Gurunedi aina ya RPG ladondokea kimakosa kwenye uwanja wa michezo Kongo DR
(last modified Sat, 30 Sep 2023 06:56:33 GMT )
Sep 30, 2023 06:56 UTC
  • Gurunedi aina ya RPG ladondokea kimakosa kwenye uwanja wa michezo Kongo DR

Mtu mmoja ameuawa wakati gurunedi aina ya RPG lilipoangukia kimakosa katika uwanja wa michezo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza kuwa tukio hilo lilisababishwa na mwanajeshi mmoja aliyefyatua gurunedi kuelekea uwanja huo wa michezo katika mji wa Goma mashariki mwa nchi hiyo. Msemaji wa jeshi Guillaume Najiki amesema mwanajeshi huo alifyatua bila kukusudia gurunedi aina ya RPG kuelekea uwanja wa michezo wa Astad de Leventis katika jiji la Goma. Taarifa ya jeshi imesema  watu 12 walijeruhiwa na  mmoja kati yao akafariki kutokana na majeraha makali aliyopata. Kuhusu jinsi tukio hilo lilivyotokea, msemaji wa jeshi la Kongo DR amesema askari huyo alikuwa akiendesha gari la kivita ambalo lilitumbukia  kwenye shimo la barabara karibu na uwanja huo na kusababisha kufyatuka gurunedi hilo.

Waasi wa kundi la M23

Uwanja wa Master de Leventie uko umbali wa kilomita 30 kutoka mstari wa mawasiliano kati ya vikosi vya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa kundi la M23,  ambalo tokea mwishoni mwa mwaka 2021 limekuwa likidhibiti maeneo makubwa ya eneo la jimbo la Kivu Kaskazini. Kama ilivyokuwa  mizozo ya miaka ya 1990 na mwanzoni mwa karne ya 21, makumi ya makundi yenye silaha yamejitokeza mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.../

Tags