Oct 20, 2016 10:33 UTC
  • Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini

Tarehe 17 Oktoba ambayo mwaka huu imesadifiana na siku ya Jumatatu, huadhimishwa kila mwaka kwa jina la Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini.

Umoja wa Mataifa ndio uliotangaza siku hiyo kwa lengo la kukutanisha pamoja nguvu za mataifa yote ya dunia katika jambo moja, nalo ni kupambana na umaskini. Kila mwaka siku hiyo hutumiwa kutangaza mshikamano wa mataifa yote ya dunia kwa ajili ya kuwaliwaza na kuwasaidia wahanga wa ukata na majanga ya njaa na vilevile kutafuta njia za kuweza kung'oa kikamilifu mizizi ya umaskini na ubaguzi na kudhamini heshima na utukufu wa mwanadamu.

Msingi wa kutengwa tarehe 17 Oktoba kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini ulimwekwa mwaka 1987. Mwaka huo zaidi ya watu laki moja walikusanyika mjini Paris, Ufaransa kwa ajili ya kuwakumbuka wahanga wa umaskini uliopundukia, ukatili na njaa. Tangu wakati huo watu, taasisi na jumuiya mbalimbali kote duniani huadhimisha siku ya tarehe 17 Oktoba kama siku ya kuonesha tena mshikamano na ushirikiano wa kung'oa mizizi ya umaskini duniani. Disemba mwaka 1992 pia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza rasmi siku hiyo kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini. Suala la kupambana na umaskini lilipata nguvu zaidi kuanzia mwaka 2000 wakati ilipopasishwa Hati ya Milenia ambayo moja ya malengo yake makuu ni kuhakikisha umaskini umepungua kwa kiwango kikubwa duniani hadi mwaka 2015.

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini

Ni vyema kusema hapa kwamba, licha ya kuweko jitihada mbalimbali za kufanikisha malengo ya Milenia ya kung'oa mizizi ya umaskini duniani, lakini maeneo mengi ya dunia yanaishi kwenye umaskini mutlaki na umaskini umeongezeka zaidi. Umoja wa Mataifa unaendesha miradi mbalimbali ya kufanikisha malengo ya milenia ili kupungaza umaskini kwa kiwango kikubwa duniani. Hata hivyo bado kuna mamilioni ya watu hususan watoto wadogo ambao wanaishi katika ukata wa kupindukia.

Kwa sasa inakadiriwa kuwa watu milioni 780 wanaofanya kazi hawawezi kupata pato linaloweza kuwaondoa wao wenyewe na familia zao chini ya mstari wa umaskini yaani pato la zaidi ya dola mbili kwa siku. Kiwango hicho kinaunda thuluthi moja ya watu wanaofanya kazi katika nchi zinazostawi. Robo ya wafanyakazi katika nchi zinazostawi pia wanapata dola baina ya 2 na 4 kwa asiku. Kundi hili ambalo haliko mbali na mstari wa umaskini daima limekuwa katika hatari ya kutumbukia kwenye ukata na ufukara kutokana na sababu mbalimbali kama vile maradhi na kadhalika.

Umaskini unaawathiri zaidi watoto wadogo

Umaskini ni suala la kiuchumi na kijamii. Umaskini na ufukara pia vina mfungamano na masuala ya kiroho na kisiasa. Umaskini huwaathiri wanadamu kwa sura mbalimbali na kwa makali tofauti kulingana na vipindi mbalimbali, nafasi zao na hali za watu binasfi. Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limearifisha umaskini kuwa ni kutokuwa na pato la kiasi fulani, kutokua na hadhi na izza ya nafsi, kutokuwa na fursa za kupata elimu na kufanya harakati za kijamii na kutoshirikishwa katika kuchukua maamuzi.

Baadhi ya watafiti pia wanasema, umaskini ni hali ya kukosa au kutopata mahitaji muhimu ya kimsingi ya mwanadamu kama vile chakula na maji ya kutosha, makazi yanayofaa, suhula za afya na tiba, umri mrefu, elimu na uwezo wa kudhamini mahitaji ya kimaisha kwa mtu na watu wa familia yake kupitia shughuli na kazi zenye manufaa.

Dini ya Uislamu imekemea mno umaskini na kuupiga vita. Imepokewa kwamba, Mtume Muhammad (saw) amesema: کادَ الفَقرُ أن یَکونَ کُفرا .

Ufakiri na maskini umekaribia sana kuwa ukafiri. Vilevile imepokewa kwamba Mtume (saw) alikuwa akiomba dua kwa kusema: Ewe Mola Mlezi! Najikinga kwako wewe na ukafiri na ufukara. Bwana mmoja alimuuza mtukufu huyo kwamba: Kwani viwili hivyo viko sawa? Mtume Muhammad (saw) alisema: Ndiyo. Hadithi nyingine iliyopokewa kutoka kwa wasii wa Mtume wetu Muhammad (saw), Amirul Muuminina Ali bin Abi Twalib (as) inasema: Ufukara ndiyo mauti makubwa zaidi. Vilevile anasema katika hadithi nyingine kwamba: "Kaburi ni bora kuliko umaskini", kwa maana kwamba, kufa na kuzikwa kaburini ni bora zaidi kuliko kuishi katika hali ya ufukara na umaskini.   

