Kutwaliwa kwa Andalusia na ustaarabu wa Kiislamu barani Ulaya
(last modified Sat, 15 Sep 2018 10:19:32 GMT )
Sep 15, 2018 10:19 UTC
  • Kutwaliwa kwa Andalusia na ustaarabu wa Kiislamu barani Ulaya

Tarehe 5 Julai miaka 1347 iliyopita ardhi ya Andalusia huko Uhispania ya leo ilidhibitiwa na jeshi la Kiislamu lililoongozwa na Tariq bin Ziyad.

Andalusia au mkono bahari wa Iberian ni ardhi iliyoko kusini magharibi mwa Ulaya ambayo inajumuisha ardhi ya Uhispania, Ureno na eneo la Jabal Twariq au Gibraltar. Nchi hiyo ya Andalusia ilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na ustaarabu wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 800 na daraja na kiunganishi cha mashariki na magharibi katika masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. 

Wakazi wa zamani wa Andalusia walikuwa watu wa kaumu ya Iberians na eneo hilo lilipewa jina la wakazi wake. Baadaye kaumu nyingine kama Phoenician na baada yao Wagiriki na kisha Carthage pia zilikwenda na kuishi katika eneo hilo. Warumi pia walitawala eneo hilo kwa miaka mingi. Peninsula ya Iberian (Iberian Peninsula) ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Warumi, kwa sababu ilikuwa njia panda inayaunganisha Ulaya na Afrika na makutano ya mabara hayo mawili. Warumi walitawala Andalusia hadi karne ya tano baada ya kuzaliwa Isa Masiih hadi walipoondolewa huko na Wagoth. Kwa utaratibu huo Andalusia ilitekwa na Wagoth katika karne ya sita Miladia. Wafalme wa Kigoth walikuwa watu madikteta na madhalimu, na ukatili na dhulma zao hazikuvumuliwa na wakazi wa eneo hilo. Kwa msingi huo wakati Waislamu waliposhambulia Andalusia mwaka 714, miji mingi mikubwa iliwafungulia milango wapiganaji wa Kiislamu. Wakazi wa eneo hilo walikumbatia itikadi na utamaduni wa Kiislamu na kuwakimbia watalawa madhalimu na waovu wa Kigoth. 

Uislamu uliingia Uhispania na Andalusia kwa ujumla katika zama za utawala wa Waliid bin Abdul Malik. Mtawala huo alimteua Mussa bin Nasiir kuwa kiongozi wa eneo la kaskazini mwa Afrika ambalo ndio kwanza lilikuwa limetwaliwa na Waislamu. Mussa bin Nasiir aliamua kutwaa maeneo zaidi na kuwalingania watu wake dini ya Uislamu. Hivyo aliamua kuelekea Uhispania. Bin Nasiir alimwamuru kamanda wake mmoja aliyejulikana kwa jina la Twariq bin Ziad kutwaa eneo la Uhispania. Twariq bin Ziad alivuka lango bahari la Jabal Twariq akiwa pamoja na idadi ndogo ya wapiganaji wake na tarehe 21 Shawwal mwaka 92 Hijria alifika eneo ambalo hii leo linajulikana kwa jina lake. Wapiganaji hao walitwaa kikamilifu eneo la Andalusia katika kipindi cha miaka minne.

Twariq bin Ziad

Wakati Twariq na jeshi la Waislamu lilipoingia Uhispania, Ulaya ilikuwa imeghiriki katika kinamasi cha taftrishi ya itikadi za watu na kupinga maendeleo ya elimu ya sayansi. Wakati huo kanisa kwenye karne za kati, lilikuwa likifanya taftishi na kukagua itikadi na imani za watu. Watu wengi hususan wasomi na wanafikra walipelekwa mahakamani na kudadisiwa imani na itikadi zao wakituhumiwa kuwa wameritadi na kuachana na Ukristo, kuwa washirikina au wachawi. Watu hawa kwanza walihukumiwa adhabu ya mateso makali na hatimaye walinyongwa na kuuawa kwa njia za kinyama na kikatili. Kuingia kwa Waislamu katika eneo hilo kulibadili kabisa hali ya mambo ya Andalusia.

