Hakika ya Uwahabi 10
Katika kipindi cha leo tunatazamia kujadili moja ya madai yanayotolewa na Mawahabi kuhusu itikadi za Uislamu, madai ambayo iwapo itathibiti kuwa ni ya kweli, basi kinyume na tulivyosema huko, Mawahabi watakuwa ndio Waislamu wa kweli na sisi wengine sote tutakuwa tumekosoa katika kuwatuhumu bila ya kuwa na hoja za kutosha.
Bismillahir Rahmanir Raheem. Tunaanza kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu ambaye ni mjuzi wa kila kitu, na salamu Zake ziwe juu yenu enyi wasikilizaji wapendwa mnaopenda kujua ukweli wa mambo.
Mjadala wetu unahusiana na hakika ya Uwahabi, na katika vipindi vilivyopita tulijadili itikadi na vitendo vyao kwa kiasi fulani na kupata kujua kuwa havina uhusiano wowote na dini tukufu ya Uislamu. Katika kipindi cha leo tunatazamia kujadili moja ya madai yanayotolewa na Mawahabi kuhusu itikadi za Uislamu, madai ambayo iwapo itathibiti kuwa ni ya kweli, basi kinyume na tulivyosema huko, Mawahabi watakuwa ndio Waislamu wa kweli na sisi wengine sote tutakuwa tumekosoa katika kuwatuhumu bila ya kuwa na hoja za kutosha.
*************
Wafuasi wa Muhammad bin Abdul Wahhab au kwa jina mashuhuri zaidi Mawahabi, hudai kuwa wao ni wafuasi wa madhehebu ya Muhammad bin Hambal. Huenda baadhi ya watu wakadhani kuwa kwa kuwa baba yake Muhammad bin Abdul Wahhab alikuwa mmoja wa viongozi wa madhehebu hiyo basi Kiongozi huyo wa Mawahabi naye alikuwa mfuasi wa Ahmad bin Hambal na hivyo wafuasi wake pia ni katika madhehebu hiyo, lakini ukweli wa mambo sio hivyo. Tulithibitisha katika moja ya vipindi vilivyopita kwamba fikra za Muhammad bin Abdul Wahhab zilitofautiana sana na za babu, ndugu na hata walimu zake kwa kadiri kwamba walimu hao daima walikuwa wakimuonya na kumtaka asiseme na kujihusisha na mambo asiyoyajua. Ndugu yake mmoja pia aliandika kitabu kinachopinga fikra na mitazamo yake kuhusiana na masuala ya Uislamu.
Jambo lililowapelekea Mawahabi kuendelea kudai kuwa ni miongoni mwa Mawahambal licha ya wanazuoni wa Kiislamu kupinga madai hayo, ni hatua ya Ahmad bin Hambal kushikilia maana ya dhahiri za Aya na Hadithi kupita kiasi. Ahmad Bin Hambal alikuwa mmoja wa wapokezi wa Hadithi wa Kisuni aliyeishi katika karne ya pili Hijiria. Alifanya juhudi kubwa katika kukusanya na kuhifadhi Hadithi kadiri kwamba baadhi ya watu walidai kuwa alihifadhi Hadithi milioni moja na hilo kumpelekea kuitwa kuwa Imamu wa Wapokezi wa Hdithi.
Alizipa umuhimu mkubwa suna za Mtume (saw) na kauli za masahaba na wafuasi wao na akizifanyia kazi kidhahiri tu Aya za Qur'ani na Riwaya za Mtume (saw). Ahmad bin Hambal alipinga vikali hatua yoyote ya kutafsiri na kufafanuliwa Aya hizo. Alijitahidi kuthibitisha maana ya itikadi kwa msingi wa Riwaya na kutokubali hoja za kiakili na kimantiki katika uwanja huo. Daima alikuwa akiwasihi wafuasi wake kufuata nyenendo na suna za masalafi wema na ndio maana wafuasi wake wakajiita kuwa ni masalafi. Neno salafi lina maana ya mtu wa zamani na hivyo usalafi una maana ya kufuata tamaduni na nyendo za watu waliotutangulia.
