Dec 04, 2017 17:02 UTC
  • Umoja kwa mtazamo wa Imam Khomeini na Kiongozi Muadhamu

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu na maadhimisho ya Wiki ya Umoja.

Wiki ya Umoja ni kipindi cha kati ya tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal ambapo baina ya Waislamu kuna hitilafu kuhusiana na tarehe aliyozaliwa Bwana Mtume saw. Waislamu wa Kisuni wanaamini kwamba, Mtume saw alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal huku Waislamu wa Kishia wao wakiamini kwamba, mbora huyo wa viumbe alizaliwa tarehe 17 ya mwezi huu. Kutokana na hitilafu hizo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikabuni kipindi cha kati ya tarehe mbili hizo kuwa ni Wiki ya Umoja, ili badala ya Waislamu kuanza kuzozana kuhusiana na tarehe aliyozaliwa Mtume wao wakutane na kujadili umuhimu wa suala la umoja na mshikamano baina yao. Kwa mnasaba wa kuwadia  Wiki ya Umoja nimekuandalieni kipindi maalumu. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Imam Ruhullah Khomeini MA

Kuwadia Wiki ya Umoja ni fursa muhimu ya kujadili suala la umoja ambalo ni zaidi ya nara na shaari na hivyo kuweka mikakati ya kivitendo katika uwanja huo. Umoja una unyeti maalumu. Wakati tunapotupia jicho kurasa za historia  tunakutana na warekebishaji na wasomi wengi kama Sayyid Jamaluddeen Asad-Abadi, Sheikh Muhammad Abdu, Ayatullah Burujerdi, Sheikh Mahmoud Shaltut, Sayyid Qutb, Imam Khomeini na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao walifanya hima na idili kubwa kwa miaka mingi kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano baina ya Waislamu. Kwa hakika Imam Khomeini ni mrekebishaji mkubwa wa zama hizi ambaye alipendekeza mikakati athirifu kwa ajili ya kuhakikisha kunapatikana umoja na mshikamano katika Umma wa Kiislamu na yeye mwenyewe alikuwa mstari wa mbele katika medani hiyo. Moja ya mikakati muhimu na ya kimsingi ya umoja wa Kiislamu kwa mtazamo wa Imam Khomeini MA ilikuwa ni kuanzisha utawala wa Kiislamu. Katika kubainisha maana na mafuhumu ya umoja, Imam Khomeini MA alizungumzia nukta mbili ambazo, mosi ni kuwa pamoja na kukusanyika Waislamu na pili ni kushikamana katika njia ya haki na alikuwa akikumbusha kwamba, umoja wa kweli hauwezi kuwa na maana bila ya kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu. Kwa mtazamo wa Qur’ani Tukufu ni kuwa, wanadamu wana umoja katika asili ya kuumbwa; na hii ni kutokana na kuwa, Mwenyezi Mungu amewaumba kutokana na nafsi moja. Umoja huu katika kuumbwa ni jiwe la msingi kwa ajili ya kuunda Umma mmoja. Kwa mtazamo wa Qur’ani Tukufu ni kuwa, Umma mmoja wa mwanadamu unasambaratika kutokana na sababu mbalimbali kama dhulma, kupenda dunia, kuwa na mitazamo ya kimakundi, njama za maadui za kufarakanisha watu na vishawishi vya shetani. Qur’ani imependekeza mipango na mikakati ili kuhakikisha hali ya umoja na mshikamano inarejea tena baina ya Waislamu kama vile udugu, huba, huruma, mapenzi na kuleta suluhu na upatanishi katika kalibu ya mafundisho ya Kiislamu. Imam Khomeini MA sambamba na kukumbusha nukta hizi alisisitiza kwamba, katika Uislamu, Waislamu ni ndugu kwa muktadha huo, Umma wa Kiislamu umeundwa na jamii ambayo watu wake wana udugu wa Kiislamu na wote wanaitakidi na kuuamini Uislamu. Imam Khomeini MA muasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu alikumbusha mara kadhaa kwamba, maana ya umoja wa Kiislamu ni Waislamu kukusanyika pamoja bila kujali itikadi zao za kimadhehebu bali wajumuike kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu na ili kufikia hilo hakuna ulazima wa kila mmoja kuweka kando madhehebu yake na kushikamana na madhehebu moja. Kwani hilo si tu kwamba, si jambo la lazima, bali ni kitu ambacho katu hakiwezekani. Waislamu wanaweza kuegemea nukta za pamoja za kidini  kama kuwa na Qur’ani moja, kuelekea upande wa kibla kimoja, kuwa na Mtume mmoja na kadhalika na hivyo kuunda umoja wa Kiislamu.

 

