Sep 28, 2023 15:15 UTC
  • Serikali ya Tanzania yalalamikiwa kwa kuvunja ahadi iliyotoa kwa Waislamu

Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini Tanzania zimeilalamikia Serikali ya nchi hiyo kwa kuvunja ahadi yake ya kuwapa umiliki wa mitaala ya somo la elimu ya dini ya kiislamu.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Amir wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania(IEP), Sheikh Mussa Kundecha, akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Jopo la Wataalamu wa Kiislamu, linaloundwa na jumuiya hiyo.

Amesema katika vikao tofauti ambavyo wamefanya na uongozi wa Wizara ya Elimu, akiwemo Waziri wa Elimu, Prof. Adolph Mkenda, kwa ajili ya kuandaa na kuratibu ufundishaji wa dini ya Kiislamu na lugha ya Kiarabu, Serikali iliahidi kuacha umiliki wa somo hilo kwa Waislamu, lakini mwisho imeshindwa kutekeleza ahadi hiyo.

Waziri wa Elimu Tanzania, Profesa Adolph Mkenda

“Kinachotutia wasiwasi ni kwamba, katika kikao cha tarehe 12 Agosti 2023, Prof. Mkenda aliomba radhi na kukiri suala hili la umiliki wa mtaala libaki kwa Waislamu wenyewe kwamba michakato yote kwenye hili Taasisi ya Elimu nchini(TET) wasiingilie", ameeleza Sheikh Kundecha.

Ameongezea kwa kusema: “Wakati vikao na michakato yote ikiendelea, kuna mambo yanatatiza bado, hadi sasa ukitembelea tovuti ya TET kwenye kiunga cha mitaala, mihutasari na moduli, ipo mihutasari ya masomo 15 ya dini haijawekwa sababu TET haina haki miliki”.

Amesema jambo la kushangaza katika mihutasari ya elimu ya sekondari upo wa somo la elimu ya dini ya kiislamu ambayo imeeleza haki miliki yote ni ya Serikali hadi kudurufu ni kosa kisheria bila kupata idhini ya maandishi.

“Kupitia mkutano huu tunaishauri Serikali kuepuka hujuma na uvunjifu wa katiba unaofanywa na baadhi ya watendaji wachache wanaotaka kutumia vibaya nafasi zao,” amesema Sheikh Kundecha.

Ikijibu kauli hiyo ya Sheikh Kundecha, Wizara ya Elimu imekanusha madai hayo huku ikieleza kuwa haijachukua haki miliki ya mitaala hiyo kama ilivyoelezwa na viongozi hao na kwamba jumuiya hiyo ilitafsiri vibaya na kwamba itatoa ufafanuzi juu ya jambo hilo.../

 

Tags