Jumatatu, tarehe 3 Aprili, 2023
Leo ni tarehe 12 Ramadhani mwaka 1444 Hijria sawa na tarehe tatu Aprili 2023.
Siku kama ya leo yaani tarehe 12 Ramadhani kwa mujibu wa baadhi ya wapokezi wengi, ni siku ambayo Nabii Issa Ibn Maryam, Masih AS aliteremshiwa kitabu kitukufu cha Injili. Neno Injili ni la Kigiriki na lina maana ya bishara. Jina hilo limetajwa mara 12 katika Qur’ani Tukufu na kitabu hicho kinaitambua Injili kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SW chenye sheria na kanuni za mbinginu. Hata hivyo kitabu kinachojulikana hivi sasa kwa jina la Injili si kile kilichoteremshwa kwa Nabii Issa Masih bali ni riwaya na kumbukumbu zilizokusanywa na wanafunzi wake baada ya Yeye kupaa mbinguni.
Siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita yaani tarehe 12 Ramadhani mwaka wa kwanza Hijria, muda mfupi baada ya Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kuhama Makka na kuelekea Madina, aliunga udugu baina ya Muhajirina na Ansar. Muhajirina ni watu ambao walihama na Mtume (SAW) kutoka Makka kwenda Madina, na Ansar ni Waislamu wa Madina waliowakaribisha Muhajirina katika mji huo. Kwenye sherehe hiyo ya kuunga udugu bina ya Waislamu, Mtume (SAW) alimtangaza Ali bin Abi Talib (AS) kuwa ndugu yake hapa duniani na Akhera.

Tarehe 12 Ramadhani miaka 847 iliyopita, alifariki dunia Ibn Jawzi, faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi katika karne ya 6 Hijria. Ibn Jawzi alizaliwa mwaka 510 Hijria na kufanya safari nyingi kwa ajili ya masomo. Mbali na kubobea katika masuala ya elimu ya fiq'hi na hadithi, alikuwa mtaalamu katika uwanja wa kutoa mawaidha na hata akaweza kuaminiwa na maulamaa wakubwa wa zama zake. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na mashuhuri zaidi ni Al Muntadhim na Mawaidhul Muluk.

Katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Mahdi Khalisi, faqihi na mujtahidi mkubwa wa zama hizo. Ayatullah Khalisi alizaliwa huko Kadhimiya nchini Iraq mwaka 1277 Hijiria na akiwa kijana alijishughulisha na kuamrisha mema na kukataza maovu sambamba na kustahamili shida nyingi kipindi cha masomo na kutafuta elimu. Katika kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia, msomi huyo akishirikiana na baadhi ya mujtahid wa Iraq, alianzisha mapambano dhidi ya uvamizi wa wakoloni Waingereza nchini humo. Baada ya muda alirejea nchini Iran na kujishughulisha na kazi ya ualimu na kufunza elimu za kidini. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa ni Kifayatul Usuul na Anawinul Usul.
Siku kama ya leo miaka 133iliyopita Otto Von Bismarck mmoja kati ya shakhsia waliokuwa na nguvu na ushawishi mkubwa katika karne ya 19 barani Ulaya na Kansela wa Ujerumani, alivuliwa madaraka na Kaiser Wilhelm II aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Ujerumani. Licha ya kuondolewa madarakani, aliendelea kubaki kwenye wadhifa huo kwa muda mchache, lakini baada ya kushadidi hitilafu kati yake na Mfalme Wilhelm II, Bismarck alilazimika kujiuzulu. Bismarck alifariki dunia mwaka 1898.
Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Aprili 1941, mji wa Baghdad ulikombolewa na Rashid A'li Gilani kiongozi wa mrengo uliokuwa ukiwapinga Waingereza, baada ya kujiri mapigano kati ya wazalendo wenye uchungu wa nchi yao dhidi ya serikali ya London. Gilani alikuwa akiungwa mkono na Ujerumani na kutokana na kutopata misaada kwa wakati mwafaka, vikosi vya Uingereza vilifanikiwa kuwakandamiza wafuasi wa wake. Baada ya tukio hilo serikali ya Iraq ilijiunga na nchi waitifaki katika Vita vya Pili ya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 21, iliyopita, yaani sawa na tarehe 3 Aprili 2002, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, katika ardhi za Palestina. Mashambulio hayo yalikuwa mwendelezo wa mashambulizi ya wiki kadhaa ya Wazayuni kwenye eneo hilo, kwa shabaha ya kuzima Intifadha ya wananchi wa Palestina. Kwenye mashambulio hayo ya majeshi ya Wazayuni huko Jenin, asilimia 70 ya mji huo ilibomolewa kabisa, mamia ya Wapalestina kuuawa shahidi na watu wengine wasiopungua 5,000 kukosa makazi.