Njia ya kufikia umoja ni kwamba, kwa uchache Waislamu wanapaswa kuwa na mtazamo mpana katika mambo yanayohusiana na Umma wa Kiislamu na kuyaangalia hayo kwa wigo mpana zaidi ya mipaka ya Kimadhehebu, utaifa, lugha na kadhalika; na katika vitendo watangulize maslahi jumla ya Uislamu na Waislamu mbele ya maslahi madogo madogo. Imam Khomeini MA analizungumzia suala la kuzusha hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu kwamba, ni uchungu na maumivu makubwa na kwamba, jambo hilo halina maslahi isipokuwa kwa watu ambao hawana itikadi ya Ushia wala ya Usuni, au Uhanafi au kundi jingine lolote lile miongoni mwa makundi ya Kiislamu. Wao wanataka hili lisiwepo wala lile na njia ya hilo ni kuzusha hitilafu na mifarakano baina yao. Sisi tunapaswa kuzingatia maana hii kwamba, sisi sote ni Waislamu, sote ni watu wa Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu na watu wa Qur’ani na tunapaswa kufanya hima za kuihudumia  Qur’ani na Tawhidi. Imam Khomeini MA alikuwa akitambua kwamba, hitilafu hizi zina mizizi na chimbuko katika asili, jiografia, lugha, na tamaduni za asili na muhimu kuliko yote ni njama za mabeberu wa dunia ambao wanapanga mikakati ya kushadidisha hitilafu, kupandikiza mifarakano na kukuza mambo madogo ambayo Waislamu wanahitalifiana. Hivyo basi, hitilafu zilizopo baina ya nchi za Kiislamu, zinapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa misingi na mbinu za kistratijia. Mazungumzo, maelewano, ukurubishaji, hisia za pamoja na kuwa na imani na hatima na mustakabali wa pamoja ni mambo ambayo yanaunda na kutengeneza umoja. Umoja wa ulimwengu wa Kiislamu lilikuwa likihesabiwa kuwa lengo la tarajio kubwa na alikuwa akisema: “Inshallah, ifikie siku Waislamu wote wawe ndugu wa kweli na mizizi yote ya uharibifu na ufisadi katika nchi za Waislamu ing’olewe; na huu mzizi wa ufisadi wa Israel katika Masjid al-Aqswa na katika nchi zetu za Kiislamu ung’olewe. Inshallah, twende kwa pamoja huko Quds na kuswali Swala ya Umoja.” Wapenzi wasikilizaji! Baada ya kuaga dunia Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini RA, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alichukua hatamu na bendera iliyokuwa ikishikiliwa na Imam Khomeini na akaitundika juu na akalifanya suala la umoja wa Kiislamu kuwa ndio mhimili wa harakati zake. Ayatullah Ali Khamenei alisema: Kama maulama wa Kiislamu wanakubali kwamba, Qur’ani Tukufu inasema: “Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu, na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu amjue anaye mnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye kushinda.”

 

Basi bila shaka kusimamisha uadilifu, kuondoa dhulma na kuleta maisha sahihi kwa ajili ya mwanadamu ndilo lengo la dini, hivyo kuna haja ya kufanya harakati kuelekea upande wa utawala wa Kiislamu na kutawala Uislamu katika nchi na jamii za Kiislamu litakuwa jambo linalowezekana.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Moja ya mbinu na mikakati muhimu katika kuyashinda matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu na kufikia mamlaka ya kujitawala kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi ni kuunda kambi moja ya Kiislamu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Waislamu wanapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja, wasifanyiane uadui; na mhimili wao wote unapaswa kuwa Kitabu, Sunna za Bwana Mtume saw na sheria za Uislamu. Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kkiislamu amesisitiza katika baadhi ya mambo kwa shabaha ya kufikia na kupatikana umoja na mshikamano katika jamii za Kiislamu. 

Ayatullah Khamenei anayataja mambo kama kupambana na kiburi na kujiona na Waislamu kupenda dunia, kutosalimu amri mbele ya mifumo batili ya dunia, kutumiwa vyema nafasi ya kijiografia ya ulimwengu wa Kiislamu, kuwa macho na hatari ya ukaumu, madhehebu na mielekeo ya utaifa, kupambana na vibaraka wa ufarakanishaji wa maadui katika ulimwengu wa Kiislamu, kuanzisha umoja kkwa aajili ya kukabiliana na Uzayuni, kuuondolewa dhana mbaya baina ya tawala na mataifa ya Kiislamu na muhimu kuliko yote, kuitambua na kuifahamuu vyema shakhsia ya Bwana Mtume saw kwamba, ni miongoni mwa mambo muhimu ya kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu.

Ayatullah Khamenei na fikra ya umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu

Hapana shaka kuwa, kutolewa fatuwa na Mamujitahidi wa makundi ya Kiislamu ni jambo lenye nafasi muhimu katika kuleta umoja wa Kiislamu na kuondoa hitilafu na mifarakano. Katika hili Ayatullah Khamenei amekuwa mstari wa mbele ambapo ametoa fatuwa ya kujuzisha Mashia kumfuata Imam wa Kisuni katika Swala na vile vile kushiriki katika Swala za Jamaa za Masuni, fatuwa ambazo bila shaka zimeandaa uwanja wa Waislamu kuwa pamoja.

Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hakusita hata kidogo kutoa fatuwa ya kuharamisha kuvunjiwa heshima wake za Mtume saw pale mmoja wa watu anayedai kuwa Shia huko nchini Kuwait aliposimama na kutoa maneno ya kumvunjia heshima mmoja wa wake za Mtume saw. Fatuwa hiyo ya Kiongozi Muuadhamu ya kuharamisha kuvunjiwa heshima wake za Mtume saw iliakisiwa pakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Kuhusiana na hilo, 

 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema: Ni haramu kuzivunjia heshima nembo za ndugu zetu Masuni kama kumtuhumu mke wa Mtume Muhammad saw. Uharamu huo unajumuisha wake wa Mitume wote hususan Sayyid al-Anbiyaa, Mtume Muhammad saw. Maulama na wanazuoni mbalimbali walitoa radiamali zao kuhusiana na fatuwa hiyo ya Ayatullah Khamenei. Ahmad al-Tayyib, Sheikh wa al Azhar huko Misri yeye alisema: Fatuwa hii imetolewa wakati mwafaka kwa ajili ya kuzuia migawanyiko na imefunga milango ya fitina. Wapenzi wasikilizaji tunakamilisha kipindi hiki maalumu kwa kukusomeeni aya ya 46 ya Surat al-Anfal ambayo inasisitiza juu ya kujiepusha na mifarakano. Aya hiyo inasema:  Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki maalumu kilichokujieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Umoja umefiklia tamati ninakuageni nikitaraji kuwa mumenufaika na yale niliyokuandalieni katika kipindi hiki. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh...

 

Tags