Feb 02, 2023 12:30 UTC
  • Afajiri Kumi, Mja Mwema

Tunakaribia Afajiri Kumi za mwaka wa 44 wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Tumekutayarishieni vipindi kadhaa maalumu kwa mnasaba huu ambavyo tunatumai vitakunufaisheni nyote wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, karibuni.

Imam Khomeini (MA) ambaye ni mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alilazimika kuishi uhamishoni kwa kipindi cha karibu miaka 14, yaani tangu tarehe 4 Novemba 1964 hadi 21 Januari 1979, kutokana a harakati zake za kisiasa na mapambano dhidi ya utawala wa kitaghuti wa Shah, kibaraka wa nchi za Magharibi nchini Iran. Tarehe 4 Novemba alikimbia nchi kwa siri na kuelekea Ankara na kisha katika mji wa Bursa huko Uturuki. Baada ya muda, alihamia mjini Najaf Iraq tarehe 23 Agosti 1965 na kuishi huko kwa muda hadi pale mashinikizo ya kumtaka ahamie kwingine yalipoongezeka na kumlazimu ahamie Ufaransa. Hatimaye alihamia katika kitongoji cha Nofel Loshato (Neauphle-Le-Chateau) nchini Ufaransa tarehe 23 Septemba 1978 baada ya mashinikizo hayo ya Shah Muhammad Reza kuongezeka dhidi yake. Katika kilele cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran kitongoji cha Nofel Loshato kiligeuka kuwa kitovu cha mapinduzi. Wakati walimpomlazimisha Imam Khomeini (MA) kuhamia Uturuki, Shah na Marekani hawakuwahi kutabiri kwamba siku moja angerejea Iran kwa kishindo na kuupindua utawala wa kifalme wa Shah.

Alfajiri ya tarehe 12 Bahman, yaani 1 Februari 1979, ndege iliyokuwa imembeba Imam iliruka kutoka uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris ikielekea Iran. Wakati swala ya alfajiri ulipowadia, Imam na ujumbe aliokuwa ameandamana nao waliswali pamoja swala ya jamaa. Wakati ndege ilipoingia katika anga ya Iran, mwandishi habari mmoja alimuuliza Imam: 'Je, una hisia gani wakati huu?' Imam huku akiwa ametulia kabisa alimjibu: 'Sihisi chochote'. Imam hakuwa na hisia yoyote maalumu wakati huo kwa sababu alikuwa anatekeleza tu jukumu lake la kidini. Ushindi au kushindwa kwake yeye yalikuwa ni mamoja na jambo la kupendeza. Kama ambavyo kushindwa hakungevunja moyo, ushindi kwake pia haungemfanya binafsi awe na hali fulani maalumu kihisia.

Hivyo tarehe 12 Bahman 1357 Hijiria Shamsia sawa na Mosi Februari 1979 Imam Khomeini (MA) alipata mapokezi makubwa zaidi kuwahi kurekediwa katika historia. Siku hii ni moja ya siku zenye kumbukumbu kubwa na ya kuvutia zaidi katika zama hizi na kwa hakika shauku na furaha waliyokuwanayo wananchi wa Iran katika mapokezi hayo haiwezi kusifika wala kubainishwa kwa maneno.