Baada ya kuingia katika eneo hilo Waislamu waliwadhaminia uhuru Wakristo na Wayahudi waliokuwa wakiishi hapo na kuwapa ulinzi na usalama baada ya kupokea jizia na kodi. Mwenendo mzuri wa Kiislamu uliwaathiri sana Wakristo wa Andalusia ambao waliishi kwa uhuru na amani isiyo na kifani katika kipindi hicho. Mali na maeneo yao ya ibada yalilindwa, na walifikishwa mara chache sana katika mahakama makhsusi na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zao wenyewe katika kesi chache. Uhuru huo wa kidini uliwakurubisha zaidi Wakristo kwa Waislamu kwa kadiri kwamba, ndoa baina ya wanaume Waislamu na wanawake wa Kikristo zilishamiri na kuenea. Mbali na hayo baadhi ya Wakristo walichagua majina ya Kiislamu na kuwafuata majirani zao Waislamu kwa hiari zao katika mambo mengi. Waislamu wa Andalusia pia waliamiliana kwa wema na Wayahudi wa eneo hilo na wakati Mayahudi walipokuwa wakiuawa katika baadhi ya maeneo ya Ulaya, baadhi yao walikimbilia hifadhi huko Andalusia na kupokewa na Waislamu kwa mikono miwili ya ukarimu na mahaba.

Baada ya kutwaliwa Andalusia, utamaduni na sanaa ya eneo hilo ilinawiri na kuchanua. Mwandishi maarufu wa kitabu cha A Short History of Civlization, Henry Stephen Lucas anasema: "Matunda adhimu ya Waislamu huko Uhispania yana umuhumu mkubwa kwa utamaduni wa Ulaya. Baada ya kufunguliwa milango ya Uhispania kwa Waislamu, watawala Waislamu walieneza utamaduni, maarifa na fikra za Kiislamu katika eneo hilo. Maisha ya wakazi wa Uhispania yalibadilika kabisa baada ya kuingia katika dini hiyo mpya kwa kadiri kwamba, miji na maeneo ya Córdoba, Toledo na Granada yalibadilika na kuwa vituo vya ustawi na maendeleo ya elimu, utamaduni na sanaa. Elimu na maarifa ya Kiislamu kutoka maeneo hayo yalienea na kushamiri katika maeneo mengine ya Kikristo barani Ulaya hususan katika nchi za Ufaransa na Ujerumani."

Harakati kubwa ya kielimu iliyotawala Andalusia baada ya Waislamu kuingia katika eneo hilo imeacha historia na kumbukumbu ya wasomi, wanafikra na wanafalsafa wakubwa kama Ibn Rushd (Averroes kama anavyojulikana huko Magharibi) Ibn Arabi, Ibn Sayyid Betlemos, Hayyan bin Khalaf Qurtubi, Abdul Hamiid bin Abduun Andalusi na wengine wengi. Maktaba ya Córdoba pekee ilikuwa na vitabu laki nne katika Andalusia ya Kiislamu, wakati maktaba kubwa zaidi ya Ulaya ya Kikristo ya kabla ya karne ya 12 haikuwa na zaidi ya mamia kadhaa ya vitabu.  

Uislamu huko Andalusia ulikuwa chanzo na chachu ya maendeleo, kuchanua kwa vipawa vya watu, ustawi wa kijamii na ujenzi. Kuchanua kwa shughuli za kiuchumi kulistawisha zaidi kazi za viwanda kama vile usokotaji wa nyuzi, kufuma na kushona. Viwanda vya nguo na vitambaa vya Granada vilikuwa mashuhuri sana, kiasi kwamba vitambaa hivyo vilienea na kuuzwa katika nchi mbalimbali za Ulaya. Kuingia kwa vitambaa vyenye ubora wa kiwango cha juu na vya aina mbalimbali katika masoko ya Ulaya kuliyafanya mavazi ya Wakristo wa bara hilo yashabihiane sana na yale yaliyokuwa yakivaliwa katika jamii za Waislamu. Utengenezaji vioo wa Andalusia ulishamiri na kushika kasi. Abbas bin Firnas alikuwa mtu wa kwanza aliyetengeneza kioo kutokana na jiwe. Firnas ambaye alikuwa mwenyeji wa Córdoba, katika karne ya 9 Hijria alifanikiwa kutengeneza miwani na kipimajoto kwa kutumia utaalamu wa hali ya juu. Vilevile alivumbua chombo cha kuruka angani. 

