Dec 01, 2018 10:28 UTC
  • Mapitio ya Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu

Assalamu Alaykum msikilizaji mpenzi wa Radio Tehran popote pale ulipo wakati huu na karibu kusikiliza kipindi hiki maalumu cha Mapitio ya Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu uliofanyika hapa mjini Tehran kuanzia tarehe 24 hadi 26 Novemba 2018, kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja ya maadhimisho ya kuzaliwa Kiongozi na Muunganishi wa Umma wa Kiislamu, Bwana Mtume Muhammad SAW. Endelea basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Tuko katika kipindi cha historia, ambapo tunashuhudia ndani yake ishara za kivitendo za umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Leo njama za kuanzisha hitilafu na uadui ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu zimegonga ukuta, na ukurasa mpya umefunguliwa katika ulimwegu huo. Hii leo nyingi ya njama hizo zimeambulia patupu, kutokana na jitihada za vikosi vya kambi ya muqawama, kujisabilia roho zao walinzi wa Haram na maziara matakatifu, kujitoa mhanga watetezi wa umoja katika ulimwengu mzima wa Kiislamu na kwa juhudi kubwa za Baraza la Kimataifa la Kuzikurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu na jumuiya nyinginezo za kuleta umoja na ukuruba ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu. Mwanzo wa ushindi huo umeadhimishwa katika Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa umoja uliofanyika hivi karibuni hapa mjini Tehran.

Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ukiendelea mjini Tehran

Mpenzi msikilizaji, Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na kutekelezwa kila mwaka na Baraza la Kimataifa la Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu sambamba na maadhimisho ya uzawa wenye baraka wa Bwana Mtume Muhammad SAW, ambapo katika mjumuiko huo wageni waalikuwa, wengi wao wakiwa ni shakhsia watajika, mawaziri wa nchi za Kiislamu pamoja na wasomi na wanafikra wa Kishia na Kisuni kutoka ndani na nje ya nchi, hutoa maoni, rai na mitazamo yao kuhusu umuhimu wa umoja katika umma wa Kiislamu na njia za kulifikia na kulidumisha jambo hilo muhimu. Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umefanyika kwa kaulimbiu ya “Quds; Mhimili wa Umoja wa Umma”. Zaidi ya shakhsia 300, wakiwemo wanafikra, wanasiasa na magwiji wa sanaa kutoka nchi 100 duniani walihudhuria mkutano huo ili kuutangazia ulimwengu kwamba, kambi ya watetezi wa uhuru kwa uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu imeundwa duniani; na wanafikra wataalamishaji na wanamapamano wa muqawama wamejipanga safu moja kukabiliana na Ubeberu na Uistikbari.

Dakta Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkuu katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo. Katika sehemu moja ya hotuba yake, Rais Rouhani alisema: “Kwetu sisi, umoja ni suala la kistratejia. Umoja si kwa ajili tu ya kuona watu wa Palestina wanarejea makwao, kwa sababu kama wananchi wote wa Palestina watarejea makwao pia, bado tutapaswa kuwa wamoja; umoja ni msingi wa dini yetu; Qur’ani inasema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَیْنَ أَخَوَیْکُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّکُمْ تُرْحَمُونَ

Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe. (Suratul Hujuraat, aya ya 10).

Rais Rouhani alifafanua katika hotuba yake hiyo kwa kusema: “Kama tutaungana, tutapata ushindi dhidi ya Wazayuni na Marekani… Kama tutawalingania na kuwaita vijana wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa maneno makini, Mwenyezi Mungu hatotuacha peke yetu. Kama tutaishika njia ya Mwenyezi Mungu, Mtume hatotuacha peke yetu, malaika hawatotuacha peke yetu.

Dakta Rouhani alitanabahisha pia kwamba maana ya umoja si kila mtu kuacha madhehebu yake, na akabainisha kwa kusema: “Kila mmoja amkubali mwenzake, wala tusiifinye nafasi ya dini kwa kutumia jina la madhehebu. Tusitumie Ushia kutaka kulihodhi eneo la Uislamu, wala tusiutumie Usuni kulihodhi eneo la Uislamu. Madhehebu inatafsiriwa ndani ya dini; madhehebu si chemchemi, ni mchirizi unaotokana na Uislamu. Haiwezekani kuikausha chemchemi kwa sababu ya mchirizi, kwani kama chemchemi itakauka, mchirizi ndio utakaokuwa wa mwanzo kukauka… Hakuna haja ya kuwafuatilia Mahanafi wawe Mashia." Rais Rouhani aliongezea kwa kusema: Wasio Waislamu wako wengi mno duniani; tuwaendee hao kuwasilimisha. Kwa kila mmoja kumtambua mwenzake kwa ulimi tu, bila ya kuwa na udugu wa moyoni, hakutufikishi popote. Ikiwa kuna watu wameuliwa Afghanistan na Pakistan na suali langu la mwanzo likawa ni kutaka kujua waliouliwa ni Shia au Suni, maana yake ni kwamba hatuko katika njia ya umoja."

Rais Hassan Rouhani akihutubia kikao cha ufunguzi cha mkutano
 

Kuwaunganisha Waislamu, kuwafanya kitu kimoja na kuleta mshikamano kati yao ni miongoni mwa kumbukumbu muhimu zaidi iliyoachwa na Bwana Mtume Muhammad SAW kwa ajili ya umma wa Kiislamu; kwa hivyo kila pale tabia na mienendo ya Waislamu inapoendana na mafundisho ya Qur'ani tukufu, Mtume wao wa rehma na huruma na Ahlul Bayt zake watoharifu, utakuwa ni wenye kufuata aina fulani ya umoja na mshikamano. Maulamaa wa dini wanautaja umoja baina ya Shia na Suni kama mbawa mbili za kuupa nguvu Ulimwengu wa Kiislamu. Kuachana na utoaji hukumu usio sahihi kuhusu suala la fiqhi na madhehebu za Suni na Shia ni maudhui muhimu inayotiliwa mkazo na maulamaa na wananadharia wa Kishia na Kisuni.

