May 23, 2023 07:31 UTC
  • Siku ya Mwalimu, kumbukumbu ya kuuawa shahidi Ayatullah Murtadha Mutahhari

Tarehe 12 Ordibehesht kwa mwaka wa Hijria Shamsia (Mei Pili) ni siku ya kumbukumbu ya kuuliwa shahidi mwalimu mahiri na hodari, Ayatullah Murtadha Mutahhari, ambaye siku ya kuuliwa kwake inatambuliwa kuwa ni siku ya kumuenzi na kumpa heshima maalumu mwalimu nchini Iran.

Mwalimu katika utamaduni wa Uislamu anajulikana kama mjenzi wa mwanaadamu na kizazi bora cha kesho, hivyo kumuenzi na kumkirimu ni kuenzi elimu, sayansi na maarifa. Kumthamini na kumuenzi mwalimu ni kumthamini mtunza bustani ambaye huamka asubuhi mapema na kuingia darasani kwa ajili ya kupandikiza mbegu za kesho yenye matumaini kwenye matawi ya nyoyo za wanafunzi wake. Mtume wetu Muhammad (saw) ambaye ndiye mwalimu wa walimu wote anasema:

 إنّ مَثَلَ العُلَماءِ کمَثَلِ النُّجومِ فی السّماءِ یُهتَدى بِها فی ظُلُماتِ البَرِّ و البَحرِ ، فإذا انطَمَسَتِ النُّجومُ أوشَکَ أن تَضِلَّ الهُداةُ 

“Mfano wa wanachuoni ni kama mfano wa nyota za mbinguni; zinaongoza wanaadamu njia nyoofu katika giza la nchi kavu na baharini, na zinapozima yumkini wakapotea njia.”

Ayatullah Murtadha Mutahhari

Elimu huongeza thamani ya mwanaadamu na ustawi wake wa kiakili, na mwalimu ndio njia ya kujifunza na kupata maarifa; hivyo, ana haki kubwa juu ya mabega ya wanafunzi na jamii nzima kwa ujumla. Mwalimu hulinda amana za Mwenyezi Mungu dhidi ya uchafu na upotofu na hujaribu kuwatayarishia wanafunzi wake mazingira mazuri ya kuelekea kwenye ukamilifu kwa mafundisho na malezi yake. Mtume Muhammad (saw) amesema:

:قال رسولُ اللّهِ صلى الله علیه و آلهم: (إن الله وملائکته وأهل السموات والأرضین، حتى النملة فی جحرها، وحتى الحوت؛ لیصلون على معلم الناس الخیر. 

“Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika na viumbe wa mbinguni na ardhini, hata chungu aliyeko katika kichuguu na samaki wa baharini, wanamswalia (wanamuombea) mtu anayefundisha wanaadamu mambo mema." Mtukufu huyo amewataka wanafunzi kuwaheshimu na kuwaenzi walimu wao na kutekeleza haki zao. Imenukuliwa kwamba, Mtume (saw) alisema mara tatu kwamba: "Mola wangu Mlezi!  Warehemu warithi wangu." Maswahaba waliuliza: "Warithi wako ni kina nani?" Mtume (saw) alisema: "Ni wale wanaofikisha Haditih na Suna zangu kwa watu wote, kisha wakazifundishe kwa Umma wangu."

Alama ya msingi na ya kwanza ya mwalimu bora ni kwamba hufanya juhudi za kumjenga na kumtengeneza mwanaadamu. Qur'ani Tukufu inamtambulisha Mtume Muhammad (saw), ambaye ni mwalimu mkuu katika historia ya mwanaadamu, kuwa anawapenda, kuwahurumia na kuwahangaikia waumini ikisema:

لَقَدْ جاءَکُمْ رَسُولٌ مِنْ أَنْفُسِکُمْ عَزِیزٌ عَلَیْهِ ما عَنِتُّمْ حَرِیصٌ عَلَیْکُمْ بِالْمُؤْمِنِینَ رَؤُفٌ رَحِیمٌ

