Jan 24, 2021 13:46 UTC
  • Harakati ya Polisario yashambulia kwa makombora kivuko cha Guerguerat kwenye mpaka wa Morocco

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Harakati ya Ukombozi wa Sahara Magharibi Polisario kimeshambulia kwa maroketi kivuko cha Guerguerat kwenye mpaka wa Morocco na kwamba jeshi la nchi hiyo limejibu shambulio hilo.

Ripoti ya toleo la leo la gazeti la Al-Qudsul-Araby imeeleza kuwa, usiku wa kuamkia leo vikosi vya wapiganaji wa harakati ya Polisario vimeshambulia kwa maroketi na makombora ya mizinga kivuko cha  Guerguerat kilichoko kwenye eneo la mpaka wa pamoja wa Morocco na Mauritania.

Serikali ya Morocco inakitumia kivuko hicho kwa ajiili ya kupitishia bidhaa zake kuelekea nchi zingine za Afrika.

Kwa mujibu wa mashuhuda na wasafiri waliokuwa wakipita kwenye kivuko cha Guerguerat, maroketi na makombora ya mizinga yaliyofyatuliwa na harakati ya Polisario yalilenga kivuko hicho na baadhi yao yaliathiri sehemu za kandokando ya kivuko hicho cha mpakani.

Hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu hasara iliyosababishwa na shambulio hilo.

Wafuasi wa Polisasrio wakipeperusha bendera ya harakati hiyo ya Sahara Magharibi

Kwa mujibu wa Al-Qudsul-Araby, ndege za kivita za Morocco zimejibu shambulio hilo la Polisario kwa kushambulia ngome za harakati hiyo.

Harakati ya Sahara Magharibi ya Polisario iliingia vitani na Morocco kuanzia mwaka 1975 hadi 1991 kupigania uhuru wa eneo hilo linalodhibitiwa na serikali ya Rabat.

Usuluhishi wa Umoja wa Mataifa uliwezesha kusitishwa mapigano wakati huo na kuanzishwa mchakato wa mazungumzo kwa ajili ya kuitisha kura ya maoni ya kuamua hatima ya eneo hilo.

Morocco imesema iko tayari kuruhusu Sahara Magharibi ijiendeshee yenyewe masuala yake ya ndani lakini ibaki kuwa sehemu ya ardhi ya nchi hiyo.

Harakati ya Polisario kwa upande wake inasisitiza kuwa, iko tayari kushiriki kwenye mchakato wa mazungumzo ya usuluhishi chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, lakini katu haitaweka chini silaha.../

Tags