Nchi za Kiafrika zakosoa ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10141-nchi_za_kiafrika_zakosoa_ukandamizaji_wa_israel_dhidi_ya_wapalestina
Kundi la nchi 54 za bara Afrika limekosoa vikali ukandamizaji na dhulma zinazofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika ardhi zao unazozikalia kwa mabavu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 28, 2016 03:17 UTC
  • Nchi za Kiafrika zakosoa ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina

Kundi la nchi 54 za bara Afrika limekosoa vikali ukandamizaji na dhulma zinazofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika ardhi zao unazozikalia kwa mabavu.

Kikao cha jana cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa cha kujadli rekodi ya haki za binadamu ya utawala haramu wa Israel mjini Geneva nchini Uswisi, kilishuhudia matamshi makali kutoka viongozi wa Afrika waliotaka kukomeshwa mara moja kughusubiwa ardhi za Wapalestina, mzingiro dhidi ya watu milioni mbili wa Ukanda wa Gaza, kukamatwa na kuzuilia kinyume cha sheria kwa Wapalestina sawa na jinai zingine wanazotendewa wananchi madhulumu wa Wapalestina na utawala katili wa Israel. Taarifa ya kundi hilo linalojiita African Group mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa imeitaka jamii ya kimataifa kutekeleza wajibu wake na kusimama dhidi ya ukandamizaji wanaofanyiwa Wapalestina sambamba na kukanyagwa haki zao za msingi. Walowezi wa Kizayuni wapatao nusu milioni wanaishi katika vitongoji haramu 230 vilivyojengwa na utawala ghasibu wa Israel tangu mwaka 1967 katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds tukufu, kinyume na sheria za kimataifa. Aidha Wapalestina zaidi ya 7,000 wanazuiliwa katika mazingira ya kuogofya katika jela zipatazo 17 za utawala haramu wa Israel.

Haya yanajiri katika kipindi hiki cha kukaribia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo ni Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.