Apr 11, 2022 10:56 UTC
  • Ramadhani, mwezi wa fursa

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunakukaribisheni kusikilizaji kipindi hiki maalumu ambacho tumekutayarishieni kwa mnasaba wa funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Ndugu wasikilizaji mliofunga, tunamuomba Mwenyezi Mungu atakabali funga, amali na ibada zenu katika mwezi huu mtukufu, mwezi ambao unatupelekea tuhisi zaidi uwepo wa Mwenyezi Mungu katika maisha yetu kuliko wakati mwingine wowote. Naam, tuko mbele ya Mungu, na nyoyo zetu, dini, imani, na maana ya maisha yetu yanapata rangi, usafi na ufahamu mpya kabisa. Katika mwezi huu, anga ya kila kitu humfanya Mwislamu kutembea kwenye njia sahihi ya maisha ya Kiislamu. Katika mtindo wa maisha ya Kiislamu, kuna nukta kadhaa ambazo ni muhimu sana. Kwanza, ni kuzingatia mambo kwa undani wake sambamba na kushikamana na mwonekano wa nje wa matendo, pili ni kuzingatia hali ya mtu binafsi na jamii, na tatu ni kuchunga utaratibu katika mambo ya mtu binafsi na ya kijamii. Katika kipindi hiki, tutajaribu kuyatazama mambo haya kwa muhtasari, karibuni.

Katika Uislamu, kuna uhusiano wa kina na wa karibu sana kati ya imani na tabia za watu. Haiwezekani mtu kumwamini Mwenyezi Mungu na Ufufuo yaani Siku ya Kiama na wakati huo huo asiwe na mienendo na tabia zinazoendana na dini. Kwa hivyo, ikiwa mtu atadai kuwa amesamehewa kufanya ibada za kidhahiri kwa sababu ana imani ya ndani moyoni, madai hayo hayatakubalika kabisa. Mtume wa Uislamu, ambaye mwenyewe alikuwa katika daraja ya juu kabisa ya imani na itikadi ya moyoni, hakuacha hata mara moja kutekeleza matendo na ibada za kidhahiri zinazotokana na imani hiyo, bali alizingatia zaidi kutekeleza majukumu na kuacha mambo yaliyoharamishwa kuliko watu wengine wote.

Kuzingatia imani, itikadi  na mambo ya ndani hakumzuii muumini kufanya matendo ya dhahiri, kama ambavyo kujishughulisha na mambo ya dhihiri kidini hakumzuii kujishughulisha na ya ndani moyoni. Kimsingi, dhihiri na undani wa matendo ni sura mbili  za ukweli na hakika moja ambapo iwapo tutashikamana na moja na kuliacha jingine basi tutakuwa tumefeli na kutodiriki vilivyo hakika hiyo. Imam Swadiq (as) anasema: “Ufisadi wa dhahiri unatokana na upotovu wa ndani, na mtu anayerekebisha mustakbali na ndani yake, Mwenyezi Mungu humrekebishia dhahiri yake." Katika Qur'ani Tukufu, Mwenyezi Mungu anawataka Waislamu wafanye "matendo mema" na matendo hayo bila shaka yanayotokana na imani safi na thabiti. Ni wazi kuwa iwapo imani na nia safi haitatekelezwa kimatendo, basi hakuna jambo litakalokuwa limefanyika, hivyo kuwa na imani safi pekee hakutoshi kumfanya mtu kuwa mwema, bali anapasa kufanya matendo kwa kuzingatia masharti yote ya muda na sehemu inayomzunguka.

Jambo linalofuata katika mtindo wa maisha ya Kiislamu ni kuzingatiwa mtu binafsi na jamii. Uislamu siku zote unawashauri wafuasi wake wafanye ibada pamoja na kimjumuiko. Hata kama idadi ya mkusanyiko huo itakuwa ni ya watu wawili tu, itakuwa ni bora kuliko ibada ya mtu mmoja na binafsi. Kutekeleza pamoja ibada ya Hija au kuswali jamaa ni jambo muhimu sana katika Uislamu. Utaratibu katika ibada, haswa unapokuwa na dhihirisho la kijamii, huonyesha mshikamano na umoja wa Umma wa Kiislamu, mshikamano na umoja ambao unapasa pia kuwa katika nyoyo za waumini. Mshikamano na umoja huo wa nyoyo hupatikana pale Waislamu wanapokuwa chini ya uongozi wa kiongozi mmoja na kufuata amri zake. Bila shaka, kiongozi ambaye Waislamu wanapasa kumfuata anapasa kutofanya  dhambi wala makosa, au kwa ibara nyingine awe ni mtu maasumu. Iwapo Imam Maasumu hayupo, umma wa Kiislamu, unahitaji kumfuata mtu ambaye ni mjuzi wa dini na kanuni zake na kuzitekeleza kivitendo, ili kudumisha umoja na mshikamano katika kamii ya Kiislamu.

