Jul 27, 2023 10:21 UTC
  • Waislamu Nigeria waandamana kulaani kuchomwa moto Qurani

Waislamu nchini Nigeria wamefanya maandamano kulaani vitendo vya mara kwa mara vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni katika jimbo la Bauchi hapo jana waliungana na kufanya maandamano makubwa ya kulaani kuvunjiwa heshima na kuchomwa moto kwa makusudi nakala za Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark.

Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba nakala za Qur'ani Tukufu wamelaani wimbi la vitendo hivyo walivyovitaja kuwa vya kichochezi, visivyokubalika na vinavyokusudia kuumiza nyoyo za Waislamu bilioni mbili kote duniani.

Waislamu wa Kishia na Kisunni walioshiriki maandamano hayo jana Jumatano jimboni Bauchi wamesema kuvunjiwa heshima kitabu chochote kitakatifu kwa kisingizio cha uhuru wa kusema ni jambo lisilo na mantiki.

Mgeni wa heshima kwenye mkusanyiko huo wa jana alikuwa Sheikh Salamul Ali, Mkuu wa Hauza ya Shahid Sadr iliyoko katika mji mtukufu wa Qum hapa nchini Iran, ambaye ameitanabahisha dunia kuhusu hatari ya kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu.

Malam Isa Bello, mmoja wa waandamanaji hao amesema hatua ya serikali za Ulaya kuruhusu kuvunjiwa heshima Kitabu hicho Kitukufu cha Waislamu kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, kwa mara nyingine tena imeonyesha unafiki na undumakuwili wa madola ya Magharibi. Amesema, "Qurani ni mstari wetu mwekundu, na hatuwezi kumfumbia macho yeyote anayejaribu kuuvuka mstari huo."

Waislamu katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Iran, Iraq, Lebanon, Yemen na Uturuki wamefanya maandamano makubwa na kulaani wimbi la vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark.

Tags