May 23, 2023 10:59 UTC
  • Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Hujuma Dhidi ya Uislamu

Kwa Waislamu wote duniani, haswa Waislamu wa New Zealand, tarehe 15 Machi ni siku chungu na isiyoweza kusahaulika. 

Mnamo Machi 15, 2019, mtu mmoja aliyekuwa na silaha aliwashambulia na kuwamiminia risasi waumini waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa ndani ya misikiti miwili huko Christchurch, New Zealand na kuwaua Waislamu 51. Gaidi huyo alikamatwa na polisi alipokuwa njiani akielekea kwenye msikiti wa tatu kwa ajili ya kuua Waislamu huko Ashburton. Shambulio hilo lililolenga Msikiti wa al Noor na Kituo cha Kiislamu cha Linwood, linatambuliwa kama mauaji makubwa zaidi katika historia ya sasa ya New Zealand.

Hujuma ya kigaidi ya tarehe 15 Machi mwaka 2019 ni miongoni mwa mashambulizi makubwa ya kigaidi dhidi ya Waislamu katika nchi zinazojinadi kuwa watetezi wa uhuru na haki za binadamu za Kimagharibi. Hapana shaka yoyote kwamba, lau hujuma hii ingetokea dhidi ya Wakristo au Wayahudi, isingepita hata siku moja bila kutajwa mauaji haya ya kikatili, na kungetengezwa filamu nyingi za matukio ya kweli (documentary) na za visa kuhusu maafa hayo. Hata hivyo serikali za nchi za Magharibi haziko tayari kukiri uwepo wa wimbi la chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hizo na zinaficha vitendo vya hujuma zinazoulenga Uislamu na Waislamu chini ya kivuli na kisingizio cha uhuru wa kujieleza.

Mwenendo wa hujuma na chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi umekuwa miongoni mwa mambo ya kawaida katika nchi hizo, na wanasiasa wa mrengo mkali wa kulia wanaopiga vita Uislamu, sasa ndio wanaoshika madaraka katika nchi nyingi za Ulaya. Vyama vingi vya mielekeo ya wastani vya kulia na kushoto pia vimeathiriwa na kaulimbiu na programu za vyama vyenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia vinavyosimamia hujuma dhidi ya Uislamu. Hasa ikitiliwa maanani kwamba, chuki dhidi ya Uislamu sasa imeoana na kuungana na upinzani dhidi ya uhamiaji na wahajiri. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Waislamu wengi barani Ulaya ni wahamiaji na wahajiri kutoka nchi za Afrika na Asia; hivyo wapinzani wa Uislamu na wapinzani wa wahajiri na wahamiaji sasa wameungana na kusimama katika safu moja. François Burgat, mwanafikra Mfaransa na mtafiti mkuu katika Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Kisayansi, anasema: "Chuki na hujuma dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa na barani Ulaya imefikia viwango hatari, na ikiwa hapo awali hujuma hizo zilikuwa zikifanywa na watu wenye mitazamo ya kufurutu mipaka, hii leo serikali zote za bara hilo zinaeneza chuki dhidi ya Uislamu, bali kwa hakika tunaweza kusema kuwa, hujuma dhidi ya Uislamu limekuwa jambo linalosimamiwa na serikali za nchi za bara hilo." 

Kuhusiana na suala hilo, mwezi Juni mwaka jana, mashirika 41 ya kiraia ya Ulaya yaliushutumu Umoja wa Ulaya kwa kushindwa kupambana na chuki na hujuma dhidi ya Uislamu, na katika barua iliyoandikwa kwa umoja huo, mashirika hayo yalitaka kuteuliwa afisa mratibu wa kupambana na chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya. Katika barua hiyo, mashirika haya yalieleza wasiwasi wao juu ya kushindwa kwa taasisi za Umoja wa Ulaya kuchukua hatua zozote za kupambana na chuki dhidi ya Uislamu. 

Hujuma ya kigaidi ya tarehe 15 Machi 2019 katika mji wa Christchurch, New Zealand, ilikuwa ya kikatili na kubwa sana katika nchi salama na ya amani kiasi kwamba, duru za kisiasa na vyombo vya habari havingeweza kuipuuza kiurahisi. New Zealand iko mbali na nchi nyingine zote za dunia, haina uadui na nchi yoyote duniani, na daima ni miongoni mwa nchi salama zaidi kwa vigezo vya viashiria vya usalama. Aghlabu ya nyumba za watu wa New Zealand hazina kufuli, madirisha hayana vyuma vya ulinzi, na kuta zinazozunguka nyua na maboma huwa fupi sana kiasi kwamba unaweza kuingia kwa urahisi katika nyumba za watu. Anga ya miji mingi ya New Zealand ni salama sana, na wizi hushuhudiwa kwa nadra katika maeneo mengi ya nchi hiyo. 

Pamoja na hayo katika nchi hii inayoonekana kidhahiri kuwa salama, hali si salama kwa Waislamu. Mfano wazi ni hujuma ya kigaidi ya 2019. Kabla ya shambulio hilo, gaidi huyo anayepiga vita Uislamu alisema waziwazi kwenye mtandao wa kijamii kwamba alichagua New Zealand kwa ajili ya hujuma hiyo kwa sababu ina vizingiti vichache vya kiusalama na kwamba atakuwa na uhuru zaidi wa kutekeleza mpango wake. Picha za awali za uhalifu huo wa mauaji ya makumi ya Waislamu misikitini zilionyeshwa kwa mara ya kwanza na gaidi huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu. Alipeperusha shambulizi hilo moja kwa moja kwenye Facebook kupitia kamera ya kubeba kichwani na akachapisha manifesto yenye  kurasa 74 kwenye majukwaa ya watu wenye misimamo mikali. Gaidi huyo mbaguzi wa rangi aliyekuwa na umri wa miaka 28 wakati huo, ni raia wa Australia na mwanachama wa chama cha mrengo wa kulia anayejulikana kwa jina la Brenton Harrison Tarrant. Aliwashambulia kwa damu baridi Waislamu katika misikiti miwili na kuanza kuwafyatulia risasi. 