"Hakika amewajia Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayowataabisha; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma." Upendo na hamu kubwa ya mwalimu ya kutaka kuwaongoza watu ni sifa ya mwalimu mkamilifu na hakuna mwalimu anayeweza kufanikiwa bila shauku na upendo huu. Tunaweza kusema kuwa, moyo huu ndiyo injini na nguvu na kumsukuma mwalimu katika kutoa elimu na malezi. Upendo na shauku ya mwalimu hufanya mazingira ya kielimu kuwa yenye utanashati na harakati. Katika mazingira haya, mwalimu na mwanafunzi hutazama siku zijazo kwa matumaini na kujitahidi kuwa na siku na mustakbali bora na angavu.

Kuwa mwalimu kuna maana ya kuwa msanii, kwa maana ya kutambua vyema sanaa na fani ya ualimu. Ndiyo, kuwa mwalimu si kukusanya maarifa kichwani tu, bali sambamba na kuwa na maarifa na utaalamu, ni lazima mwalimu awe na ujuzi wa kufundisha. Kuwa na ujuzi, maarifa, kutafakari na ubunifu ni miongoni mwa sifa za mwalimu anayeendana na sayansi na elimu ya kisasa. Mwalimu amwenye mafanikio ni mtu anayefahamu maarifa na maendeleo ya kisayansi ya zama zake na anazitumia kufundisha na kuelimisha wanafunzi wake.

Katika upande mwingine, wanafunzi huathiriwa sana na mwalimu wao, kwa sababu ya ushawishi wa kiakili na kiroho wa mwalimu, ambao wakati mwingine hubadilisha hatima ya taifa. Aghlabu ya watu waliofanikiwa maishani huyahusisha mafanikio yao na walimu wao, na kinyume chake pia ni sahihi, kwa maana kwamba wapo watu ambao kufeli na kushindwa kwao katika maisha kumesababishwa na mienendo mibaya na isiyofaa ya walimu wao. Ayatullah Shahidi Murtadha Mutahhari ni miongoni mwa wanazuoni walioathiriwa sana na walimu wao. Anasema kuhusu taathira ya mwalimu wake, Al Haj Agha Mirza Ali Shirazi kwamba: "Alikuwa mtu adhimu. Ndiye aliyenifunisha Nahjul-Balagha kwa mara ya kwanza, na kukutana na kusoma kwake ni moja ya hazina za thamani za maisha yangu ambazo siko tayari kuzibadilisha na chochote. Hakuna mchana au usiku unaopita pasi na kumbukumbu, kumuweka akili mwangu na kutaja jina lake.” 

Mapinduzi ya Kiislamu yana deni kubwa kwa juhudi za kifikra na kitamaduni ambazo zimefanywa na wanafikra na wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu kwa miaka mingi. Ayatullah Mutahhari ni miongoni mwa wanafikra mashuhuri wa zama hizi, ambao wamekidhi mahitaji mengi ya kifikra ya kizazi cha sasa kutokana na ujuzi na utambuzi wao wa kina wa fikra na mafundisho ya Kiislamu. Miongoni mwa sifa kuu za Shahidi Mutahhari ni kuwa na fikra na mawazo mapya, ubunifu na maarifa sahihi ya Uislamu. Ayatullah Mutahhari alikuwa na mchango mkubwa katika kuelimisha wasomi, hasa katika nyanja za kiutamaduni za jamii na ametuachia kazi na vitabu vya thamani ambavyo vimekidhi na kutoa majibu ya kifikra ya vizazi vya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa miaka mingi. Ayatullah Mutahhari aliifasiri dini ya Kiislamu kwa mujibu wa mahitaji ya jamii na kizazi cha vijana, na kufufua maadili ya dini hiyo kwa namna ambayo ilizuia hujuma za kifikra za Kimagharibi na fikra mgando kwa wakati mmoja.

