Hikma za Nahjul Balagha (5) + SAUTI
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 5 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama zilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya Tano.
الْعِلْمُ وِرَاثَهٌ کَرِیمَهٌ، وَالاْدَابُ حُلَلٌ مُجَدَّدَهٌ، وَالْفِکْرُ مِرْآهٌ صَافِیَهٌ
Imam Ali AS amenukuliwa akisema: Ilmu; ni urithi wenye thamani, na adabu ni mapambo ambayo muda wote ni mapya, na tafakuri ni kioo safi muda wote.
Labda swali hili limewahi kukupitikia na wewe mpenzi msikilizaji, kwamba ni vipi baadhi ya watu wa familia au wanafunzi shuleni na katika vyuo vikuu, au wafanyakazi wenzako ofisini n.k, licha ya kwamba nyote mna hali sawa za elimu na suhula nyinginezo, lakini fikra na akili zenu haziko sawa? Kwa nini wengine wanashindwa kufikia mafanikio makubwa! Uchunguzi na tafiti mbalimbali zimefanywa katika uwanja huu. Matokeo ya tafiti hizo yanaonesha kuwa siri ya mafanikio ya watu hawa ni kujua jinsi ya kutumia vizuri fursa anazopata mtu kwa ajili ya kuwa na matokeo bora katika jitihada zake.
Ikiwa pia unatafuta mafanikio katika mambo yako ya maisha, unapaswa kuzingatia ukweli kwamba katika kila kitu, wewe si wa kwanza! Kumbuka kuwa kabla yako, kuna wenzako wengi wamewahi kuwa katika mazingira kama yako. Kwa hakika, baadhi yao wamepata ujuzi unaofaa kwa kazi zao kupitia mawazo, masomo na uzoefu. Kwa hiyo, ili kufikia mafanikio kamili, inatosha kujifunza na kutumia ujuzi ambao unapatikana kutoka kwa waliokutangulia. Imam Ali AS anaitaja ilmu kuwa ni turathi yenye thamani katika sehemu ya kwanza ya Hekima ya Tano ya Nahjul Balagha aliposema: “الْعِلْمُ وِرَاثَهٌ کَرِیمَهٌ: Ilmu ni urithi wenye thamani." Ni wajibu kwa kila mmoja wetu kuthamini na kukumbuka ujuzi ambao wengine walituachia kwa ukarimu wao, pamoja na yale ambayo tumeongeza juu yake kupitia ubunifu na uzoefu wetu.
Katika sehemu ya pili ya hikma hii, Imam Ali AS anasema: “وَالاْدَابُ حُلَلٌ مُجَدَّدَهٌ: Na adabu ni mapambo ambayo muda wote ni mapya. Adabu; Ni kuchunga mipaka ya kila kitu na kutochupa mipaka hiyo. Kwa mfano, mtu anapochanganya maneno yake na matusi, tunasema kwamba hana adabu, kwa sababu amechupa mstari mwekundu wa tabia ya kuzungumza na hakuheshimu mipaka yake. Katika hikma hii, Imam Ali AS amelinganisha adabu na mavazi ya mapambo. Lakini kama tujuavyo; kila nguo kuna siku lazima itachakaa. Kwa hiyo, Imam ametumia neno mujadaddah, kwa maana ya kwamba mavazi hayo yanakuwa mapya muda wote, hayachakai. Naam, kuchunga adabu katika wakati na hali zote ni kama pambo maridadi na jipya ambalo wakati wote humfanya mtu kuonekana maridadi. Kwa kweli, kuchunga maadili mema na desturi sahihi kivitendo, huongeza uaminifu wake mtu kwa wengine na hupata mafanikio mengi.
Katika kipande cha mwisho cha hikma yake hii, Imam Ali AS baada ya kuzungumzia umuhimu wa ilmu na adabu ameingia kwenye suala la kufikiri na kusema: " الْفِکْرُ مِرْآةٌ صَافِیَةٌ: Na fikra ni kioo safii kinachong'aa." Naam fikra ni kama kioo safi kinachoakisi vizuri kila kitu. Kwa hivyo, mambo yote hayo inabidi yakusanyike pamoja ili mtu uweze kupata mafanikio. Inabidi uwe na ujuzi na ufahamu wa kazi unayofanya, uzingatie adabu na heshima wakati wa kufanya kazi na pia lazima uwe na mawazo yanayojenga na fikra za maana ndipo utaweza kufikia kilele cha mafanikio. Naam, fikra ni kama kioo safi kinachoonesha kila kitu jinsi kilivyo, na kinaonesha kasoro na matatizo yote ya kazi. Pia, kwa kufikiria kwa makini katika kila kazi, matokeo na taswira yake huwekwa kwenye kioo safi cha akili na hutengeneza njia ya kufikia kilele cha mafanikio.