Uwezekano wa shambulio la kijeshi dhidi ya Niger wazidi kupata nguvu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101276-uwezekano_wa_shambulio_la_kijeshi_dhidi_ya_niger_wazidi_kupata_nguvu
Huku mzozo wa kisiasa nchini Niger ukiendelea, ECOWAS (Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi) imeamua kufanya shambulio la kijeshi dhidi ya nchi hiyo, lakini haijatangaza tarehe ya kuanza shambulio hilo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 20, 2023 11:13 UTC
  • Uwezekano wa shambulio la kijeshi dhidi ya Niger wazidi kupata nguvu

Huku mzozo wa kisiasa nchini Niger ukiendelea, ECOWAS (Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi) imeamua kufanya shambulio la kijeshi dhidi ya nchi hiyo, lakini haijatangaza tarehe ya kuanza shambulio hilo.

Abdulfattah Musa, Kamishna anayehusika na Masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama wa ECOWAS, baada ya kukutana mjini Accra Ghana na wakuu wa vitengo tofauti vya kamisheni hiyo, huku akitangaza habari hiyo amedai kwamba uingiliaji wowote wa kijeshi nchini Niger utakuwa wa muda mfupi na kuwa utalenga kurejesha mpangilio wa kidemokradia nchini humo kwa msingi wa katiba.

Abdul Fattah Moussa, Kamishna wa Masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama wa ECOWAS 

Huku uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi nchini Niger ukizidi kuongezeka, habari zinasema kuwa ndege za kivita za Mali na Burkina Faso tayari zimekwishatumwa nchini Niger. Burkina Faso na Mali, ambazo nazo zimeshuhudia mapinduzi ya kijeshi kama Niger katika miezi sita iliyopita, zimetangaza kupitia taarifa ya pamoja kwamba uingiliaji wowote wa kijeshi dhidi ya Niger utachukuliwa kuwa tangazo la vita dhidi ya nchi hizo mbili na hivyo zitalazimika kuingilia vita hivyo.

Mapinduzi ya Niger yalifanywa Julai 26, 2023 ambapo walinzi wa rais walimkamata Rais Mohammad Bazoum na kutangaza kuipindua serikali yake. Kufuatia mapinduzi hayo, Jenerali Abdul Rahman Tiani alitangaza kuchukua madaraka ya nchi.

Tangu mwanzo, mapinduzi hayo yamekabiliwa na msimamo mkali wa nchi nyingi wanachama wa ECOWAS pamoja na nchi za Magharibi, hasa Ufaransa na Marekani. Ufaransa ilitangaza tangu mwanzo kwamba ingeunga mkono ECOWAS katika shambulio lolote la kijeshi dhidi ya wanajeshi wafanyamapinduzi wa Niger.

Pamoja na hayo mapinduzi ya Niger yanaungwa mkono na raia wengi wa nchi hiyo ambapo maelfu wanapinga vikali uwepo wa kijeshi wa Ufaransa katika ardhi yao. Wanamchukulia Bazem kuwa kibaraka wa nchi za Magharibi hususan Ufaransa hivyo wanaunga mkono kuondolewa kwake madarakani na kuzitaka nchi za Magharibi kutoingilia mambo ya ndani ya nchi yao.

Niger ni nchi muhimusana kwa Ufaransa. Madini muhimu yakiwemo ya urani ambayo yanadhamini zaidi ya asilimia 30 ya nishati inayotumika katika vinu vya nyuklia vya Ufaransa, ni miongoni mwa sababu muhimu zinazoipelekea Paris kuizingatia sana Niger. Vilevile nchi hii inachukuliwa kuwa ngome ya mwisho ya Ufaransa barani Afrika, hivyo kuipoteza kutatoa pigo kubwa kwa Wafaransa. Hio ndio maana Ufaransa inatumia kila mbinu inayowezekana kumrudisha madarakani rais aliyepinduliwa wa Niger na hivyo kuimarisha nafasi yake katika nchi hiyo.

Ni kwa kuzingatia hali hiyo ndipo Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Waislamu wa Nigeria akatahadharisha dhidi ya fitna za Ufaransa na Marekani katika nchi za eneo hilo na kusema: Nchi mbili hizi ndizo chanzo kikuu cha mgogoro wa Nigeria na Niger.

Nchi wanachama wa ECOWAS

Ijapokuwa ECOWAS imetangaza utayari wake wa kuishambulia kijeshi Niger na wakuu wengi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo pia kukaribisha uamuzi huo, lakini kiutendaji, wengi wanaona kuwa ECOWAS haina nguvu za kijeshi wala kifedha zinazohitajika kwa ajili ya operesheni hiyo. Jarida la Wall Street Journal la Marekani hivi karibuni lilimnukuu kamanda wa kijeshi katika moja ya nchi wanachama wa ECOWAS ambaye hakutaka jina lake litajwe, akitilia shaka uwezekano wa uingiliaji huo wa kijeshi na kusema: Maandalizi ya kuingilia kijeshi kwa lengo la kukomesha mapinduzi nchini Niger yanaweza kuchukua miezi 6.

Kwa upande mwingine, inaonekana kuwa suala la mashambulizi dhidi ya Niger limekuwa suala la heshima kwa ECOWAS, ambapo jumuiya hiyo itapoteza itibari yake iwapo tishio hilo halitatekelezwa. Hata hivyo, baadhi ya nchi zinazotaka Niger ishambuliwe pia zimeingiwa na shaka kuhusu suala hilo.

James Barnett, mkuu wa Taasisi ya Hudson nchini Marekani, anasema: "Hivi sasa, mgawanyiko mkubwa wa kikanda unaendelea Afrika Magharibi, na haya yatakuwa machafuko na kuchanganyikiwa kukubwa."

Kwa vyo vyote vile, ni wazi kuwa siku zijazo zitakuwa siku muhimu kwa hatima ya Niger na nchi zote za Afrika Magharibi.