Raia 49, askari 15 wauawa katika mashambulizi ya kigaidi Mali
(last modified Fri, 08 Sep 2023 07:41:19 GMT )
Sep 08, 2023 07:41 UTC
  • Raia 49, askari 15 wauawa katika mashambulizi ya kigaidi Mali

Makumi ya raia na wanajeshi wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na magenge ya wabeba silaha kaskazini mashariki mwa Mali.

Duru za habari zimeliarifu shirika la habari la Reuters kuwa, wanamgambo hao jana Alkhamisi walivamia kambi ya jeshi katika mji wa Bourem Circle eneo la Gao na kufanya ukatili wa kutisha. 

Habari zaidi zinasema kuwa, raia 49 na wanajeshi 15 wameuawa katika shambulizi hilo dhidi ya kituo cha kijeshi na jingine lililolenga boti, huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.

Serikali ya mpito ya Mali hata hivyo imesema imewaangamiza wanamgambo zaidi ya 50 katika shambulizi la kulipiza kisasi, huku ikitangaza siku tatu za maombolezo.

Katika shambulizi la pili, genge la kigaidi lisilojulikana lilishambulia boti iliyokuwa imebeba raia katika mto uliopo baina ya miji ya Gao na Mopti, na kuua kadhaa miongoni mwao.

Mwishoni mwa mwezi uliopita pia, raia wasiopungua 21 waliuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na wanachama wenye mfungamano na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) katika eneo la Mopti, katikati ya Mali.

Askari wa Umoja wa Mataifa nchini Mali

Mashambulizi hayo ya umwagaji damu yanaendelea kushuhudiwa licha ya uwepo wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA. Mali imetaka kuondoka kwa vikosi hivyo vya kigeni katika ardhi yake. Aidha wananchi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara ya kutaka kufukuzwa kwa majeshi hayo ajinabi.

Tayari kikosi hicho kimekamilisha awamu yake ya kwanza ya kuondoka kikamilifu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Msafara wa mwisho wa ujumbe huo kulinda amani uliondoka kwenye kambi ya Menaka ya kaskazini mashariki mwa Mali tarehe 25 ya mwezi uliopita wa Agosti.