Amani na Usalama katika Mtazamo wa Uislamu
(last modified Sun, 25 Sep 2016 12:58:30 GMT )
Sep 25, 2016 12:58 UTC
  • Amani na Usalama katika Mtazamo wa Uislamu

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi katika kipindi cha wiki hii cha Makala ya Wiki ambacho kitazungumzia usalama na amani katika mtazamo wa Uislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani.

Tarehe 21 Septemba kila mwaka inasadifiana na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani. Siku hiyo ilipasishwa katika kikao cha 57 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alizitaka pande zote zinazopigana kote duniani kusimamisha mapigano kwa masaa 24 hapo tarehe 21 Septemba.

Amani ya Kimataifa

Sehemu moja ya ujumbe wa Ban Ki-moon imesema: Sisi sote tunajua kwamba, amani si jambo linalotokea kwa sadfa na wala si zawadi na hadia ya kupewa na mtu, bali sisi sote tunawajibika kufanya jitihada kila siku na katika kila nchi kwa ajili ya kuimarisha amani na usalama", mwisho wa kunukuu.

Inasikitisha kwamba, hii leo licha ya juhudi kubwa zinazofanywa kwa ajili ya kulinda amani na usalama wa dunia, kunashuhudiwa ongezeko la vita na machafuko katika pembe mbalimbali za dunia. Hivyo katika siku hii ya kimataifa itakuwa bora kutupia jicho tena maana ya amani na kuchunguza mafundisho ya dini ya Uislamu kuhusu amani na usalama.

Uislamu na mafundisho yake unahesabiwa kuwa mfumo kamili na muhimu zaidi wa sheria katika dunia ya leo. Mtume mtukufu wa dini hiyo, Muhammad bin Abdullah (saw) alisema tangu mwanzoni mwa kutangaza ujumbe aliopewa na Mwenyezi Mungu kwamba, lengo lake ni kusimamisha usawa na uadilifu kwa wanadamu wote.

Uislamu ni dini ya amani usalama

Dini ya Uislamu ina mitazamo inayofanana na dini nyingine za mbinguni kuhusu suala hili la amani na usalama. Katika mtazamo wa Uislamu usalama una maana ya amani na utulivu katika jamii. Katika upande mwingine, usalama na minyambuliko yake ni neno lililotumiwa mara nyingi katika aya za Qur'ani tukufu. Neno hilo na amani kwa ujumla limezungumziwa katika karibu aya 140 za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Katika mtazamo wa Uislamu, usalama na Uislamu ni maneno mawili yanayoambatana, yenye mfungamano na yasiyotengana. Wasomi wa Kiislamu wanasisitiza kuwa, maneno mawili yana maana ya amani na usalama:

Amani katika Uislamu

Kwanza ni neno "Silm" au "Al Salm" ambalo katika lugha ya Kiarabu lina maana ya utulivu, kusalimika au usalama kwa istilahi ya zama hizi. Usalama na amani vina mfungamano na Mwenyezi Mungu Muumba. Mwenyezi Muumba mwenyewe amejitaja kuwa ni "Assalam" kwa maana ya amani na Mwenye amani na salama na kwa msingi huo kila usalama na amani ni mwangwi wa dhati yake tukufu. Dhati ya mwanadamu pia daima huwa katika hali ya kustawi na kufanya harakati za kuelekea kwenye amani na utulivu kamili ambao haupatikana ila kwa amani na usalama mutlaki, yaani dhati ya Mwenyezi Mungu Muumba. Hii ndiyo siri ya falsafa ya wito wa Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu ambayo daima humlingania mwanadamu wito wa amani na usalama na kumuelekeza kwenye amani na usalama mutlaki na kamili. Aya ya 208 ya Suratul Baqara inasema:

یَا أَیُّهَا الَّذِینَ آمَنُواْ ادْخُلُواْ فِی السِّلْمِ کَافَّةً وَلاَ تَتَّبِعُواْ خُطُوَاتِ الشَّیْطَانِ إِنَّهُ لَکُمْ عَدُوٌّ مُّبِینٌ

Enyi Mlioamini! Ingieni katika usalama nyote. Wala msifuate nyayo za She'tani; hakika yeye kwenu ni adui aliyewazi.