Licha ya Mawahabi kudai kuwa wanawafuata watu wa zamani na wa mwanzo wa Uislamu lakini ni wazi kuwa wanafanya kinyume na alivyofundisha Ahmad bin Hambal. Moja ya tofauti kubwa zilizopo kati ya Ahmad bin Hambal na Mawahabi ni kuwa licha ya kuwa alikuwa akiamini dhahiri ya Aya, lakini alipofika kwenye Aya mithili ya zile zinazozungumzia 'mkono' au 'uso' wa Mwenyezi Mungu, kamwe hakufikia uamuzi kwamba Mwenyezi Mungu ana mwili wa kimaada unaofanana na wa mwanadamu kwa sababu alitambua vyema kuwa dhihiri ya Aya nyingine zinasema kuwa hakuna chochote kinachofanana na Mwenyezi Mungu. Hivyo aliamini kuwa Mwenyezi Mungu hafanani na kiumbe chochote kile.
Abul Fadhl Baihaqi anaamini kuwa Ahmad bin Hambal alikuwa akipinga itikadi ya Mwenyezi Mungu kuwa na mwili wa kimaada na kusema: 'Majina yametokana na sheria na lugha ambapo wajuzi wa lugha huvipa vitu majina kwa msingi wa urefu, upana, umbo, mfumo na sura katika hali ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu ametukuka na kujitenga na vitu hivyo. Hivyo haijuzu kumfungamanisha Mwenyezi Mungu na kiwiliwili.'
Tofauti nyingine muhimu iliyopo kati ya Mahambal na Mawahabi ni kuhusu fikra na tabia ya kuwakufurisha Waislamu. Licha ya kuwa Ahmad bin Hambal alikuwa na fikra zilizotofautiana na za Waislamu wengine na baadhi ya wakati akisumbuliwa na watawala wa Bani Abbas kutokana na fikra hizo, lakini hakuwa akiwakufurisha Waislamu wenzake waliotofautiana naye kifikra. Yeye na wafuasi wake hawakuwa wakiituhumu miji ya Waislamu kuwa ni miji ya kufri wala kuwatuhumu Waislamu wanaozuru kaburi takatifu la Mtume (saw) ua ya viongozi wengine wema wa dini kuwa ni makafiri na washirikina.
Baadhi ya vyanzo vya kihistoria vinathibitisha wazi kuwa licha ya kwamba Ahmad bin Hambal alikuwa akiamini dhahiri ya Aya na kupinga kutafsiriwa vingine Aya hizo lakini yeye mwenyewe alikuwa akitafsiri baadhi ya Aya hizo na kutoa maana iliyotofautiana na dhahiri ya Aya hizo. Kwa mfano tunasoma katika Aya ya 22 ya Surat al-Fajr kama ifuatavyo: 'Na akaja Mola wako na Malaika safu safu.' Dhahiri ya Aya hii inaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu anatembea na kufanya aina fulani ya harakati, lakini Ahmad bin Hambal ameifasiri kwa maana ya 'kuja kwa amri au thawabu.' Tafsiri hii mbali na kuwa inapinga Mwenyezi Mungu kuwa na kiwiliwili bila shaka inathibitisha kutumiwa akili katika kufahamu maana halisi na sahihi ya Aya. Kwa msingi huo hatuwezi kudai kuwa Ibn Hambal alitupilia mbali umuhimu wa akili na kutaja matumizi yake katika kufasiri maana halisi ya Aya kuwa ni bida'.
*************************
Licha ya uwepo wa tofauti hizi zote, lakini ni wazi kuwa hatua ya Ahmad bin Hambal ya kupinga matumizi ya akili au tusema, hatua yake ya kuamua kutumia akili katika sehemu chache sana za kutafsiri maana ya Aya za Qur'ani Tukufu, ziliwapelekea wafuasi wake akiwemo Ibn Taymiyya kutafsiri kidhahiri baadhi ya sifa za Mwenyezi Mungu na hatimaye kudai kuwa ana kiwiliwili kinachofanana na cha mwanadamu. Tunaweza kusema kuwa itikadi potofu ya Ibn Taymiyya ambayo ilitokana na kutazama mambo kijuujuu tu inatokana na aina fulani ya upotofu ulioonekana kwenye itikadi za Ahmad bin Hambal. Upotofu huo ulipingwa vikali na wanazuoni wa Kiislamu katika siku zilezile za mwanzoni na ndio maana ukampelekea Ibn Taymiyya kupitishia sehemu kubwa ya umri wake kwenye jela.
