kifalme nchini humo.
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita wiki mbili tu baada ya wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini kuteka ubalozi wa Marekani mjini Tehran ambao ulitambuliwa kuwa pango la ujasusi la nchi hiyo, mateka wanawake na weusi wenye asili ya Afrika waliokamatwa katika ubalozi huo waliachiwa huru kwa amri ya hayati Imam Ruhullah Khomeini. Ubalozi huo ulikuwa kituo cha ujasusi na kupanga njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa sababu hiyo wafanyakazi wake walishikiliwa mateka kama majasusi wa Marekani hapa nchini. Hata hivyo Imam Khomeini na kwa sababu za kibinadamu na vilevile kwa kutilia maanani kwamba, wanawake na Wamarekani weusi wanadhulumiwa na kubaguliwa nchini kwao, alitoa amri waachiwe huru. Sehemu moja ya barua ya hayati Imam Khomeini kwa wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakiwashikilia mateka Wamarekani hao inasema: Uislamu umetunga sheria makhsusi kwa ajili ya wanawake, na watu weusi kwa miaka mingi wamekuwa chini ya mashinikizo na dhulma za Marekani na pengine wamelazimishwa kuja Iran. Kwa msingi huo wapeni tahfifu iwapo haitathibitika kwamba wamefanya ujasusi", mwisho wa kunukuu. Kwa utaratibu huo mateka 13 wa kike na wale wenye asili ya Afrika waliachiwa huru.