Imam alipokuwa anarejea nchini tarehe Mosi Januari 1979

Hivi sasa Mapinduzi ya Kiislamu yameingia katika mwaka wake wa 44. Ni wazi kuwa moja ya sababu za kufanikiwa mapinduzi hayo ni nafasi aliyokuwanayo Kiongozi shupavu na mwanasiasa mcha-Mungu, Imam Khomeini (MA). Akiwa ni mwanazuoni mashuhuri, mwanafikra mwenye mwamko na mwanasiasa aliyetambua vyema changamoto za wakati wake, Imam Khomeini alitumia uzoefu na mafundisho ya Mtume Mtukufu (saw) pamoja na Maimamu watoharifu (as) na hivyo kufanikiwa kuokoa taifa ambalo lilikuwa limekandamizwa na kupokonywa uchangamfu na uhuru wake na kuweza kulirejesha tena katika uwanja sahihi wa maisha yake ya kawaida kijamii. Hayo yote yalifanyika katika kipindi na zama ambazo dini ilikuwa imepigwa vita vikubwa na kuwekwa pembeni kabisa. Kwa kufanya hivyo Imam alifanikiwa pakubwa katika kuanzisha serikali na utawala uliosimama juu ya msingi wa matakwa ya wananchi katika kalibu ya katiba ya Jamhuri ya Kiislamu, inayosimamia na kutetea uadilifu, uhuru na kujitawala. Alifanikiwa kubuni serikali aliyosimama juu ya msingi wa matakwa ya wananchi na mafundisho ya dini na kuweza kuliakisi hilo katika katiba, jambo ambalo liliharakisha mwenendo wa ustawi, marekebisho na ukarabati wa miundombinu nchini. Kwa kufanikisha jambo hilo Imam (MA) aliweza kubuni serikali ya Kiislamu katika zama hizi na hivyo kuwacha nyuma urithi wake wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Mrithi wake ambaye si mwingine bali ni Ayatullah Ali Khamenei anamsifu Imam Khomeini (MA) kuwa ni 'Muumini Mcha-Mungu na Mwanamapinduzi' ambapo katika kulifafanua hilo anasema: Mojawapo ya majina na sifa ambazo zimetumika mara chache sana na sisi pia tumelitumia mara chache sana kuhusu Imamu wetu mpendwa, ni jina hili. Siku zote tunamtaja Imam kwa sifa nyingi, lakini sifa hii - ambayo tunaitumia mara chache sana kumuhusu Imam - ni sifa hii pana ambayo ni; 'Muumini, Mcha- Mungu na Mwanamapinduzi.'

Muumini: Maana yake ni mtu anayemwamini Mungu, anayeamini kufikia lengo fulani, anayeamini njia ambayo itamfikisha kwenye lengo hilo na pia anawaamini wananchi. Ufafanuzi huu pia umetajwa katika Qur'ani Tukufu kuhusu Mtume Mtukufu (saw) ambapo inasema kuwa yeye anamwamini Mwenyezi Mungu, njia itakayomfikisha kwenye lengo na anawaamini pia watu.

Yeye ni mtumwa, ni mwabudu; Yaani yeye anajiona kuwa mtumwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Hii pia ni sifa muhimu sana. Tazameni, ndani ya Qur'an, Mwenyezi Mungu amemsifu Mtume Mtukufu (saw) kwa sifa nyingi, ambazo kila moja inaeleza pande nyingi za sifa za Mtume; Lakini sifa ambayo sisi Waislamu tumeamrishwa kuirudia kila siku kuhusu Mtume katika swala zetu ni hii inayosema: “Ninashuhudia kwamba Muhammad ni mja (mtumwa) na mjumbe wake”; Hili linaonyesha umuhimu wa utumwa. Utumwa ni muhimu sana kiasi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anawafundisha Waislamu kurudia sifa hii mara kadhaa kila siku katika swala zao. Imam alikuwa na sifa hii, sifa ya utumwa. Alikuwa mnyenyekevu, mtu wa kuomba dua, alikuwa mtu wa maombi; muumini mcha Mungu. Lakini sifa ya tatu, yaani, muumini mcha-Mungu mwanamapinduzi... Imam alikuwa mapinduzi hasa."

Shakhsia huyu aliyezingatia sana mafundisho ya dini, aliposhika hatamu za uongozi na kurejea nchini kwake, aliwasilisha upeo mpya wa Uislamu kama dini iliyoendelea, kustawi na kukamilika katika pande zote na ambayo inaambatana kikamilifu na maisha ya mwanadamu na kumkidhia mahitaji yake yote. Kwa hiyo, watu walimwamini na kufuata yote aliyosema. Imam alitoa ufafanuzi sahihi wa dini na akaitambulisha katika nyanja zote za maisha yao. Alileta mtazamo mpya kuhusu Uislamu na kuwasilisha fikra mpya ya "Uislamu halisi wa Mohammadi (saw)." Kwa mtazamo huo, Uislamu haukujumuisha tu nasaha za kimaadili na kiibada bali ulikuwa dhihirisho la rehema na neema ya Mwenyezi Mungu, ambapo uliweza kukidhi mahitaji yote ya mwanadamu, ya humu duniani na Akhera. Huu ni Uislamu ambao ulishughulikia masuala yake yote ya kisiasa, kijamii, kiuchumi n.k.. Huu ni Uislamu ambao ulikuwa na sheria madhubuti na za wazi kwa ajili ya kumuhudumia mwanadamu katika mahitaji yake yote ya kimaada na kimaanawi.

