Mar 22, 2023 02:24 UTC
  • Jumatano, tarehe 22 Machi, 2023

Leo ni Jumatano tarehe 29 Shaaban 1444 Hijria sawa na 22 Machi mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 1225 iliyopita inayosadifiana na 29 Shaaban 219 Hijria, alifariki dunia Ibn Naeem mtaalamu wa elimu ya hadithi, faqihi na mpokezi wa riwaya za kihistoria. Msomi huyo alizaliwa nchini Iraq, na anahesabiwa kuwa mmoja wa wapokezi wenye itibari, mwenye kuheshimiwa na mwenye kuaminiwa kati ya maulamaa wa Kiislamu.

Siku kama hii ya leo miaka 1126 iliyopita alifariki dunia Ibn Mundhir faqihi, mfasiri na mpokeaji hadithi wa Kiislamu. Ibn Mundhir alijifunza masomo ya fiqih na hadithi kwa wasomi watajika wa zama zake. Ibn Mundhir aliishi katika mji wa Makka hadi mwisho wa maisha yake baada ya kuwasili mjini humo kwa lengo la kuzidisha elimu na maarifa ya kidini. Msomi huyo wa Kiislamu aliandika vitabu kadhaa akiwa Makka. Kitabu alichokipa jina la al Ashraaf ni moja ya vitabu vya msomi huyo ambacho ndani yake ameonyesha kipawa na elimu aliyokuwanayo katika taaluma ya hadithi. 

Siku kama ya leo miaka 142 iliyopita lilianzishwa Muungano wa Soka wa Kimataifa  kwa shabaha ya kusimamia mashindano ya mpira wa miguu kote duniani. Kabla ya kuundwa muungano huo, mashindano ya soka yalikuwa yakifanyika katika nchi mbalimbali kwa muundo usiokuwa rasmi. Muungano huo ulibadilisha muundo wake na kujulikana baadaye kwa jina la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na liliandaa pambano rasmi la kwanza la kimataifa mwaka 1901, kati ya Uingereza na Ujerumani.

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, yaani sawa na tarehe 22 Machi 1945, iliundwa Jumuiya ya Waarabu kutokana na mapendekezo ya Farouk,  aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Misri na kutiwa saini makubaliano ya kuundwa jumuiya hiyo na serikali za Syria, Iraq, Saudi Arabia, Misri na Yemen mjini Cairo. Lengo la kuanzishwa jumuiya hiyo lilikuwa ni kuhifadhiwa ardhi zote, kujitawala nchi wanachama na kuwepo ushirikiano wa karibu wa kisiasa kiuchumi na kiutamaduni kati ya nchi hizo.

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita aliuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwanachuoni na mwasisi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas pamoja na watu wengine 10. Sheikh Ahmad Yassin aliuawa shahidi baada ya kumaliza swala ya Alfajiri katika msikiti mmoja ulioko eneo la Ukanda wa Gaza, wakati aliposhambuliwa na helikopta za utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheikh Ahmad Yasin aliasisi harakati ya Hamas mwaka 1987 akishirikiana na wanamapambano wengine kadhaa wa Kipalestina na miaka miwili baadaye alifungwa jela na utawala ghasibu wa Israel. Mauaji ya mpigania uhuru huyo ambaye alikuwa kiwete na kipofu wakati wa kuuawa kwake, yalidhihirisha tena ugaidi wa kiserikali wa utawala haramu wa Israel.

Sheikh Ahmad Yassin

Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, ilianza operesheni kubwa ya 'Fat-hul Mubiin' ya wapiganaji shujaa wa Kiislamu huko kusini magharibi mwa Iran kwa shabaha ya kuyarejesha nyuma majeshi vamizi ya Iraq. Kwenye operesheni hiyo iliyopelekea kukombolewa miji ya Dezful, Andimeshk, Shush na mamia ya vijiji vya eneo hilo, wanajeshi wasiopungua elfu 25 wa Iraq waliuawa na wengine elfu 15 kukamatwa mateka.