Jul 15, 2023 02:47 UTC
  • Jumamosi, 15 Julai, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1444 Hijria mwafaka na tarehe 15 Julai 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 885 iliyopita alizaliwa huko katikati mwa Iraq Abul-Fadhail Amedi fakihi na mwanafasihi wa Kiislamu. Baada ya kusoma elimu za fiqhi, Usul Fiqhi, fasihi na hisabati katika mji wa Baghdad aliondokea kuwa mahiri katika elimu hizo. Abul Fadhail Amedi alikuwa na mashairi yenye kubeba maana kubwa. Amedi aliaga dunia akiwa katika eneo alilozaliwa akiwa na umri wa miaka 49. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 435 kulitokea vita vya Bahari ya Manche (English Channel) kati ya jeshi la majini la Uhispania maarufu kama Jeshi la majini lisiloshindwa na jeshi la majini la Uingereza. Katika vita hivyo meli kubwa 135 za kivita za Uhispania ziliishambulia Uingereza kwa shabaha ya kulipiza kisasi cha mauaji ya malkia Mary Stuart wa Scotland lakini kutokana na kimbunga kikali meli 85 za Uhispani zilizama majini na kikosi cha jeshi la majini kisichoshindwa cha Uhispania kikapata kipigo kikubwa. Tangu wakati huo nyota na umashuhuri wa kikosi hicho ukaanza kuzama. ***

 

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, alifariki dunia Anton Chekhov, mwandishi mashuhuri wa visa wa karne ya 19 wa Urusi akiwa na umri wa miaka 64. Chekhov alikuwa tabibu na katika kujitolea alijenga kituo cha tiba ambacho alikitumia katika shughuli hiyo. Baada ya hapo alijiunga na taaluma ya uandishi ambapo alianza kujishughulisha na kazi za uandishi katika magazeti na kuandika makala tofauti wakati huo. Alikuwa mahiri katika tenzi fupifupi na akatokea kuwa mashuhuri katika uga huo. Miongoni mwa athari za mwandishi huyo ni pamoja na kitabu cha "Jogoo wa Bahari". ***

 

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1318 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo katika shule ya sekondari, alijikita zaidi katika masomo ya kidini kutoka kwa baba yake, na kupiga hatua kubwa ya kielimu katika kipindi kifupi. Ayatullah Khamenei alielekea Qum kwa masomo ya juu ya kidini na kupata fursa ya kunufaika na elimu kutoka kwa maulamaa wakubwa katika mji huo, kama vile Imam Ruhullah Khomeini, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai katika masomo ya fiqh, usululi na falsafa. Akiwa bado kijana, Sayyid Khamenei alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi dhidi ya utawala kibaraka wa Shah hapa nchini, na mara kadhaa alitiwa mbaroni, kutumikia vifungo na hata kupelekwa uhamishoni. Baada ya kufariki dunia Imam Khomeini MA mwaka 1368 Hijria Shamsia, Baraza la Wanachuoni linalomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran, lilimchagua Ayatullah Khamenei, wakati huo akiwa rais wa nchi, kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. ***

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei

 

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita yaani tarehe 15 Julai mwaka 1944, jeshi la Marekani lilianza kuishambulia Japan kwa maelfu ya mabomu katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulio hayo ya mabomu ya Marekani yaliendelea hadi Japan iliposalimu amri. Tukio hilo chungu licha ya kusababisha makumi ya maelfu ya wananchi wasio na hatia wa Japan kuuawa kwa halaiki, lilipelekea pia zaidi ya viwanda elfu tatu vikubwa kwa vidogo kuharibiwa kabisa. ***

Vita vya Pili vya Dunia

 

Katika siku kama ya leo miaka 55 iliyopita yaani tarehe 24 Tir mwaka 1347 Hijria Shamsia, Ismail Balkhi mwanamapambano na mwanafikra wa Kiafghani aliuawa shahidi mjini Kabul. Alizaliwa katika kijiji kimoja kaskazini mwa Afghanistan. Alianza kusoma kwa bidii masomo ya dini tangu akiwa mdogo na kipindi fulani alifanya safari nchini Iran na Iraq, lengo likiwa ni kujiendeleza zaidi kielimu. Ismail Balkhi alikuwa akiendesha mapambano dhidi ya udikteta na daima alikuwa akiwashajiisha wananchi Waislamu wa Afghanistan kupambana na tawala dhalimu. Kutokana na harakati hizo, shahidi Balkhi alikuwa chini ya mashinikizo ya watawala wa wakati huo wa Afghanistan, na kwa miaka kadhaa alifungwa jela. ***

Ismail Balkhi

 

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1389 Hijria Shamsia, kwa akali watu 27 waliuawa na wengine 169 kujeruhiwa kwenye milipuko miwili ya mabomu iliyotokea katika mji wa Zahedan, ulioko kusini mashariki mwa Iran. Milipuko hiyo ilitokea mkabala na Msikiti Mkuu wa Zahedan, wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib (as) mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Kikundi cha kigaidi kilichojiita Jundullah, ndicho kilichotekeleza shambulio hilo la kigaidi. ***

 

Tags