Mtu huyo lazima awe na mwamko unaohitajika wa kisiasa na kijamii na ujasiri wa kusimama mbele ya ukandamizaji na dhulma. Kumfuata mtu wa namna hii kunaweza kuulinda umma wa Kiislamu hadi kudhihiri tena kwa Imam Maasumu.

Kutokana na kuwa mtu binafsi na jamii ni muhimu katika Uislamu na ukuaji na ukamilifu wao wa kidini na kidunia daima hutimia pamoja, ibada zote katika Uislamu zina sura ya mtu binafsi na ya kijamii na hivyo funga pia haiko nje ya kanuni hii. Sura ya mtu binafsi katika kufunga, ni juhudi zake za kujitakasa na kuboresha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu, ilihali sura ya kijamii ya funga ni kuzingatia, kuelewa na kukidhi mahitaji ya watu wasiojiweza katika jamii hiyo. Kwa kuvumilia njaa na kiu, Waislamu wanaelewa vyema hali ya wahitaji ambao hawana uwezo wa kujikimu. Wakiwa na ufahamu huu, wanaweza kutekeleza vizuri zaidi majukumu ambayo mwenyezi Mungu amewapa ili kukidhi mahitaji ya wenzao. Katika mwezi wa Ramadhani, Waislamu huandaa chakula na kuwaalika wahitaji ili wapate kula na kunufaika na chakula hicho.

Kwa pamoja, hujaribu kulipa madeni ya wadaiwa na kusaidia kuachiliwa huru wafungwa ambao wanakabiliwa na matatizo ya kifedha. Kuandaa mazingira yanayofaa ya kuanza maisha na ajira kwa ajili ya vijana pia ni miongoni mwa mambo ambayo Waislamu huyazingatia zaidi katika mwezi huu mtukufu. Kwa kufanya mambo hayo ya kijamii, huwa wamefanikisha mahusiano yao ya kijamii na hivyo kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Kupata radhi za Mwenyezi Mungu hakuna uhusiano wowote na utawa wala kujitenga kijamii bali kunapatikana ndani ya jamii yenyewe.

Swala ya jamaa ni moja ya nembo za ibada za kijamii katika nchi ya Kiislamu

Uislamu unazingatia sana kuchungwa utaratibu katika kufanya mambo na umebainisha nyakati na sehemu maalumu za kufanyia ibada zote. Waislamu popote walipo duniani huswali kwa wakati maalumu na kuelekea kibla kimoja. Huenda Hijja kwa wakati maalumu na kwa kufuata adabu na taratibu maalumu na kufunga kwa njia na namna maalumu. Katika mwezi wa Ramadhani, Waislamu huamka kabla ya jua kuchomoza, kula chakula chepesi na kumwabudu Mwenyezi Mungu, na kujiepusha na chakula au kinywaji chochote kuanzia sauti ya muadhini alfajiri hadi jioni wakati wa Maghrib. Kuzingatia utaratibu na nidhamu katika Uislamu ni muhimu sana kiasi kwamba Imam Ali (as) katika dakika za mwisho za maisha yake humu duniani, na baada ya kuwasihi wanawe na wafuasi wake kuchunga mipaka ya ucha-Mungu na kuzingatia imani, aliwataka wazingatie utaratibu na nidhamu katika mambo yao. Kama yalivyo mambo mengine yote utaratibu na nidhamu pia ina sura ya dhahiri na ya ndani. Imam Ali (as) katika barua kwa mmoja wa masahaba zake wema, Malik Ashtar, anaeleza kiini cha nidhamu na kumshauri kwa kusema: "Usiharakishe kufanya mambo ambayo wakati wake haujafika, usiwe mvivu katika kutekeleza mambo yanayoweza kufanywa, usisisitize kufanya mambo ambayo hayaeleweki vyema, na fanya mambo yanapaokuwa wazi. Fanya kila jambo mahali na kwa wakati wake."