Vilevile aya ya 61 ya Suratul Anfal inasema:

وَإِن جَنَحُواْ لِلسَّلْمِ فَاجْنَحْ لَهَا وَتَوَکَّلْ عَلَى اللَّهِ إِنَّهُ هُوَ السَّمِیعُ الْعَلِیمُ

Na (wapinzani wako) wakielekea kwenye amani nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.

Neno "Islam" pia linatokana na msingi wa neno "Silm", na kwa hakika lina maana ya kumfuata Mwenyezi Mungu ambaye Yeye mwenyewe ndiye amani na usalama mutlaki na utulivu kamili.

Neno jingine ni "sulh" ambalo lina maana na amani, maelewano na uhusiano mwema baina ya wanadamu. Uislamu umetumia neno hilo ukitaka kuwepo upendo, kuheshimiana, kujiepusha na uchokozi na uhasama na kuchupa mipaka ya wanadamu wengine.

Ili kuweza kupatikana amani na uadilifu, Uislamu umeweka safari yenye awamu tatu tofauti. Kwanza ni usalama na amani ya ndani ya nafsi. Katika awamu hii watu wote wa jamii wanatakiwa kutakasa nafsi zao na kuzipamba kwa taqwa na uchamungu. Nukta ya mwanzo ya harakati hii ni ile inayotajwa katika elimu za alkhaki na irfani kuwa jihadi ya nafsi.

Taqwa na amani ya ndani ya nafsi

Katika awamu hii, muumini anapaswa kukomesha mpambano na vita liyopo baina ya matamanio na matakwa yake ya kinafsi na yale ya kiroho, na kufikia amani na usalama wa ndani ya nafsi ili pande hizo mbili za kinafsi na kiroho ziishi pamoja kwa amani na kumsaidia mwanadamu kufikia kilele cha ukamilifu. Ni baada ya hapa ndipo mwanadamu anapokuwa tayari kwa ajili ya harakati ya kijamii na wanadamu wenzake kuelekea kwenye malengo aali na ya juu zaidi. Aya ya 103 ya Suratu Aal Imran inasema:

وَاعْتَصِمُواْ بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِیعًا وَلاَ تَفَرَّقُواْ 

Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote kwa pamoja, wala msifarikiane.

Kwa msingi huo amani ya ndani ya nafsi ndiyo msingi wa ukamilifu wa kimaadili na kiroho kwa ajili ya kuwa na taathira kubwa zaidi katika jamii ya Kiislamu.

Kuna udharura wa kulindwa amani ya jamii

Awamu ya pili ya amani na usalama katika Uislamu ni amani na usalama wa jamii. Baada ya kuwa tayari kinafsi kwa kuitakasa na kuisafisha, mwanadamu huwa ametengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya muungano mpana zaidi wa kijamii na wanadamu wenzake. Hapa ndipo inapokuja amri ya Mwenyezi Mungu inayowataka Waislamu kuwa na umoja na kujenga udugu. Sehemu moja ya aya ya kwanza ya Suratul Anfal inasema:

 فَاتَّقُواْ اللَّهَ وَأَصْلِحُواْ ذَاتَ بَیْنِکُمْ وَأَطِیعُواْ اللَّهَ وَرَسُولَهُ إِن کُنتُم مُّؤْمِنِینَ

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na msuluhishe mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni waumini.

Kwa utaratibu huo Waislamu hutoka katika minyororo ya ubinafsi, ubaguzi, dhulma na sifa nyingine mbaya na kuwa watu wema na wenye faida kwa jamii.

