Ijumaa tarehe Pili Disemba 2022
Leo ni Ijumaa tarehe 7 Jumadil Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe Pili Disemba 2022.
Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, Mirza Kuchak Khan Jangali, mwanaharakati na mpigania ukombozi wa Kiirani aliuawa shahidi na vibaraka wa Reza Khan, dikteta wa wakati huo wa Iran kwa ushirikiano wa madola ya Umoja wa Kisovieti na Uingereza. Mirza Kuchak Khan Jangali alijifunza masomo ya dini akiwa katika rika la ujana na kufanikiwa kukwea daraja za juu za kielimu. Baadaye alijiunga na safu ya wapigania uhuru hadi alipokamatwa na vibaraka wa Reza Khan na kuuawa kwa kukatwa kichwa kilichopelekwa kwa mfalme huyo kibaraka.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, Peninsula ya Korea iligawanywa katika sehemu mbili za kaskazini na kusini. Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa Japan ambayo ilikuwa imedhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya mashariki mwa Asia, viongozi waitifaki walifanya vikao katika miji ya Yalta na Potsdam wakijadili juu ya namna ya kuongoza dunia baada ya kumalizika kwa vita hivyo. Hata hivyo katika vikao hivyo kulibainika mapema kwamba Marekani na Urusi ya Mazani, zilikuwa zikiwania fungu kubwa zaidi kwa ajili ya kupenyeza siasa zao na kulidhibiti eneo tajwa. Hivyo eneo hilo na kwa mujibu wa mapendekezo ya viongozi wa nchi zilizoibuka washindi katika vita, likagawanywa sehemu mbili katika siku kama ya leo.
Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, Laos ilipata uhuru kamili. Uhuru wa nchi hiyo ulipasishwa katika mkutano uliofanyika Geneva mwaka 1945 kwa kuhudhuriwa na nchi za eneo na serikali kubwa duniani. Laos ilikuwa chini ya uongozi rasmi wa Ufaransa tangu mwaka 1893. Na ilipofika mwaka 1949, Ufaransa ililazimika kuipatia Laos uhuru wa kiwango fulani katika fremu ya Umoja wa Kifaransa, kufuatia mapambano ya ukombozi yaliyoanzishwa katika eneo la India na China.
Miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo, Fidel Castro alianzisha harakati ya kuikomboa nchi yake ya Cuba. Castro akiwa na lengo la kupambana na dikteta Fulgencio Batista, alianzisha mapambano ya silaha akiwa pamoja na wenzake kwa kuishambulia kambi ya kijeshi ya Moncada. Hata hivyo vikosi vya dikteta Batista viliikandamiza vibaya harakati hiyo na kumtia mbaroni Fidel Castro na kumfunga jela. Baada ya muda Castro alipelekwa uhamishoni. Hata hivyo baadaye aliunda kundi jingine la wapiganaji na kurejea Cuba alikoanzisha mapambano mapya. Hatimaye wanamapinduzi hao wa Cuba walifanikiwa kuyadhibiti maeneo muhimu ya nchi hiyo hali iliyomfanya dikteta Fulgencio Batista akimbilie katika kituo cha kijeshi cha Marekani na baadaye kutoroka nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, aliuawa kwa kunyongwa mjini Cairo, Misri Sayyid Qutb, msomi na mwanamapambano mashuhuri wa nchini Misri akiwa pamoja na wanafunzi wake wawili. Akiwa na umri wa miaka kumi, Qutb aliweza kuhifadhi Qur'ani yote na kuanza kujihusisha na masuala ya kisiasa na mapambano dhidi ya ukoloni na udikteta wa zama hizo. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha mjini Cairo na kusoma kwa miaka 16, huku akifanya safari nchini Marekani mnamo mwaka 1948 kwa ajili ya kuendelea na masomo yake. Matukio ya ukandamizaji na ukatili aliyoyashuhudia nchini Marekani, yalimfanya awachukie sana Wamagharibi. Katika harakati za mapambano yake ya kisiasa, Sayyid Qutb alifahamiana na Hassan al-Banna, mwasisi wa Harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin na hatimaye naye akajiunga na harakati hiyo ambapo alitokea kuwa na nafasi kubwa. Hata hivyo kutokea tofauti baina yake na Gamal Abdel Nasser, rais wa wakati huo wa Misri, kulimpelekea atiwe mbaroni na hatimaye kunyongwa katika siku kama ya leo.
Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, Umoja wa Falme za Kiarabu ulipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na kila inapowadia siku kama hii ya leo nchi hiyo huiadhimisha kama siku ya taifa. Ni vyema kutaja hapa kuwa, tawala za kifalme za kusini mwa Ghuba ya Uajemi zilikuwa chini ya utawala wa Uingereza tangu mwaka 1920 Miladia. Uingereza iliasisi vituo vingi vya kijeshi katika eneo hilo, hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, nchi hiyo ilidhoofika na ikaliweka katika ajenda yake suala la kuondoka katika Ghuba ya Uajemi.
Na tarehe Pili Disemba kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Kufutwa Utumwa kote duniani. Japokuwa utumwa umefutwa katika maeneo mengi ya dunia lakini suala hilo lingali linashuhudiwa duniani katika kalibu ya utumwa mambo leo.