Apr 01, 2023 22:51 UTC
  • Jumapili, 02 Aprili, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 11 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1444 Hiijria, mwafaka na tarehe Pili Aprili 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 591 iliyopita, alifariki dunia mjini Cairo Ibrahim Karaki, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na Hadithi wa Kiislamu. Baada ya kusoma Qur'ani na masomo ya awali ya kidini, Ibrahim Karaki alianza kufanya safari katika maeneo mbalimbali katika vituo vya elimu ya kidini kwa lengo la kukamilisha masomo yake ya juu kama vile fiqihi na fasihi ya lugha ambapo alifanikiwa kufikia daraja ya juu katika uwanja huo. Kitabu cha I'rabul-Mafsal ni miongoni mwa athari zilizoachwa na msomi huyo. ***

Ibrahim Karaki

 

Katika siku kama ya leo miaka 218 iliyopita, alizaliwa huko nchini Denmark, Hans Christian Andersen malenga, mwandishi na msimulizi wa visa maarufu vya watoto. Andersen ambaye alikuwa mtoto wa bwana mmoja maskini na fundi viatu, alihamia Copenhagen mji mkuu wa Denmark na kuanza kucheza michezo ya kuigiza. Baada ya muda, Hans Andersen alianza kutunga visa na kuwa mashuhuri baada ya kuandika kitabu chake cha kwanza cha hadithi alichokipa jina la "Fairy Tales, Told for Children" mnamo mwaka 1838. ***

Hans Christian Andersen

 

Miaka 41 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya jeshi la majini la Argentina vilivamia visiwa vya Falkland kwa jina jingine (Malvinas) na kuvidhibiti visiwa hivyo vya kiistratejia vilivyoko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Visiwa vya Falkland ambavyo kwa lugha ya Kiargentina vinatamkwa kama Malvinas, viligunduliwa katika karne ya 16 na kukaliwa kwa mabavu na Uingereza mwaka 1832. ***

 

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, vibaraka wa utawala wa Baath uliokuwa ukiongozwa na Saddam Hussein walivamia na kuvunjia heshima Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib A.S katika mji mtakatifu wa Najaf na ya Imam Hussein A.S huko katika mji mtukufu wa Karbala, sambamba na kuyakandamiza mapambano ya Waislamu wa kusini mwa Iraq. Wananchi wa Iraq walianzisha mapambano ya kuuondoa madarakani utawala wa kidikteta Saddam Hussein baada ya muungano wa vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa kutekeleza oparesheni ya kuwaondoa wanajeshi wa Iraq katika ardhi ya Kuwait. Wakati huo wanajeshi wa Marekani walisitisha oparesheni zao za kijeshi na kuungana na wanajeshi wa Saddam ili kumwaga damu za Wairaqi waliokuwa wakiendesha mapambano huku wakiwa kwenye saumu. ***

 

Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, aliaga dunia Papa John Paul II aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani. Papa John Paul II alizaliwa mwaka 1920 huko Poland na kufikia daraja ya uchungaji baada ya kuhitimu masomo ya dini. Mwaka 1964 Papa John Paul alikuwa askofu wa mji wa Kraku huko Poland na miaka mitatu baadaye akawa Kadinali. Hatimaye mwaka 1978 John Paul wa Pili aliteuliwa kushika wadhifa wa ngazi ya juu zaidi wa kanisa Katoliki, yaani Papa. Papa John Paul wa Pili alikuwa mfuasi wa mazungumzo baina ya dini mbalimbali hususan kati ya Uislamu na Ukristo. Alikuwa akipinga vikali utoaji mimba na ndoa za watu wa jinsia moja na ufisadi wa kimaadili kwa ujumla uliotanda katika ulimwengu wa Magharibi. Aidha alikosoa vikali mashambulio ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iraq. ***

Papa John Paul II