اUislamu, dini ya amani

Awamu ya tatu ya amani na usalama inahusiana na usalama na amani kwa wasio Waislamu. Miongoni mwa misingi na kanuni zinazotawala jamii ya Kiislamu ni kuishi kwa amani na usalama na wasio Waislamu. Kinyume na fikra na dhana za wanafikra wengi wasio Waislamu na propaganda chafu za nchi za Magharibi, Uislamu ni dini ya amani na kuishi kwa usalama na wasio Waislamu. Hii ni pamoja na kwamba, huwezi kupata hata aya moja ya Qur'ani inayowalazimisha watu kukubali dini hiyo kwa vita na mabavu. Vita katika Uislamu vina sura ya kujihami na kujilinda mbele ya mashambulizi yanayolenga jamii ya Waislamu au watu wengine wanaodhulumiwa au kwa ajili ya kuzuia uchokozi na hujuma za adui.

Suala la kuishi kwa amani na usalama na wasio Waislamu limesisitizwa sana katika aya za Qur'ani tukufu na hadithi, sira na mwenendo wa Mtume na Aali zake watoharifu. Suala hili pia limejengeka juu ya nguzo ya utukufu wa kiumbe mwanadamu. Katika mtazamo wa Uislamu wanadamu wasio Waislamu wana heshima na utukufu wa kidhati na kimaumbile kutokana na kushirikiana kwao na Waislamu katika maumbile na ubinadamu japo wanatofautiana katika dini na imani. Uhakika huu unathibitishwa na sira, mwenendo na maisha ya Mtume Muhammad (saw).

Uislamu ni dini ya mapatano na amani

Mfano wa wazi wa mwenendo huo wa amani na suluhu na wasio Waislamu ni Mapatano ya Ungwana yaliyofikiwa baina ya Mtume (saw) na washirikina wa Makka kabla ya kutangazwa dini ya Uislamu, Mapatano ya Hudaibiyya, mwenendo wa Mtume Muhammad (saw) na jinsi alivyokuwa akiamiliana na tawala na wafalme wa maeneo mbalimbali kama Iran na Roma na kutumia njia ya kutuma barua kwa watawala na wafalme wa zama hizo baada ya kuunda dola la Kiislamu mjini Madina. Kwa mfano tu Mtume (saw) alisema katika amri aliyompa Amru bin Hazm wakati alipomtuma Yemen kwamba: Kila Myahudi au Mkristo atakayekubali Uislamu na kudhihirisha Uislamu halisi atakuwa mmoja kati ya waumini, atakuwa na haki sawa na za Waislamu na kushirikiana nao katika vipindi vyote vya shida na raha. Na kila mtu atakayeamua kubakia katika dini yake ya Uyahudi au Unaswara kamwe hatalazimishwa kuacha dini yake, kwa sababu ujumbe wa dini na risala za Mitume wote wa Mwenyezi Mungu ni kuleta amani, uadilifu, kueneza masuala ya kiroho, kumkamilisha mwanadamu na kumfikisah kwenye saada na ufanisi", mwishio wa kunukuu.

Uhuru wa kuabudu wa wasio Waislamu nchini Iran

Kwa msingi huo, katika mtazamo wa Uislamu suala la usalama na kuishi kwa amani na wanadamu wengine wenye itikadi na imani tofauti, ni jambo lenye thamani na umuhimu mkubwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, ni katika mazingira ya amani na usalama ndipo wanadamu wanapoweza kuelekea kwenye ukamilifu wa kimaada na kiroho, bali hata kuweza kumjua na kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Hivyo suala la kujenga na kuimarisha amani na usalama na vilevile juhudi za kulingania amani na usalama wa kimataifa na kuishi pamoja kwa amani wanadamu wote kwa msingi wa Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, uadilifu na usafi wa nafsi bila ya kujali dini, rangi, na tofauti zao nyingine ndio lengo la mwisho la Uislamu na wafuasi halisi wa dini hiyo. Ni wazi kuwa, kufuata mafundisho ya dini hiyo kunaweza kuwa suluhisho la kumwondoa mwanadamu katika kinamasi cha vita, mapigano na migogoro ya dunia ya sasa.