Mwandishi wa habari Richard Pérez-Peña aliandika hivi katika ripoti yake ya Machi 15 katika gazeti la New York Times: “Majeruhi walikuwa wakijaribu kujivuta hadi mahali salama au kulala chini; wengine walijaribu kukimbia au kujificha nyuma ya maiti za watu, lakini katili huyo aliyekuwa na bunduki hakumbakisha mtu yeyote. Hakuwaonea huruma wanawake na wasichana na alijaza risasi kwenye bunduki yake mara kwa mara na kupiga miili ya wafu wasio na uhai iliyokuwa imelala chini." Gaidi huyo katili alirekodi tukio zima la jinai hiyo kubwa na kulionyesha mubashara mtandaoni kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Maziko ya Waislamu New Zealand

Filamu hiyo ilikuwa moja ya matukio ya kushtua na kuhuzunisha sana yaliyoonyeshwa kwenye mitandao ya kijamii. Ripota wa New York Times aliandika kwamba: “Tukio hili la kutisha lilifanyika katika zama ambapo mitandao ya kijamii imeungana na ubaguzi wa rangi. Ni mauaji ya umati, ambayo inaonekana kwamba yamechochewa na chuki ya watu weupe wenye misimamo mikali, na yameonyeshwa moja kwa moja kwenye Facebook na kuenea haraka kwenye anga ya mtandao mithili ya maambukizi ya virusi." Ripota huyo wa gazeti la New York Times anaongeza kwamba: "Shambulio hilo lilisambaratisha hali ya usalama katika mojawapo ya nchi zilizoendelea na salama zaidi duniani." Anaendelea kusimulia kwamba: Mtu mmoja aliyekuwa amesimama kwenye mlango wa msikiti alimuona mshambuliaji na kumwambia: "Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yako ndungu yangu", lakini haikuchukua muda, Muislamu huyo alianguka chini na alipojaribu kutambaa na kwenda mahali salama, alipigwa risasi na kuuawa."

Waislamu waliouawa katika shambulizi la kigaidi New Zealand

Baada ya miaka mitatu ya juhudi za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa ombi la Pakistan, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha siku ya tarehe 15 Machi kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Chuki Dhidi ya Uislamu katika kalenda ya matukio ya jumuiya hiyo, kwenye azimio lililopasishwa mwaka jana, 2022. Hata hivyo serikali za nchi za Magharibi hazikuwa tayari kuunga mkono kwa uwazi uamuzi huu. Nicolas de Rivière, mwakilishi wa kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa amelitaja azimio hilo kuwa lisiloridhisha na lenye matatizo na kuwaambia wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba: "Neno Islamophobia (chuki au hujuma dhidi ya Uislamu) ni kinyume cha uhuru wa dini au imani na hakuna ufafanuzi uliokubaliwa kimataifa kuhusiana na maana yake. Huu ni uhuru ambao Ufaransa inautetea na inatetea uhuru mwingine wote wa umma, kama vile uhuru wa kujieleza."

Msimamo huu wa serikali ya Ufaransa kwa hakika ni himaya na uungaji mkono wa waziwazi kwa magaidi wanaopiga vita Uislamu nchini Ufaransa na duniani kote. Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya unaojumuisha nchi 27 za Ulaya mwenye hadhi ya uangalizi wa kudumu katika Umoja wa Mataifa pia alikariri eti wasiwasi wa mwakilishi wa kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa kuhusu kuainishwa tarehe 15 Machi kuwa siku ya kupambana na chuki dhidi ya Uislamu. Ufaransa ndiyo inayoongoza kati ya nchi za Magharibi katika kuweka vikwazo na vizuizi kwa maisha ya Waislamu kwa kuzingatia imani zao za kidini. Tunaweza kusema kuwa, chuki dhidi ya Uislamu imekita mizizi katika nchi za Magharibi, na uhuru wa kusema ni kifuniko tu cha kuhalalisha ubaguzi na ubaguzi wa rangi na kuunga mkono vitendo vya kigaidi dhidi ya Waislamu. 

Makumi ya Waislamu walioawa wakitekeleza Swala ya Ijumaa, New Zealand

Katika barua zake alizowaandikia vijana wa nchi za Magharibi baada ya matukio ya kigaidi huko Paris, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alizungumzia hatari ya utamaduni wa Magharibi akisema unafanya jinai ukiwa na sifa mbili za uchafu wa kimaadili na ukatili, na unatengeneza magaidi ambao wanahatarisha usalama wa dunia. Leo hii hasira na mishale ya chuki ya wanasiasa wa nchi za Magharibi inaweza kuonekana waziwazi kutokana na moto wa silaha unaoulenga Uislamu na Waislamu wanaodhulumiwa na wasio na ulinzi katika maeneo mbalimbali ya duniani. Tukio la kigaidi la Machi 15, 2019 huko New Zealand ni matokeo ya moja kwa moja ya sera za chuki dhidi ya wahamiaji na Uislamu za serikali za nchi za Magharibi.

Tags