Sep 18, 2023 10:45 UTC
  • RSF: Baada ya kushindwa kwenye medani, jeshi la Sudan limeamua kufanya mashambulio ya kipunguani Khartoum

Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan (RSF) vinavyoongozwa na Jenerali Hemedti vimesema kuwa, baada ya jeshi la Sudan (SA) kushindwa katika medani za mapambano, limeamua kufanya mashambuizi ya kiholela na kipunguani katika maeneo ya umma na ya serikali mjini Khartoum.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, mapigano yanaendelea baina ya majenerali wawili wa kijeshi, Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la Hemedti anayeongozwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan anayeongoza jeshi la Sudan (SA). 

Katika taarifa yake, vikosi vya RSF vimesema kuwa, jeshi la Sudan chini ya uongozi wa al Burhan linafanya mashambulizi ya kiholela na ya kiwendawazimu dhidi ya vituo vya serikali, dhidi ya miundombinu na kwenye maeneo ya rais mjini Khartoum.

Vita vya kuwania madaraka vinaendelea kusababisha hasara kubwa nchini Sudan

 

Taarifa ya RSF imeongeza kuwa, jeshi la Sudan linafanya mashambulizi ya makusudi dhidi ya vituo vya serikali na miundombinu ya nchi hiyo kama vile jengo la Wizara ya Mahakama, Jengo la Idara ya Kodi, Jengo la Idara ya Viwango, shirika la mafuta liitwalo al Nabil na maeneo ya raia na masoko ya biashara katika mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum.

Taarifa hiyo imetolewa dakika chache baada ya jeshi la Sudan kuvituhumu Vikosi vya Msaada wa Haraka kwamba vinafanya uharifu mtawalia katika miundombinu ya Sudan.

Vikosi vya RSF vimelituhumu jeshi la Sudan kuwa limeua watu 104 na kujeruhi mamia ya wengine katika mashambulio yake ya anga, huku msemaji wa Jeshi la Sudan akikanusha na kudai kuwa, ndege za kivita za jeshi hilo linashambulia tu mikusanyiko ya askari wa RSF na maficho yao.

Vita vya kuwania madaraka baina ya majenerali hao wawili wa kijeshi vilianza tarehe 15 Aprili mwaka huu na vimesababisha uharibifu mkubwa hadi hivi sasa. Kwa uchache watu laki tano wameshauawa wengi wao wakiwa ni raia wa kawaida, zaidi ya 12,000 wengine wamejeruhiwa na zaidi ya milioni 5 wamekuwa wakimbizi.