Athari za Waisalmu nchini Uhispania.

Waislamu pia walibadilisha maisha ya watu wa vijiji huko Andalusia kwa kupeleka huko teknolojia na mbinu mpya ya kilimo. Katika kitabu chake cha Book of Agriculture, Mohamed bin Awwam alichunguza na kufanyia utafiti zaidi ya mimea 600. Kitabu hicho kilikuwa na nadharia mpya kuhusu aina mbalimbali za udongo, mbolea, maradhi ya mimea na jinsi ya kuyatibu, namna ya kuhifadhi matunda, mazao na kadhalika.

Mbali na hayo watu wa Ulaya walijifunza mengi kutoka kwa Waislamu wa Andalusia kuhusu ustawi wa kilimo cha mimea ya mazao kama katani, zafarani na kadhalika. Ustawi wa kilimo ulikuwa na taathira nzuri kwa shughuli za biashara na bandari za Málaga na Almería zilikuwa vituo vikuu vya harakati kubwa za uuzaji nje wa bidhaa za kibiashara. Bidhaa zilizozalishwa Uhispania katika kipindi hicho ziliuzwa katika nchi nyingine za Ulaya na baadhi ya bidhaa za Andalusia zilionekana pia katika miji ya Damascus, Makka na Baghdad.

Msikiti wa Cordoba.

Majengo makubwa ya Andalusia pia ni kielelezo cha vipawa na umahiri mkubwa wa Waislamu. Nguzo adhimu za majengo hayo, masakafu, milango na madirisha yenye umbo na sura ya hilali, minara, kuba na nakshi za kuvutia na maridadi na kadhalika ni kielelezo cha usanifu majengo wa Kiislamu wa watu wa Andalusia. Miongoni mwa kazi kubwa zaidi za usanifu majengo wa Kiislamu wa wakati huo ni Msikiti Mkuu wa Córdoba. Hata hivyo inatupasa kuashiria hapa kuwa, sehemu moja ya eneo hilo la ibada iliharibiwa baada ya Wakristo kuvamia Andalusia na kukajengwa kanisa kubwa badala yake. Pamoja na hayo sehemu kubwa ya msikiti huo ingalipo hadi hii leo.  

Kanisa la Córdoba

Mtafiti wa Kijerumani, Sigrid Hunke ameandika kuwa: Uhispania ni kielelezo kamili na kilele cha sanaa ya Kiislamu. Kama kulikuwepo ustawi duniani basi ulipatikana Andalusia…"

Inasikitisha kusema hapa kuwa, ustaarabu na utamaduni huo adhimu wa Kiislamu huko Andalusia na Uhispania kwa ujumla ulisambaratika na kuporomoka baada ya kutawala kwa kipindi cha miaka 800 kutokana na kuenea ufisadi, ufuska wa watawala na kutupiliwa mbali mafundisho asili ya Uislamu. Kudhihiri na kuporomoka huko kwa ustaarabu wa Uislamu katika eneo hilo la Ulaya kunatoa somo kubwa na ibra kwa Waislamu wa leo. Mwanafikra wa Kiislamu wa zama hizi, Ayatullah Murtadhaa Mutahhari anasema: Historia ya mwanadamu inaonesha kuwa, mara zote watawala wanapotaka kuwadhibiti watu wa jamii na kuwanyonya hufanya mikakati ya kueneza ufuska katika jamii husika, na ili kutimiza suala hilo hutumia njia za kueneza anasa na ngono katika jamii na kuwahamasisha wananchi kufanya hivyo. Mfano hai wenye ibra na mafunzo wa mbinu hiyo ni maafa yaliyowakumba Waislamu wa Uhispania. Wakristo wa Magharibi walitumia mbinu hiyo ili kuweza kuwanyang'anya Waislamu eneo hilo, na wakaweza kuua azma, irada, imani, ushujaa na utakasifu wa nyoyo baina ya jamii ya Waislamu na badala yake wakawafanya kuwa watu dhaifu, walioghariki katika matamanio ya ngono na anasa, walevi na wazinzi; na ni wazi kuwa ni rahisi sana kuweza kuwashinda watu wenye sifa kama hizi."