Katika mtazamo wa mfumo wa uchumi wa Uislamu, umaskini na ufuraka hautokani na ukosefu au uhaba wa maliasili za dunia hii. Hii ni kwa sababu dunia ina vyanzo vya awali na maliasili ya kutosha kwa ajili ya kukidhi mahitaji halisi ya wanadamu wote. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 34 ya Suratu Ibrahim inasema:

وَآتَاکُم مِّن کُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ وَإِن تَعُدُّواْ نِعْمَتَ اللَّهِ لاَ تُحْصُوهَا إِنَّ الإِنسَانَ لَظَلُومٌ کَفَّارٌ

Na akakupeni kila mlichomuomba. Na mkihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti. Hakika mwanaadamu ni dhalimu mkubwa, mwenye kuzikufuru neema.   

Wanadamu wapenzi wasikilizaji wana sifa tofauti za kiroho, kimwili na kifikra na kwa sababu hiyo hutofautiana katia jinsi ya kukabiliana na matatizo ya aina mbalimbali, katika uwezo wao wa kuchukua maamuzi, katika ushujaa na ujasiri, katika umakini na katika uwezo wa kubuni na kuvumbua mambo mbalimbali. Hivyo basi hata kama watapewa rasilimali na suhula sawa hapana shaka kuwa watatofautiana katika matokeo na uzalishaji wa rasilimali na maliasili hiyo. Dini ya Uislamu imepinga na kupiga vita hitilafu na tofauti za kimapato zinazotokana na ubaguzi na dhulma lakini wakati huo huo imekubali hitilafu zinazotokana na tofauti za vipawa na uwezo wa kifikra na ubunifu.

Pamoja na hayo yote baadhi ya wanadamu wanakumbana na matatizo maishani kutokana na uwezo mdogo wa kimwili au kiroho na wako wengine wanaopoteza mali, milki na hata familia zao kutokana na matukio ya kimaumbile kama mafuriko, mitetemeko ya ardhi na kadhalika. Ili kukabiliana na umaskini na matatizo mengine kama haya, Uislamu umefaradhisha amali kama vile kutoa zaka, khumsi yaani moja ya tano ya mali ya muumini kwa mwaka na kuwahamasisha Waislamu kutoa sadaka na kufanya hisani na umeweka sheria zinazowalazimisha waumini kutoa kiwango fulani cha mali na milki zao kama kafara ya madhambi na makosa yao ambavyo vyote hutumika kuondoa na kufuta umaskini katika jamii.

Takwimu za umaskini mwaka 2015

Makadirio na takwimu zinaonesha kuwa, baina ya mwaka 2015 na 2030 watu milioni 570 –wanawake kwa wanaume-, watajiunga na nguvu kazi kote duniani hususan katika maeneo ya Afrika na Asia. Kwa msingi huo kuna udharura mkubwa wa kutayarishwa nafasi za kazi na ajira ili kukomesha ufukara na kubadilisha hali ya kimaisha ya mamilioni ya wanadamu. Katika uwanja huo na ili kuweza kupambana ipasavyo na ufukara na umaskini, kwanza kuna ulazima wa kutambuliwa vyema watu wanaosumbuliwa na tatizo hilo ambao wanaishi chini ya mstari wa umaskini au umaskini uliopindukia, kuweka wazi sababu za hali hiyo na kubuni ratiba na mipango mwafaka ya kukidhi mahitaji yao. Sambamba na hayo kuna haja na ulazima wa kuchukua hatua za kupunguza sababu za umaskini na ufukara kama ongezeko la kiholela la jamii, vita na mapigano, maradhi ya kuambukiza, ujinga, ufuska na kuenea kwa maasi, dhulma na ukosefu wa uadilifu na kadhalika.

Wataalamu wanasema kuwa, ni vigumu kuweza kung'oa mizizi ya ukata na umaskini duniani bila ya kuwekeza kwenye watoto na vijana kwa ajili ya vizazi vijavyo. Vilevile wanasisitiza udharura wa kuweko uadilifu katika upatikanaji na utumiaji wa suhula mbalimbali kama elimu bora, huduma za afya, uwekezaji, kujenga misingi madhubuti ya familia, kulindwa mazingira na kadhalika.

Maskini hawana suhula za kukidhi mahitaji yao

Juhudi za kutekeleza uadilifu wa kijamii na kugawanywa kwa uadilifu utajiri kati ya matabaka mbalimbali ya watu nazo zina umuhimu mkubwa sana katika kupunguza na hatimaye kung'oa kabisa mizizi ya umaskini. Siasa za kikoloni za nchi zinazopenda makuu nazo zinachangia pakubwa katika kuzidisha umaskini kwenye mataifa mengine. Ni jambo lililo wazi kuwa, madola ya kibeberu ni kikwazo kikuu katika juhudi za kupambana na umaskini. Hivyo kuna haja kwa nchi za kibeberu kuachana na siasa za kutenga fedha nyingi za kugharamia masuala ya kijeshi na kuelekeza mitaji na fedha hizo katika masuala ya ustawi wa mwanadamu na si katika kutengeneza na kununua silaha za kuua wanadamu.

Tunamalizia kipindi hiki kilichozungumzia siku ya kupambana na umaskini kwa kusoma aya ya 96 ya Suratul Aaraf ya Qur'ani tukufu unayosema:

وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَىٰ آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَفَتَحْنَا عَلَیْهِم بَرَکَاتٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ وَلَٰکِن کَذَّبُوا فَأَخَذْنَاهُم بِمَا کَانُوا یَکْسِبُونَ

Na lau watu wa miji wangeliamini na wakamcha Mwenyezi Mungu, kwa yakini tungeliwafungulia baraka kutoka mbinguni na katika ardhi. Lakini walikadhibisha haki, basi tuliwaadhibu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Juhudi zaidi zinahitajika kung'oa mizizi ya umaskini

 

Tags