Mar 30, 2023 02:43 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 30 Machi, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 8 Ramadhani 1444 Hijria sawa na 30 Machi 2023.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kulianza kufanyika kura ya maoni ya nchi nzima kwa lengo la kuainisha mfumo utakaotawala hapa nchini. Kura hiyo ya maoni ya kihistoria ilifanyika kwa muda wa siku mbili kutokana na kupokelewa kwa wingi na wananchi wa Iran. Asilimia 98.2 ya wananchi Waislamu wa Iran, walipiga kura ya kutaka mfumo wa Kiislamu utawale hapa nchini. 

Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, alifariki dunia mwanachuoni mkubwa wa Iran, Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi, mmoja wa wasomi mashuhuri wa Iran. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alielekea mjini Najaf Iraq na kupata kusoma kwa walimu wakubwa wa kidini wa mji huo, kisha akarejea nchini Iran. Ayatullah Burujerdi kwa kushirikiana na wanachuoni wengine wakubwa wa Kiislamu alianzisha Umoja wa Ukurubisho wa Madhehebu ya Kiislamu. Ayatullah Burujerdi licha ya kuandika vitabu kadhaa, alijenga misikiti kadhaa ndani na nje ya Iran, ukiwemo Msikiti wa Hamburg nchini Ujerumani.

Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi

Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, maandamano makubwa ya "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa tarehe 18 Oktoba mwaka 1975 mkutano wa kutetea ardhi ulifanyika katika eneo la Jalil kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika azimio la kwanza la mkutano huo, washiriki walieleza kusikitishwa kwao na hatua ya utawala wa Kizayuni ya kughusubu ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina na kulaani vikali hatua hiyo. Mkutano wa Jalil ulisisitiza kuwa, siasa za utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu zinakiuka haki za wananchi Waislamu wa Palestina katika ardhi zao na kwamba, utawala wa Kizayuni umepuuza wazi wazi hati ya haki za binadamu na misingi ya demokrasia na usawa. 

Yaumul Ardh

Na siku kama ya leo miaka 156 Russia iliiuzia serikali ya Marekani ardhi yenye utajiri ya Alaska inayopatikana huko kaskazini magharibi mwa Canada na katika pwani ya bahari za Pacific na Arctic. Russia iliiuza ardhi ya Alaska kwa Marekani kwa thamani ya dola milioni saba na laki mbili kutokana na mahitaji ya kifedha iliyokuwanayo. Alaska ni jimbo la 49 la Marekani lenye ukubwa wa kilomita mraba zaidi ya milioni moja. Jimbo la Alaska pia lina thamani kubwa za kiuchumi kutokana na kuwa na maliasili nyingi za madini, khususan mafuta na dhahabu pamoja na mapato yanayotokana na uvuvi wa samaki. 

 

Tags