Mambo haya yote, yaani, kuzingatiwa mahusiano ya kijamii na ya mtu binafsi, kuzingatia mambo ya ndani sambamba na kufungamana na dhihiri na kutekeleza mambo kwa umakini, ni mambo ambayo yamezingatiwa na dini zote za mbinguni, lakini yamekuwa yakipuuzwa na baadhi ya wafuasi potovu wa dini hizo. Pengine kuwepo kwa mikengeuko hiyo ndiko kulimfanya Mwenyezi Mungu awakumbushe watu amri zake kupitia dini ya kipekee ya Uislamu.

Mtindo wa maisha wa kila mtu au jamii hutokana na aina ya imani, mtazamo na maadili yanayomtawala mtu au jamii hiyo. Mitazamo na maadili ya kimaada huunda mtindo wa maisha unaoambatana na maadili hayo. Katika upande wa pili mitazamo, maadili na thamani za kiungu huandaa mtindo wa maisha ambao unaendana na thamani za kiungu. Katika maisha ya Kiislamu, kuifahamu Qur'ani na kufuata maelekezo yake ni moja ya nguzo za msingi na muhimu katika maisha ya aina hii. Tangu siku ya kwanza ambapo Mtume Mtukufu (saw) aliitambulisha dini yake kuwa ni mfumo wa ulimwengu kwa wanadamu wote, katika hotuba na kauli zake zote, alitumia na kutolea hoja Aya tukufu za Qur'ani. Katika zama ambazo mawingu meusi ya shirki, dhulma na ujahili yalijaza giza anga ya maisha ya mwanadamu na kusimamisha ubinadamu, ni Aya za Qur'ani ndizo zilifungua njia ya ubinadamu katika giza hilo. Kwa mafundisho yake yaliyo hai na yenye uzima wa milele kwa mwanadamu, Qur'ani huvutia upande wake nyoyo na kuwaonyesha wanadamu njia ya mfumo na mtindo sahihi wa maisha.

Bila shaka, hatua muhimu na ya juu zaidi ya kuifahamu Qur'ani Tukufu ni kufuata mafundisho yake. Kitabu hiki cha mbinguni kina miongozo na mafundisho yenye thamani kubwa katika kumwongoza mtu binafsi na jamii nzima kwa ujumla. Ikiwa miongozo hii itafahamika na kutekelezwa ipasavyo, ulimwengu utachukua muelekeo tofauti na kuondokana na minyororo ya maovu na uharibifu. Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran anatoa wito kwa kila mtu kufuata miongozi na mafundisho ya Qur'ani na kusisitiza: “Iwapo tunaamini kuwa kutekeleza mafundisho ya Qur’ani ndio msingi wa kuihuisha na kwamba suala hilo haliishii tu kwenye kuisoma, tunapasa kuifanya jamii yetu kuwa ya Qur’ani, matendo yetu yawe ya Qur’ani, tuiamini Qur'ani na kuzichukulia ahadi za Qur'ani kuwa ni za kweli na haki."

Tangu kuteremshwa kwake, Qur’ani imevutia nyoyo za mabilioni ya watu, na kufikia sasa watu wa matabaka mbali mbali hutumia muda wao mwingi kusoma, kutafakari, kuhifadhi na kufasiri Qur’ani ili kuzifariji nyoyo zao kwa nuru inayopatikana humo. Kwa mujibu wa wanazuoni na wataalamu wa Qur’ani, iwapo wanadamu watadiriki vyema thamani kubwa zilizomo katika maandiko ya Qur'ani kwa ajili ya kuendeshea maisha yao, bila shaka watakikumbatia kitabu hicho kitakatifu kwa moyo mkunjufu na shauku kubwa.

Ni matumaini yetu kwamba sisi pia katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, tutapata taufiki ya kushikamana kikamilifu na Aya za Qur'ani ikiwa ni katika juhudi za kuimarisha mtindo wa maisha ya Kiislamu na Qur'ani......Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags