Ghana yapinga juhudi za kuzima sheria ya kukabiliana na ushoga
Mahakama ya Kilele ya Ghana imetupilia mbali pingamizi la kisheria lililotaka kuzuiwa Bunge la nchi hiyo kupasisha muswada wa sheria kali ya kukabiliana na vitendo vichafu vya ubaradhuli nchini humo.
Hatua hiyo iliyochukuliwa jana Jumatano na Mahakama ya Juu ya Ghana sasa imefungua mlango wa kupasishwa kwa sheria hiyo. Bunge la Ghana limekuwa likiujadili muswada huo tokea Agosti mwaka 2021, na akthari ya Wabunge wanaunga mkono kupasishwa kwa sheria hiyo.
Muswada huo dhidi ya mahusiano ya watu wenye jinsia moja na watu waliobadilisha jinsia zao (LGBTQ) unaainisha hadi kifungo cha miaka 10 jela kwa wale watakaohusika na uovu huo au kuushajiisha, mbali na kutaka kujinaishwa ufuska huo.
Kwa sasa wanaojihusisha na usenge na usagaji nchini Ghana wanaweza kukabiliana na kifungo cha hadi miaka mitatu jela. Nchi za Magharibi zimetiwa kiwewe na wimbi la nchi za Afrika kupasisha sheria kali za kupambana na ubaradhuli.
Machi mwaka huu, Mbunge wa Ghana katika eneobunge la Ningo Prampram, Samuel George, alimjia juu Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris akiwa safarini nchini Ghana, kwa kuunga mkono na kushajiisha ushoga.
Alisema Harris hana "haki ya kimaadili" ya kuzungumza kuhusu masuala ya haki za binadamu katika taifa hilo la Afrika Magharibi huku kukiwa na vurugu za bunduki katika nchi yake.
Mwanasiasa huyo alisema muswada wa kupinga LGBTQ, ambao umekuwa kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria tangu mwaka jana, utawasilishwa kwa wenzake katika Bunge kwa mjadala zaidi na kupigiwa kura. Amesisitiza kuwa muswada wake huo haukiuki haki za binadamu za raia wa Ghana.