Jan 21, 2023 08:27 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (50)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu ya 50 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia Akhlaqi za Jihadi katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Kabla ya kuingia kwenye mada ya kipindi chetu cha leo kuna haja ya kuitolea jibu kwanza shubha na utata ambao umekuwepo tokea tangu na tangu kuhusu maudhui ya Jihadi katika Uislamu. Baadhi ya Wataalamu wa Masuala ya Ulimwengu wa Mashariki wanaojulikana kama Maorientalisti, lakini wenye kasumba na utegemezi kwa Magharibi wanajaribu kuonyesha kwamba Uislamu ni dini ya ulazimishaji na utezaji nguvu, ambayo imeenea na kusambaa duniani kwa vita na nchi ya upanga. Hoja na ushahidi chungu nzima wa kihistoria unathibitisha kwa uwazi kabisa kwamba madai hayo si sahihi na hayana ukweli wowote. Pamoja na hayo kuna udharura pia wa kutilia mkazo nukta moja ya msingi, nayo ni kwamba, madai hayo hayawezi kutufanya tuupuuze na kuufumbia macho ulazima wa kutumia nguvu kukabiliana na maadui waliodhamiria kufanya kila wawezalo ili kuuangamiza Uislamu, kama inavyoeleza sehemu ya aya ya 217 ya Suratul-Baqarah ya kwamba: "Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika Dini yenu kama wakiweza". Katika hali kama hiyo, kuna mtu gani mwenye akili timamu atakayekubali kwamba, -anapokabiliwa na maadui kama hao ambao hawawazi kitu kingine isipokuwa kutumia vitisho na nguvu za kijeshi ili kuuangamiza Uislamu na Waislamu na hawakubali hoja yoyote ya kimantiki-, asichukue hatua ya kupambana nao wala kutoa jibu lolote la kijeshi dhidi ya hujuma zao?

Kinyume na mawazo hayo potofu, Mwenyezi Mungu, Mola Mwenye hikima anawaamuru Waislamu wachukue hatua wanaposhambuliwa na maadui wasio na huruma wala mantiki na wenye chuki na vinyongo dhidi yao, kama aya ya 14 ya Suratu-Tawba inavyosema: "Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awahizi na akunusuruni muwashinde, na avipoze vifua vya kaumu ya Waumini". 

Kwa muda wote wa miaka 10, ambayo Nabii Muhammad SAW aliipitisha katika mji wa Makka baada ya kubaathiwa na kupewa Utume, licha ya kuandamwa na kila aina ya vitisho, vikwazo, ususiaji, maudhi na mateso ya kinyama ya mamwinyi na vinara wa shirki na ukafiri, Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu alitumia hoja za kimantiki tu kukabiliana na kina Abu Sufyan na kina Abu Lahab na Abu Jahal sambamba na kuwaasa wafuasi wake wawe na istikama, subira na uvumilivu. Alivumilia kwa muda wa miaka mitatu mazingira magumu kabisa ya joto kali na lenye kuunguza katika Bonde liitwalo Shib Abi Talib. Aliwaagiza baadhi ya Waislamu, ambao maisha yao yalikuwa hatarini zaidi wahajiri kuelekea Uhabeshi, lakini pamoja na hayo katu hakushika upanga kupigana. Na pale ilipofika hatua ya maadui waliomkamia kula njama ya kuivamia nyumba yake wakati wa usiku ili kumuua, aliihama Makka kwa amri ya Mola wake, akahajiri na kuhamia Madina. Kipindi hicho cha historia chenye kumbukumbu isiyosahaulika, kinadhihirisha kwamba kadiri ilivyowezekana, Bwana Mtume SAW alitumia njia za hoja na mantiki katika kuwalingania wito wa Tauhidi na imani ya Mungu Mmoja pekee wa haki waabudu masanamu, majahili na watu wapotofu waliokuwa wakiabudu hawaa na matamanio ya nafsi zao. Na ushahidi wa hilo ni aya ya 108 ya Suratu-Yusuf ambayo inasema: "Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua - mimi na wanao nifuata".

Kwa upande mwingine, Mwenyezi Mungu Mtukufu akambainishia Mtume wake mbinu ya kuitangaza na kuisambaza dini yake kama aya ya 125 ya Suratu-Nahl inavyoeleza ya kwamba: "Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka".

Mbinu hii ya kimsingi na kimantiki iliendelea mpaka kilipomalizika kipindi cha Bwana Mtume SAW kulingania Uislamu Makka na kuanza kipindi cha Hijra na kuhamia Madina. Maashrafu na mamwinyi wa Kikureishi, ambao walibaini kuwa mipango na njama zao zote za kiuadui zimefeli na kugonga mwamba baada ya Bwana Mtume kuhama Makka, walijitosa kwenye medani ya vita vilivyolenga kuusambaratisha, na kwa dhana yao, kuufuta moja kwa moja Uislamu. Kuanzia kipindi hicho ndipo zilipoanza zama mpya, kwa sababu hakukuwa na njia wala mbinu nyingine ya kutumia isipokuwa kuingia kwenye mapambano ya kukabiliana na maadui wasio na mantiki na wasio tayari kwa jengine lolote lile zaidi ya vita. Na hapo ndipo Mwenyezi Mungu alipowatangazia Waislamu njia na mbinu mpya ya kutumia kwa ajili ya kukabiliana na maadui wa dini yao, kama aya ya 29 ya Suratu-Tawba inavyosema: "Piganeni na wasio muamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho, wala hawaharimishi alivyo harimisha Mwenyezi Mungu na Mtume, wala hawashiki Dini ya Haki, miongoni mwa walio pewa Kitabu, mpaka watoe kodi kwa khiari yao, hali wamet'ii".

Kwa hivyo kwa muda wote ambapo upo uwezekano wa kuwa na suluhu, amani na mapatano; na maadamu inawezekana kuwa na maelewano kupitia mazungumzo na majadiliano ya hekima na busara, Uislamu haulipi nafasi suala la kupigana vita. Lakini inapofika hadi Mfumo wa Kiislamu ukahisi kwamba adui ana dhamira ya kuwasha moto wa vita ili kufikia malengo yake yasiyo ya kibinadamu na kuyaandama mambo matakatifu ya dini na anafanya kila njia na kutumia uwezo wake wote ili kuuangamiza Uislamu na Waislamu, hapo tena huwa ni jambo la lazima kujibu mapigo kwa kuimarisha nguvu na uwezo wa kijeshi na kuingia kwenye medani ya vita na Jihadi ili kuweza kulinda kwa nguvu na uwezo kamili mipaka ya dini na usalama wa jamii ya Kiislamu. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji, niseme pia kuwa sehemu ya 50 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 51 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/