Jun 30, 2016 07:56 UTC
  • Kabila ataka mazungumzo ya kitaifa yaanze mara moja

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametoa wito wa kuanza mazungumzo ya kitaifa mara moja ili kuutafutua ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Akilihutubia taifa jana usiku kwa mnasaba wa maadhimisho ya uhuru wa nchi hiyo ya Kiafrika, Rais Kabila amesema serikali yake inaunga mkono kufanyika mazungumzo ya kitaifa chini ya usuluhishi wa Edem Kodjo, Waziri Mkuu wa zamani wa Togo. Miaka 56 iliyopita mwafaka na tarehe ya leo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaani Zaire ya zamani, ilitangaza uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mbelgiji. Rais Kabila amesema lengo la mazungumzo hayo ya kitaifa ni kutanzua hitilafu zilizopo, ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao unafanyika chini ya anga ya amani na matokeo yake yanakubalika na pande zote za kisiasa. Mtandao wa habari wa Afrika Time hivi karibuni ulimnukuu Rais Kabila akiwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, zoezi ambalo linatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi ujao wa Julai. Wapinzani wanasema kuwa, lengo la mazungumzo hayo ni njama ya serikali kutaka kuakhirisha uchaguzi wa rais wa Novemba mwaka huu na hivyo kuongeza muda wa Rais Kabila kuendelea kuweko madarakani. Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, uchaguzi wa rais unapaswa kufanyika mwezi Novemba ambapo Rais Kabila hafai kuwania kiti hicho kwa muhula mwingine.

Tags