Shahidi Ayatullah Mutahhari alizaliwa tarehe 13 Bahman 1298 Hijria Shamsia (1919) huko Fariman, umbali wa kilomita 75 kutoka mji mtakatifu wa Mash'had, katika familia ya kidini. Baada ya kipindi cha utoto wake, alienda shule na kuanza kujifunza masomo ya msingi. Akiwa na umri wa miaka kumi na mbili, alikwenda katika shule ya seminari ya Mash'had na kusoma misingi ya sayansi na elimu za Kiislamu. Mnamo 1316 Hijria Shamsia (1927), na licha ya vita kali ya Reza Khan dhidi ya wanazuoni wa Kiislamu, alielekea kwenye mji wa Qum kukamilisha masomo yake licha ya upinzani wa jamaa na watu wa karibu yake. Katika kipindi cha miaka 15 ya kuwa kwake Qum, Shahid Mutahhari alijifunza elimu za fiqhi na usulu kwa marehemu Ayatullah Borujerdi na kupata elimu ya falsafa, irfani na maadili kwa Imam Ruhullah Khomeini na Allama Muhammad Hussein Tabatabai. Alihamia Tehran mwaka 1952 na kuanza kufundisha, kutoa mihadhara na kuandika vitabu katika Akademia ya Marv. Mwaka 1955 alifanya kikao chake cha kwanza cha kufunza tafsiri ya Qur'ani katika Jumuiya ya Kiislamu ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu.

Shahidi Murtadha Mutahhari alikuwa miongoni mwa nguzo kuu za kuunda jumuiya ya wanazuoni wa Kiislamu wakati Imam Khomeini alipopelekwa uhamishoni nje ya nchi na utawala dhalimu wa Shah. Alisimama imara kama jabali na mlima katika kuwaongoza wananchi na kufunga njia ya ukengeufu wa aina yoyote katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu. Alikuwa na imani kamili juu ya uwezo wa Uislamu wa kusimamia mambo ya jamii na alianza kueleza na kubainisha mitazamo ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuwasilisha vipengele vyake mbalimbali kwa watu wote.

Katika hali ambayo zilisikika kauli mbalimbali kutoka pande zote za kupigia debe na kueneza mifumo isiyo ya Kiislamu, Shahidi Mutahhar alifuata njia ya Imam Khomeini, na kutetea itikadi za Mapinduzi ya Kiislamu. Mawazo na fikra makini za Ayatullah Murtadha Mutahhari, kama mtaalamu wa taaluma za Kiislamu, mtambuzi wa nyakati, mwanasayansi nguli anayejua matatiizo ya zama na mwanafalsafa hodari, siku zote zimeendelea kuwavutia wasomi na wanafikra hususan viijana wenye kiu ya elimu na maarifa. Alikuwa mtu aliyefanya jitihada kubwa kujibu maswali ya zama na kukabiliana na upotovu wa kifikra na kiitikadi, hadi akatoa mhanga maisha yake katika njia hiyo.

Katika ujumbe wake wa taanzia baada ya kuuliwa shahidi Murtadha Mutahhar kwa kupigwa risasi, Imam Ruhullah Khomeini kiongozi na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: "Nimefiwa na mtoto mpendwa sana na niko katika maombolezo kwa ajili yake. Alikuwa miongoni mwa matunda ya maisha yangu. Kuuliwa shahidi mwana huyu mpendwa na msomi kumetia pengo katika Uislamu, ambalo halitazibwa na kitu kingine chochote."

Imam Khomeini: "Nimefiwa na mtoto mpendwa sana na niko katika maombolezo kwa ajili yake."

Ayatullah Ali Khamenei pia anawahimiza wasomi kupitia na kusoma vyema athari na maandiko ya mwanazuoni huyo mkubwa na kusema: "Kazi za msomi huyo ziko hai kama kumbukumbu yake. Vitabu vya Shahid Mutahhari haviwezi kufa na kumalizika. Jamii yetu, kizazi cha vijana, na jamii ya kitamaduni na kisayansi bado wanahitaji kujua mambo yale yale ambayo msomi huyo ameyaeleza na kuyaandika kwa ajili ya Umma wa Kiislamu.