Ugonjwa wa dondakoo wauwa watu 600 Nigeria, wengi wakiwa ni watoto
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i103408-ugonjwa_wa_dondakoo_wauwa_watu_600_nigeria_wengi_wakiwa_ni_watoto
Nigeria imekumbwa na mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa (Dondakoo) yaani Diphtheria ambao umepelekea vifo vya zaidi ya watu 600, haswa watoto, tangu mwezi Desemba mwaka 2022.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 13, 2023 02:37 UTC
  • Ugonjwa wa dondakoo wauwa watu 600 Nigeria, wengi wakiwa ni watoto

Nigeria imekumbwa na mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa (Dondakoo) yaani Diphtheria ambao umepelekea vifo vya zaidi ya watu 600, haswa watoto, tangu mwezi Desemba mwaka 2022.

Mlipuko huu wa hivi karibuni wa ugonjwa huu umepindukia ule ulioripotiwa nchini humo mwaka  2011, ambapo watu 98 waliaga dunia. Kitovu cha ugonjwa huu ni katika jimbo la Kano linalopatikana kaskazini mwa Nigeria ambapo hadi sasa watu 500 wamepoteza maisha.

Dondakoo au  Diphtheria ni ugonjwa unaoambukiza sana ambao kimsingi huathiri pua na koo na pia unaweza kusababisha vidonda katika ngozi. Ugonjwa huu unaenea kupitia kukohoa, kupiga chafya na kugusana na watu wenye maambukizi huku kesi kali mara nyingi zikisababisha vifo.  

Dakta Faisal Shuaib Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Maendeleo ya Afya ya Msingi nchini Nigeria amesisitiza hali ya kuzuilika ya ugonjwa huu wakati alipokitembelea kituo cha kuwahudumia wagonjwa wa Diptheria kilichotengwa katika jimbo la Kano na kuongeza kuwa: Inaumiza sana mioyo kuona  watoto wadogo wakiwa wamelazwa katika kituo hiki wakiugua ugonjwa huu unaoweza kuzuilika.

Hii ni katika hali ambayo idadi ya vifo vya maambukizi ya ugonjwa wa Dondakoo huko Nigeria inaendelea kuongezeka huku Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha nchi hiyo (NCDC) kikitangaza kuwa hadi sasa watu 453 wamepoteza maisha huku idadi inayoshukiwa kuwa na maambukizi tangu  tarehe 24 Septemba mwaka huu ikiwa watu 11,587.

Maambukizi ya Diptheria Nigeria 

Wakati huo huo Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kwamba idadi ya vifo na maambukizi huenda vikaongezeka kutokana na upimaji duni na baadhi ya wagonjwa kutoripoti dalili zao.