Madaktari wa Sudan: Tumesajili kubakwa wanawake 19 na RSF huko El Fasher
-
Wakimbizi Sudan
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umetangaza kuwa timu zake katika kambi ya Al-Afad, mashariki mwa mji wa Al-Dabba kaskazini mwa Sudan, zimesajili visa 19 vya ubakaji wa wanawake waliofurushwa kutoka El-Fashir hadi katika mji wa Al-Dabba na wanachama wa kundi la waasi wa RSF.
Mtandao huo umeongeza katika taarifa yake leo Jumapili kwamba "waathiriwa wawili ni wajawazito na kwa sasa wanapewa huduma maalumu ya matibabu chini ya usimamizi wa timu za matibabu."
Mtandao huo umelaani vikali "ubakaji mkubwa unaofanywa na waasi wa RSF dhidi ya wanawake wanaokimbia huko El Fasher," na kusema vitendo hivyo "vinawalenga moja kwa moja wanawake na ni ukiukwaji wa wazi wa sheria zote za kimataifa ambazo zinatambua kuwa ni uhalifu kutumia miili ya wanawake kama silaha ya kuwakandamiza."
Mtandao huo umesema kwamba "kuendelea uhalifu huo kunaonyesha mwenendo hatari katika unyanyasaji wa makundi yaliyo hatarini zaidi," na kuonya kuwa "ukimya wa jamii ya kimataifa mbele ya vitendo hivi viovu unawahamasisha wahalifu kuendeleza ukatili huo."
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umetoa wito kwa jamii ya kimataifa, Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine husika za kutetea haki za binadamu kuwalinda wanawake na watoto katika njia za kuelekea ukimbizini, kutuma timu huru za kuchunguza ukweli, na kuhakikisha misaada ya kibinadamu na wafanyakazi wa matibabu wanawafikia wakimbizi hao.
Mtandao huo pia umetoa wito wa kuzidishwa mashinikizo kwa viongozi wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) ili kukomesha mara moja uhalifu huo na kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.
RSF haijatoa taarifa yoyote kuhusu ripoti hiyo ya Mtandao wa Huru wa Madaktari wa Sudan.