Abbas bin Ali (AS) alivyopambika kwa fadhila kubwa za uungwana
(last modified Fri, 20 Apr 2018 16:28:11 GMT )
Apr 20, 2018 16:28 UTC
  • Abbas bin Ali (AS) alivyopambika kwa fadhila kubwa za uungwana

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi na karibuni katika makala hii maalumu ambayo tumekuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Abul Fadhlil Abbas, mwana wa Imam Ali AS na ambaye alikuwa jemedari shujaa na uti wa mgongo wa Imam Husain AS katika mapambano ya Karbala.

Abul Fadhlil Abbas AS aliishi na baba yake Imam Ali AS kwa muda wa miaka 14 na alipambika kwa sifa za imani, elimu na ukamilifu wa kibinaadamu kama baba yake Imam Ali AS, alikuwa fasaha wa maneno, mweledi wa mambo na mwenye muono wa mbali. Alipambika kwa sifa nzuri nzuri kiasi kwamba Imam Ali AS amenukuliwa akisema: Mwanangu Abbas ameelimika akiwa bado mtoto mdogo na amejifunza maarifa kutoka kwangu na kuwa mithili ya kifaranga cha njiwa ambaye anatiliwa maji na chakula mdomoni na mama yake.

Hivi sasa tumo katika maadhimisho ya kukumbuka siku ya kuzaliwa mtukufu huyo ambaye jina lake katika historia limeshikana vilivyo na sifa za uaminifu na kujitolea muhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu mithili ya ulimi na mate, viwili hivyo havitenganishiki. Abul Fadhlil Abbas AS ni mtu mtukufu ambaye sira ya uungwana wake inameremeta mithili ya loho ya thahabu katika uwanda wa dunia. Mwezi Nne Shaaban inasadifiana na siku ya kuzaliwa Hadhrat Abbas bin Ali AS. Alipewa lakabu ya Abul Fadhl, yaani "Baba wa Fadhila" kutokana na fadhila nyingi alizokuwa amepambika nazo. Wakati tunapoamua leo hii kuwataja kwa wema watu wa Mwenyezi Mungu kama Abul Fadhlil Abbas AS ni kwa sababu sira, maisha na mienendo yao siku zote imekuwa ni ruwaza na kigezo cha wanadamu kuelekea kwenye saada na uja mwema. Tunatumia fursa hii kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa sikukuu za mwezi wa Shaaban hususan siku ya kukumbuka kuzaliwa Abul Fadhlil Abbas AS.

 

Tarehe 4 Shaaban mwaka wa 26 wa Hijria Qamaria, nyoyo za wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW zilijawa na furaha kwa kuzaliwa mwana wa kiume katika nyuma ya Imam Ali AS. Wakazi wa Madina walielekea haraka kwa Imam Ali AS ili kwenda kutoa tabriki na pongezi bora kabisa kwa kujaaliwa kupata mtoto mwingine wa kiume. Mama yake Abul Fadhlil Abbas AS aliyejulikana kwa jina maarufu la Ummul Banin, kwa upole na huruma kubwa alimkabidhi mwanawe huyo kwa baba yake Imam Ali AS, na Imam akamsomea adhana katika sikio lake la kulia na iqama katika sikio lake la kushoto mwanawe huyo mpenzi kwani adhana na iqama ni naghma ya Tawhidi na Utume. Imam Ali ambaye jicho lake lilikuwa linaona upeo wa mbali ambao haukuwa ukionekana na watu wengine wa kawaida, aliona sifa za ujasiri, ufahali na ushujaa mkubwa ndani ya mtoto huyo na ndio maana alimpa jina la Abbas lenye maana ya "Simba Shujaa na Mshindi."

Jina la asili la mama yake Abul Fadhlil Abbas AS lilikuwa ni Faatima binti Huzzam ambaye baadaye alijulikana kwa jina maarufu la Ummul Banin. Mama huyu aliwalea vizuri sana watoto wa Bibi Fatimatuz Zahra SA, alikuwa mwenza mzuri sana kwa mumewe Imam Ali AS na siku zote alikuwa akijihesabu kuwa ni mtumishi wa Imam Ali na wana wa Bibi Fatimatuz Zahra SA. Kwa kweli kumenukuliwa maelezo mengi sana kuhusu fadhila na utukufu wa mke huyo wa Imam Ali AS yaani mama wa Abul Fadhlil Abbas AS. Aalim Zaynuddin maarufu kwa jina la Shahiduth Thani amesema haya kuhusu bibi huyo:

"Ummul Banin alikuwa ni mwanamke mweledi wa mambo na mwenye heshima kubwa. Alikuwa na mapenzi makubwa na Watu wa Nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Alikuwa mtu mwenye ikhlasi kubwa na alitumia umri wake wote kuwatumikia Ahlul Bayt AS. Watu wa Nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW nao walimpa heshima kubwa mama huyu." Mwisho wa kunukuu.

 

Hadhrat Abul Fadhlil Abbas AS alipewa pia lakabu ya Qamar Bani Hashim yaani mwezi wa Bani Hashim kutokana na sura yake ya kuvutia, sira yake tukufu na umbo zuri sana la kupendeza. Ibnu Shahrashub, mufassir na mpokezi mkubwa wa hadhithi amesema hivi katika kitabu chake cha Manaqib.