Katika mkutano wa umoja, ilitiliwa mkazo pia nukta kwamba, ili kuweza kusimama imara kukabiliana na njama za maadui wa Uislamu, umoja ni sababu muhimu zaidi ya kufanikishia lengo hilo; na uzembeaji wowote katika suala hilo utawafanya Waislamu wawe mbali na malengo matukufu ya Uislamu.

Mbali na masuala mengine, maudhui iliyopewa umuhimu wa aina yake katika Mkutano wa Kimataifa wa Umoja ilikuwa ni kadhia ya Palestina kwa kusisitiziwa haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi zao za jadi, kupatiwa haki zao za kisheria na kisiasa, kukabiliana na mipango mingine yoyote mbadala yenye lengo la kuifuta kadhia ya Palestina, hali halisi ya Ukanda wa Gaza na kuunga mkono Maandamano ya Haki ya Kurejea. Abu Said al Minawi, mmoja wa maulamaa kutoka Tunisia alizungumzia suala hilo kwa kusema: "Waislamu duniani wanaweza kuwatambua maadui zao na kujitenga nao kupitia Palestina. Suala la Palestina na Quds ni suala la kujengea umoja; na ikiwa Ulimwengu wa Kiislamu utajitenga na masuala hayo utapotea. Suala la Palestina ndiyo dira halisi. Leo Mapinduzi ya Kiislamu yametupatia hidaya sisi Waislamu; na hidaya yenyewe ni wito wa umoja chini ya mhimili wa Quds na Palestina… Haki za Waislamu zimeporwa Palestina na inapasa zirejeshwe. Suala la Palestina ndio mhimili wa nembo zote za Umma wa Kiislamu."

Msikilizaji mpenzi, "Muamala wa Karne" ni istilahi ya kisiasa na mpango uliopendekezwa na Marekani kwa madhumuni ya kile kinachodaiwa kuwa ni kutafuta suluhu kati ya Palestina na Israel, na kuhitimisha mzozo wa zaidi ya miaka 70 baina ya pande hizo mbili. Mpango huo ambao ni maarufu kwa jina la Muamala Mkubwa wa Karne unalenga kuipatia upendeleo mkubwa Israel mkabala na kuundwa kijinchi kidogo cha Palestina kitakachojumuisha nusu ya eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Gaza na baadhi ya sehemu za Baitul Muqaddas Mashariki. Kwa mujibu wa mpango huo, mji wa Abu Dais umekusudiwa uwe ndio mji mkuu wa Palestina.

Kiongozi wa harakati ya Palestina ya HAMAS, Ismail Haniya akihutubia mkutano wa umoja kwa njia ya vidio kutokea Ukanda wa Gaza

Katika kamati ya kukabiliana na mpango huo wa Mapatano ya Karne ya Mkutano wa Kimataifa wa Umoja, wajumbe wa kamati hiyo walisisitiza kwamba, mpango huo uliopendekezwa na Trump utasababisha madhara kwa Ulimwengu wa Kiislamu. Tayseer Al-Khatib, mwandishi na mchambuzi wa Kipalestina ameuelezea mpango huo kuwa ni mtego kwa wananchi wa Palestina. Pendekezo alilotoa yeye ni kubuniwa mpango wa kitaifa wa Palestina ili kuweza kukabiliana na mpango huo wa kihaini wa Muamala wa Karne. Na sababu ni kwamba, endapo nchi za Kiarabu na Kiislamu zitaanzisha uhusiano na Israel zitaidhoofisha kadhia ya Palestina; kwa hivyo nchi zote zinapaswa kutekeleza wajibu wao kuhusiana na suala hilo.

Sheikh Hassana al-Baghdadi, mjumbe kutoka Lebanon katika Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, yeye pia aligusia katika hotuba yake kuhusu mpango wa Muamala wa Karne na kuutaka Ulimwengu wa Kiislamu usilifumbie macho suala hilo kwa kusema: Utawala wa Kizayuni na Marekani zimepigwa kipigo kikali na Muqawama katika nchi za Iran, Lebanon, Palestina na Syria; na Trump anataka kuutumia Mpango wa Muamala wa Karne ili kuvitia mkononi vyanzo vya mafuta katika eneo, lakini njama hiyo itashindwa kutokana na muqawama wa Iran na waitifaki wake. Sheikh Al-Baghdadi aidha aliashiria mpango wa Israel wa kutaka kuunda muungano wa pande tatu za Waebrania, Wasaudi na Wamarekani na kubainisha kwamba: Njama hii inapangwa katika hali ambayo Iran imekuwa kila mara ikichukua hatua ya kuukata mnyororo huo na kutoruhusu kuthibiti kwa jambo hilo.

Ni vyema kukumbusha pia kuwa, kwa mnasaba wa kuadhimisha uzawa wa Bwana Mtume Muhammad SAW na Imam Jaafar Sadiq (as), wageni washiriki wa Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu walihitimisha mkutano wao huo kwa kuonana na kuzungumza na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei.

Mpenzi msikilizaji, ni hayo basi niliyokuwa nimekuandalia kuhusiana na mapitio ya mkutano wa 32 wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu. Nakushukuru kwa kunisikiliza na nakutakia usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu…/

 

Tags