Kwa fikra hiyo mpya, Imam aliweza kuanzisha shule mpya ya kifikra. Katika shule hiyo ya Imam Khomeini (MA), ulimwengu na mfumo wa uumbaji uko mbele na katika udhibiti kamili wa Mwenyezi Mungu, ambapo viumbe wote wako mbele yake, na wanaweza kuwasiliana moja kwa moja na Muumba wao. Kwa hivyo maishani, mtu anapaswa kufuata njia ambayo itamuwezesha kufahamu fika kwamba daima yuko mbele ya Mwenyezi Mungu. Imam Khomeini alikuwa na mtazamo wa kuwa na upendo mkubwa kwa Mwenyezi Mungu, mwanadamu na ulimwengu.

Mmoja wa watu wa karibu na Imam Khomeini (MA) anasema kuwa kwa muda wa miaka 50 Imam hakuwahi kuwacha kuswali swala za usiku. Iwe ni katika hali ya afya nzuri au ugonjwa, kwenye jela au huru nje ya jela, uhamishoni au hospitalini Imam daima alikuwa akitekeleza ibada hiyo muhimu ya swala za usiku. Wakati mmoja Imam alikuwa mgonjwa mjini Qum na madaktari wakashauri ahamishiwe mjini Tehran kwa ajili ya kupata matibabu zaidi ya maradhi ya mayo. Siku hiyo kulikuwa na baridi kali na na barabara ya kuelekea Tehran ilikuwa imeganda barafu. Imam alilazimika kubakia kwenye ambulenzi kwa masaa mengi lakini pamoja na hayo hakuadha kuswali swala ya usiku alipofikishwa hospitalini. Usiku ule alipokuwa akirejea mjini Tehran kutoka Paris watu wote waliokuwa kwenye ndege walilala lakini Imam hakupitwa na swala hiyo muhimu ya usiku ambayo aliswali katika orofa ya juu ya ndege. Ama kwa kweli Imam alikuwa mfano halisi wa Aya ya 16 ya Surat as-Sajdah inayosema:

Mbavu zao zinaachana na vitanda kumwomba Mola wao kwa khofu na kutumaini, na hutoa katika yale tuliyowaruzuku.

Ni kutokana na ukweli huo ndipo Ayatullah Khamenei akamzungumzia Imam kwa kusema: "Kile ambacho kilimuwezesha Imam kuongoza taifa na Mapinduzi haya makubwa ni mawasiliano, mafungamano, mazingatio na kutawakali kwake kwa dhati kwa Mwenyezi Mungu. Alikuwa mtumwa na mja mwema. Sipati ibara nyingine bora zaidi kuliko hii kumuhusu Imam."

Kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, watu wa Iran walipata fursa ya kuketi kwenye meza ya chakula iliyoandaliwa na Imam Khomeini (MA). Alianzisha mapinduzi ambayo yalihuisha dini na umaanawi duniani, mapinduzi ambayo yalipiga vita na kupambana na dhulma pamoja na ubeberu wa madola makubwa yenye kiburi duniani. Utukufu, heshima, uhuru na kujitawala ni nembo na malengo muhimu ya mapinduzi haya. Moyo wa umaanawi na maadili pamoja na kuzingatia makatazo na maamrisho ya Mwenyezi Mungu uliimarishwa miongoni mwa watu na wakati huo huo maendeleo na ustawi wa nchi ukaboreshwa. Hii leo pia ambapo Mapinduzi ya Kiislamu yametimiza miaka 44, na licha ya kuwepo shari, usaliti na njama zinazofanywa na madola ya kibeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ushirikiano wa vibaraka wao wa ndani ya nchi, lakini bado Mapinduzi haya yamesimama imara na jina la Imam linaendelea kunawiri katika nyoyo za wananchi na kuwapa matumaini zaidi maishani.

Tags