Hikma za Nahjul Balagha (10) + SAUTI
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 10 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya Kumi.
خَالِطُوا النَّاسَ مُخَالَطَهً إِنْ مِتُّمْ مَعَهَا بَکَوْا عَلَیْکُمْ، وَ إِنْ عِشْتُمْ حَنُّوا إِلَیْکُم
Ishini na watu kwa namna ambayo watakulilieni mkifariki dunia na mkiwa hai watapenda kusuhubiana nanyi.
Moja ya sifa za asili za mwanadamu ni kuipenda nafsi yake yaani kujipenda. Sifa hii ya kipekee ya kimaumbile ni chimbuko la vitendo vyake vingi. Hata imani ya kidini na suala la kumpenda Mwenyezi Mungu limo kwenye sifa hiyo ya kipekee ya mwanadamu, na sababu yake ni kuwa kila mwanadamu anapenda kufikia daraja za juu kabisa za ukamilifu, ufanisi na furaha. Ufanisi ambao si tu utamdhaminia maisha bora duniani, lakini pia utamuokoa siku nzito ya Kiyama.
Mwanadamu ambaye dhati yake ni kujipenda, huwa anaupa umuhimu mkubwa mtazamo wa watu kuhusu yeye. Ni muhimu sana kwake kujua watu wanamuangalia vipi. Dini tukufu ya Uislamu nayo imeipa umuhimu mkubwa mitazamo na mahitaji ya mwanadamu. Kumepokewa hadithi nyingi ambazo zinasema kama mtu atakufa na maziko yake yakahudhuriwa na waumini wa kweli 40 na wakasoma maneno haya:
اَللّهُمَّ اِنّا لا نَعْلَمُ مِنْهُ اِلاّ خَیراً وَ اَنْتَ اَعْلَمُ بِهِ مِنّا
Ewe Mola wetu sisi tunajua kheri tu kutoka kwa mtu huyu na Wewe unamjua zaidi kuliko sisi, Mwenyezi Mungu atamuelekea kwa rehema Zake mtu huyo na atasema: Ninakubaliana na ushahidi wenu na nimemsamehe yale makosa yake ambayo Mimi ninayajua na nyinyi hamyajui.

Pia imepokewa hadithi kutoka kwa Mtume Muhammad SAW akisema: Risala ya kwanza kabisa anayoandikiwa muumin baada ya kufariki dunia, ni yale mambo ambayo watu wanasema kuhusu yeye. Kama watamzungumza kwa wema, ataandikiwa mema na kama watamzungumza kwa ubaya, ataandikiwa mabaya.
Amma moja ya njia bora za kuwavutia watu na kupelekea watupende wakati wa uhai wetu na hata baada ya kufariki kwetu dunia, ni tabia nzuri. Amirul Muumini Ali Bni Abi Talib AS anasema katika hikma hii ya 10 ya Nahjul Balagha kwamba:
خَالِطُوا النَّاسَ مُخَالَطَهً إِنْ مِتُّمْ مَعَهَا بَکَوْا عَلَیْکُمْ، وَ إِنْ عِشْتُمْ حَنُّوا إِلَیْکُم
Ishini na watu kwa namna ambayo watakulilieni mkifariki dunia na mkiwa hai watapenda kusuhubiana nanyi.
Ruwaza na kigezo kamili na chema cha tabia hii nzuri ni Mtume wetu kipenzi, Muhammad al Mustafa (SAW), ambaye ni kiumbe anayependwa mno duniani tangu wakati wa uhai wake na hata baada ya kutangulia kwake mbele ya Haki, hadi hivi sasa na milele itakuwa hivyo hadi mwisho wa dunia.

Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW ni kipenzi cha viumbe wote na hasa Waislamu kiasi kwamba wakati alipokuwa akitia udhu, Waislamu walikuwa wakipigania kila mmoja kupata matone ya maji yanayodondoka kutoka kwenye viungo vyake vitoharifu. Wakati wa sulhu ya Hudaibia wakuu wa Kiquraish walimteua Urwah ibn Masʽud kuwa mjumbe wao maalumu wa kufikia mapatano na Mtume Muhammad SAW. Alipofika kwa Mtume aliona mapenzi makubwa yasiyo na kifani ya Masahaba kwa Mtume Muhammad SAW. Aliporejea kwa wakuu wa Kiquraish aliwaambia: Mimi nimeona wafalme mbalimbali wakubwa. Nimeona falme zenye nguvu kama za Kaisari wa Roma na ufalme wa Habasha, lakini hakuna hata mmoja anayemfikia Muhammad kwa mapenzi ya watu wake. Nimeona kwa macho yangu jinsi masahaba wake walivyokuwa wakipigania matone ya maji yake ya udhu na hawakuruhusu hata tone moja la maji lidondoke chini kutoka kwenye viungo vyake. Masahaba wake wanatafuta baraka zake kwa kila tone la maji yake ya udhu. Hakuna yeyote aliyeko tayari kuwa mbali naye. Enyi wakuu wa Kiquraish yazingatieni kwa kina mazingira hayo niliyoyaona. Nina wasi wasi kama mtaamua kuingia vitani naye, basi mtashindwa vibaya na kwa udhalili kabisa. Naam, huu ni mfano mmoja tu wa mapenzi makubwa aliyoyapata Bwana Mtume Muhammad SAW wakati wa uhai wake uliojaa baraka.
Hata baada ya kuondoka kwake duniani, mapenzi ya Bwana Mtume Muhammad SAW yanaongezeka siku baada ya siku kiasi kwamba hata hivi sasa, na licha ya kuweko uadui mkubwa wa makafiri, lakini mamilioni ya Waislamu wanampenda, wanamuombea dua kila siku na ni kigezo chao bora na cha juu kabisa. Mapenzi haya ya watu hayakomei kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW bali yameenea kwa yeyote anayetenda kwa usahihi tabia na maadili bora na kumfanya Bwana Mtume kuwa ndiye ruwaza yake kuu.