Familia za Wasudan zatafuta hifadhi Sudan Kusini
(last modified Fri, 27 Oct 2023 13:09:49 GMT )
Oct 27, 2023 13:09 UTC
  • Familia za Wasudan zatafuta hifadhi Sudan Kusini

Ripoti zinasema kuwa katika hali ya kusikitisha, familia zinazoepuka ghasia na machafuko nchini Sudan zinaendelea kuwasili katika maeneo ya mbali ya kaskazini mwa Sudan Kusini.

Raia wanaokimbia makazi yao huko Sudan wanatafuta hifadhi katika maeneo ambayo mashirika ya misaada ya kibinadamu yanapambana na changamoto kubwa ya kusambaza misaada ya dharura. Imeelezwa kuwa hali hii inachangiwa zaidi na msimu wa mvua na ukosefu mkubwa wa fedha za wafadhili, jambo ambalo linakwamisha juhudi za kuwahamisha kutoka katika maeneo ya mpakani. Hii imezidisha hali mbaya ya kibinadamu  katika kituo cha kuwapokea wakimbizi kwa muda ambacho tayari kimejaa idadi kubwa ya watu katika mji wa mpakani wa Renk.

Tangu kuibuka mapigano huko Sudan mwezi Aprili mwaka huu, yaani katika kipindi cha miezi sita  watu wanaokadiriwa milioni 6 wamelazimika kuhama makazi yao na kujaribu kutafuta hifadhi katika nchi jirani ikiwemo huko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini.  

Wakimbizi wa Sudan 

Kufuatia mzozo huko Sudan khususan uliouathiri mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum, baadhi ya raia wa nchi hiyo wameamua kukkimbilia katika mikoa mbalimbali ya nchi hiyo. 

Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa UNHCR imesema kuwa ongezeko la wakimbizi wa Sudan Kusini wanaorejea nchini na wale kutoka Sudan linazidisha mashinikizo kwa rasilimali chache za nchi ambayo bado inajikwamua kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda mrefu sambamba na kuathiriwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Wakati huo mashirika ya misaada ya kibinadamu yanafanya kila yawezalo kukabiliana na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa fedha, kushindwa kufika katika baadhi ya majimbo na miundo mbinu dhaifu.