Jukwaa la Afrika kuhusu wanawake, amani na usalama lafunguliwa Tunisia
Jukwaa la Sita la Ngazi za Juu la Umoja wa Afrika kuhusu Wanawake, Amani na Usalama lilifunguliwa jana Jumanne nchini Tunisia, likisisitizia udhrura wa kuweko uratibu wa pande nyingi wa kukabiliana na changamoto za pamoja.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia, jukwaa hilo la siku mbili linatoa fursa muhimu ya kuendeleza ajenda za kupigania haki, amani na usalama wa wanawake.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia, Mohamed Ali Nafti ameshukuru uamuzi wa Umoja wa Afrika (AU) wa kuitisha jukwaa hilo nchini Tunisia kwa mara ya kwanza nje ya makao makuu ya AU, akibainisha kuwa hatua hiyo inaonesha kujitolea Tunisia kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika katika ngazi zote.
Amesisitiza kwamba muktadha wa hivi sasa wa kimataifa unahitaji mshikamano mkubwa na hatua zilizoratibiwa vizuri ili kukabiliana na changamoto za pamoja, hasa katika masuala ya amani na usalama.
Nafti pia amesisitiza kwamba, amani ya kudumu inahitaji kubuniwa mbinu za kuzuia kutokea uvunjifu wa amani na za kina ambazo zitakuwa zinashughulikia sababu za kimuundo za ukosefu wa amani na usalama kama vile ukosefu wa usawa na umaskini, mambo ambayo huchochea kuhisi baadhi ya watu kuwa wametengwa na wananyanyaswa na kundi jingine la watu.
Kikao hicho cha ufunguzi cha jana Jumanne kiliwaleta pamoja wawakilishi wa nchi wanachama wa AU, mashirika ya kikanda na kimataifa pamoja na vikundi vya asasi za kiraia.