Kwa bahati mbaya moja ya sababu kuu za madhara na matatizo yanayoikumba jamii ya Kiislamu leo hii ni tatizo hili la kuitazama mambo kidhahiri na kijuu juu tu bila kuzingatia kina chake. Jambo hilo mdilo lililopelekea itikadi potofu za Mayahudi au kwa ibara nyingine Israeliyaat kuenea miongoni mwa Waislamu tangu mwanzoni mwa Uislamu. Ni vipi tutawataka Waislamu wasitumie akili katika hali ambayo sisitizo la kutumiwa akili katika uzingatiaji wa alama na maumbile ya Mwenyezi Mungu, limekaririwa kwa njia moja au nyingine zaidi ya mara mia tatu (300) katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani?!! Katika Aya nyingi za kitabu hiki kitukufu, Mwenyezi Mungu anawataka waja wake kutumia akili katika mambo wanayoyafanya na wakati huo huo kuwakemea wale wasiotumia akili katika maamuzi wanayoyachukua maishani. Mwenye kufikiria na asiyejua na vile vile Aalim na jahili hawawi sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Sehemu ya Aya ya 50 ya Surat al-An'am inasema:........Je, wanakuwa sawa, kipofu na mwenye kuona. Basi hamfikiri?
Katika Aya ya 36 ya Surat Israa, Mwenyezi Mungu anawakataza watu kufuata mambo wasiyoyajua. Anasema: Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo.
Katika sehemu ya Aya ya 100 ya Surat Yunus, Mwenyezi Mungu huwajaalia uchafu wale wasiotumia akili. Anasema: Na hujaalia achafu kwa wale ambao hawatumii akili.
***************
Sisi sote tunajua vyema kwamba Uislamu ni dini iliyokamilika katika kila upande na wala haijaacha nje wala kughafilika na mambo yanayomkamilisha mwanadamu na hasa uwezo wake wa kutafakari na kuchambua mambo kwa kutumia akili aliyopewa na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ni vipi dini hii tukufu ya mbinguni inaweza kupuuza umuhimu na neema hii kubwa ya akili na kutaka kuikandamiza?! Tunasoma katika Aya ya 108 ya Surat Yusuf kama ifuatavyo: Sema: Hii ndiyo Njia yangu ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua, mimi na wanaonifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina. Katika zama za uhai wake humu duniani, Mtume Mtukufu (saw) mara nyingi alikuwa akiwataka wafuasi na masahaba zake kutumia akili na kutafakari kwa kuwaambia: 'Saa moja ya mtu anayetafakari ni bora kuliko miaka sabini ya ibada inayofanywa bila kutafakari.'
Kimsingi Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa wanafikra wakubwa zaidi katika zama zao na bila shaka kutafakari kwao ni moja ya sifa zilizowapelekea kuteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa mfano bora wa kuigwa na kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu kwenye njia sahihi inayowadhaminia saada humu duniani na huko Akhera. Ni wazi kuwa kiwango chetu cha kufikiria na kutafakari ni kidogo na wala hakiwezi kulinganishwa na cha Manabii, lakini pamoja na hayo hilo halituzuii kufanya juhudi kadiri ya uwezo wetu ili tunufaike na akili katika kutambua hakika ya dini. Wakati huo huo hilo halipasi kutufanya tukate tamaa kuwa hatuna uwezo kabisa wa kujua na kufahamu maneno ya Mwenyezi Mungu kwa kutumia akili. Kama hali ingekuwa ni hivyo, Mitume hawangetumwa kwetu kama mifano bora ya kuigwa na kufuatwa na wanadamu, bali lingekuwa ni jambo lisilo na busara wala maana, na bila shaka jambo lisilo na maana haliwezi kunasibishwa na Mwenyezi Mungu. Kwa ibara nyingine ni kuwa Mwenyezi Mungu Mjuzi na Mwenye Hekima hafanyi jambo ila kwa lengo maalumu.