May 31, 2023 09:59 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (19)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 19 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 19.

مَنْ جَرَى فِی عِنَان أَمَلِهِ، عَثَرَ بِأَجَلِهِ

Anayetekwa na tamaa yake, kifo kitamwangamiza.

Moja ya mada muhimu na inayojirudia katika Nahj al-Balagha ni matumaini na tamaa. Tamaa na matumaini ni injini ya harakati za mwanadamu. Mtu ambaye hana ndoto wala matamanio na matumaini, huwa hana msukumo wala mori wa kuendelea na maisha wala kufanya juhudi za kuboresha maisha yake. Kama inavyosemwa; Mwanadamu anaishi kwa matumaini. Neno hili limechukuliwa kutoka katika Hadith ya Mtume Mtukufu SAW inayosema: "Matumaini ni rehema kwa umma wangu, na bila ya matumaini, hakuna mama angenyonyesha mwanawe wala mkulima angeotesha mmea." Matumaini ni rehema kwa umma wangu na kama kusingekuwa na matumaini na matamanio, hakuna mama ambaye angemnyonyesha mtoto wake na hakuna mtunza bustani ambaye angepanda miche na kuotesha miti na mimea.

Mama ni ishara ya mapenzi na wema, lakini kinachomfanya mama kuwa mkarimu, na kufanya mvua ya wema wake inyeshe, ni matumaini. Ikiwa siku moja wataondoa matumaini ndani ya moyo wa mama, hatakuwa tayari hata kumnyonyesha mtoto wake mpendwa na hatafanya jitihada wala hatakuwa na moyo wowote wa kujitolea kwa namna yoyote ile kumshughulikia mwanawe. Imepokewa Hadith kutoka kwa Nabii Isa AS kwamba siku moja alikuwa amekaa mahali akamuona mzee mmoja ameshughulika kuchimba ardhi kwa kutumia jembe na sururu. Nabii Isa AS alimwelekea Mola wake, akamuomba kwa kusema: Ewe Mola wangu, mpokonye matumaini mzee huyu. Ghafla yule mzee aliweka chini jembe na sururu na kujitupa chini akalala. Baadaye kidogo Nabii Isa AS alimuomba tena Mola wake akisema: Ewe Mola wangu, mrejeshee mzee huyu matumaini na hamu ya maisha. Mara alimuona yule mzee amenyanyuka na kuanza tena kufanya kazi kwa bidii. Nabii Isa AS alimfuata yule mzee na kumuuliza mbona hapa nimekuona katika hali mbili tofauti kabisa? Mara moja nimekuona umetupa chini jembe na sururu na kujibwaga chini ukalala, lakini muda haukupita nimekuona umenyanyuka na kuendeleza kufanya kazi kwa bidii? Yule mzee alijibu kwa kusema: Kwanza ilinipitikia akilini kwamba mimi ni mzee tena na ni mtu dhaifu, kwa nini nijisumbue vyote hivi? Ndio maana niliweka pembeni jembe na sururu yangu na kujilaza chini. Lakini hapo hapo imenipitikia akili kwamba nani anayejua, huenda muda wangu uliobakia wa kuishi hapa duniani ni mrefu. Na maadamu mtu yuko hai, lazima afanye kazi kwa bidiii kwa ajili yake na familia yake. Hivyo nimeinuka na kuchukua sururu na jembe na kuendelea na kazi.

Kwa hakika ni matumaini ndiyo ambayo yanaleta nishati kwa mwanadamu. Lakini kuna jambo jingine la msingi nalo ni kwamba kila jambo ambalo ni fursa linaweza wakati huo huo kuwa tishio pia. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kwamba, jambo lolote jema linaweza kuwa baya na hatari lisipotumiwa ipasavyo. Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS katika hikma hii ya 19 ya Nahjul Balagha anatutahadharisha na madhara ya tamaa ambayo ni sehemu ya matumaini akitutaka tudhibiti tamaa zetu. 

Katika hikma hii ya 19 ya Nahjul Balagha, Imam AS AS anasema: 

مَنْ جَرَى فِی عِنَان أَمَلِهِ، عَثَرَ بِأَجَلِهِ

Anayetekwa na tamaa yake, kifo kitamwangamiza.

Katika Kiswahili pia tuna msemo unaosema; Tamaa mbele, mauti nyuma. Katikak hikma hii, Imam Ali AS anatukumbusha kwamba ndoto za uwongo na zisizo za kweli humburuza mtu kwenye maangamizi na kumpotezea mtu mtaji bora wa maisha na ujana wake. Wakati mwingine hata humpotezea heshima yake na mwisho wa siku hata asiweze kufikia ndoto zake. Kwa hakika, ndoto za alinacha ambazo haziko kwenye upeo wa uwezo wetu ni kama sarabii na mazigazi yanayomtia matumaini mwenye kiu akadhani kuna maji lakini kila akifika hapati maji yoyote ghairi ya huzuni na majuto na kutumbukia kwenye shimo la maangamizi.