Sep 17, 2023 04:39 UTC
  • Hilali Nyekundu ya Iran yatuma misaada ya kibinadamu Libya

Mkuu wa Shirika la Hlilali Nyekundu la Iran (IRCS) amesema jumuiya hiyo imetuma tani 40 za misaada ya dharura nchini Libya, kufuatia maafa makubwa ya roho na mali za watu yaliyosababishwa na mafuriko makubwa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Pir-Hossein Kolivand amesema shehena ya misaada ya binadamu na ya dharura iliyotumwa nchini Libya na Hilali Nyekundu imesheheni mahema, mablangeti, mazulia, vifurushi vya chakula, bidhaa za usafi n.k.

Amenukuliwa na shirika la habari la Iran Press akisema, timu tatu za waokoaji na wahudumu wengine zimetumwa nchini humo kwenda kusaidia katika shughuli za kusaka manusura na kusambaza misaada hiyo ya Hilali Nyekundu kwa waathiri wa mafuriko.

Huku akiashiria juu ya wajibu wa kidini na kibinadamu wa kuwasaidia waathiriwa na wanaohitaji misaada, Mkuu wa Shirika la Hlilali Nyekundu la Iran ameeleza kuwa, "IRCS kama mwanachama wa Harakati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, inafanya kadri iwezavyo kuwasaidia wahanga wa ajali na majanga kote duniani."

Pir-Hossein Kolivand, Mkuu wa Shirika la Hlilali Nyekundu la Iran

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA limesema watu 900,000 nchini humo wameathirika, mbali na watu wengine 300,000 ambao tayari wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Limesema mahitaji ya dharura zaidi nchini Libya kwa sasa ni vifaa vya kutafuta watu walionasa kwenye matope na katika majengo yaliyoharibiwa, malazi, chakula, maji safi na usafi wa mazingira, pamoja na huduma muhimu za matibabu, kwa sababu tishio la kipindupindu linazidi kuwa kubwa.

Kuna tetesi kwamba inawezekana watu takribani 20,000 wamepoteza maisha katika mafuriko makubwa yaliyosababishwa na Kimbunga Daniel kilichotokea mwishoni mwa juma nchini Libya. 

Tags