"Abul Fahlil Abbas AS alipewa lakabu ya Qamar Bani Hashim, yaani Mwezi wa Bani Hashim kutokana na kuwa uso wake uliojaa baraka ulikuwa unameremeta mithili ya nuru ya mwezi."

Vile vile kumenukuliwa hadithi nyingi kutoka kwa Watu wa Nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW kuhusiana na Abul Fahlil Abbas AS. Imam Ali AS wakati alipokuwa kwenye kitanda ya kuuawa shahidi alimwita kwake Abbas AS na kumkumbatia kifuani pake na kumwambia mwanawe huyo kwamba: Karibuni hivi jicho langu litafurahi kuonana na wewe tena mbele ya Haki, ikiwa ni kumtabiria kuwa na yeye angeliuawa shahidi katika jangwa la Karbala akiwa pamoja na kaka yake Imam Husain AS.

Aidha kumenukuliwa hadhithi nyingi kutoka kwa Imam Husain AS kuhusiana na utukufu wa Abul Fahlil Abbas. Miongoni mwa hadithi hizo ni matamshi ya Imam Husain AS kuhusu Abul Fahlil Abbas jioni ya tarehe 10 Muhamarram, maarufu kwa siku ya Ashura. Imam Husain alimwambia Abul Fadhlil Abbas kwamba: "Ndugu yangu mpenzi, roho yangu iwe fidia kwako, panda juu ya farasi na nenda katikati ya adui." Katika maneno hayo ambayo Imam Husain AS alimweleza ndugu yake baada ya kulazimika kwenda katikati ya maadui kwa ajili ya kuteka maji ya watoto waliokuwa wanateseka kwa kiu, Imam AS alitumia maneno "roho yangu iwe fidia kwako" yaani niko tayari kumwaga damu yangu kwa ajili yako ikiwa ni kuonyesha mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kuhusiana na Abul Fahlil Abbas AS.

Historia inathibitisha kuwa, Imam Ali AS alikuwa akimpenda mno mwanawe Abul Fadhlil Abbas na alilipa uzito wa hali ya juu pia suala la kumuelimisha, kumjenga kiimani na kumzatiti kwa sifa za ukamilifu wa kibinadamu, jambo lililomfanya Abul Fahlil Abbas AS awe na umbuji wa hali ya juu wa balagha na ufasaha wa maneno. Abul Fadhlil Abbas alipambika kwa sifa hizo kiasi kwamba katika kitabu cha Ghurarul Ahkam, juzuu ya 6, ukurasa wa 96, Imam Ali AS ananukuliwa akisema: Mwanangu Abbas ameelimika akiwa bado mtoto mdogo na amejifunza maarifa kutoka kwangu na kuwa mithili ya kifaranga cha njiwa ambaye anatiliwa maji na chakula mdomoni na mama yake.

 

Mbali na kumlea mwanawe huyo kwa fadhila za kiroho na kimaanawi, alimjenga pia katika upande wa ushujaa na nguvu za mwili. Alimfundisha fani zote za kishujaa zilizokuwa maarufu wakati huo ikiwa ni pamoja na kulenga shabaha kwa mishale. Ni jambo lililo wazi kuwa kuandamana kwake na baba yake Imam Ali AS ambaye pia alikuwa maarufu kwa jina la Simba wa Mungu mwenye kushinda, kutokana na ushujaa wake mkubwa, ilikuwa ni fursa nzuri kwa Abul Fadhlil Abbas kuzidi kujipamba kwa sifa za utukufu wa baba yake na akaja akazitumia fadhila na sifa zote hizo katika siku alipohitajika kuzitumia.

Amma nukta muhimu zaidi katika maisha ya Abbas bin Ali AS ni mapenzi yake makubwa, ukuruba na utiifu wake mkubwa kwa kaka yake Imam Husain AS. Kuandamana na kuwa pamoja na watu watukufu kama baba yake Ali bin Abi Talib na kaka zake Hasan na Husain AS kulimpa fadhila na utukufu mwingi Abul Fadhlil Abbas AS. Siku zote alikaa kwa heshima kubwa mbele ya kaka zake, kamwe hakuwahi kwenda kwa Imam Husain AS bila ya kuomba idhini kwanza. Hadithi zinasema kuwa, katika kipindi chote cha miaka 34 ya umri wake uliojaa baraka, Abul Fadhlil Abbas hakuwahi hata siku moja kumwita Imam Husain AS kwa jina la "kaka yangu" bali mara zote alikuwa akitumia majina kama "Yabna Rasulillah yaani Ewe mwana wa Mtume" au "Bwana wangu" na majina kama hayo. Alikuwa pamoja na kaka yake mtukufu Imam Husain AS tangu udogoni mwake hadi alipouawa shahidi pamoja naye siku ya tarehe 10 Muharram, siku ya Ashura, katika jangwa la Karbla la Iraq ya leo.

Kwa mara nyingine tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwenu nyinyi nyote kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Abul Fadhlil Abbas, mwana wa Imam Ali AS, aliyekuwa jemedari mkubwa katika jeshi la Imam Husani AS kwenye mapambano ya Karbala tukimuomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki ya kupamba maisha yetu kwa sira na mienendo iliyojaa baraka ya watu watukufu katika Uislamu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags