Sierra Leone: Kuna haja Baraza la Usalama la UN lifanyiwe mageuzi
Rais Ernest Bai Koroma wa Sierra Leone amesema msimamo wa viongozi wa Afrika kutaka kufanyiwa marekebisho Baraza la Usalama la Umoja Mataifa bado uko pale pale.
Akizungumza katika mji mkuu Freetown, baada ya kurejea nchini kutoka ziara ya kuzitembelea nchi nne za Afrika, Rais Koroma amesema azma ya viongozi wa bara hilo ya kutaka kufanyiwa mageuzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ingalipo na kwamba hilo limedhihirika katika safari yake hiyo ya kuzitembelea nchi za Chad, Zimbabwe, Misri na Afrika Kusini na kufanya mazungumzo na marais wa nchi hizo. Rais Koroma ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Marais wa Nchi 10 (C-10), iliyotwikwa jukumu la kutekeleza Makubaliano ya Ezulwini yaliyoafikiwa na viongozi wa Kiafrika nchini Afrika Kusini mwaka 2003. Makubaliano hayo yanahusu kushinikiza mageuzi katika Baraza la Usalama la UN na bara la Afrika kupewa heshima na hadhi kama nchi zingine wanachama wa baraza hilo. Amesema wamekubaliana na marais wa nchi hizo kwamba kilichosalia sasa ni bara la Afrika kupiga 'hatua nyingine' kuhusiana na nafasi yake katika baraza hilo na kwamba wamechoshwa na kufanyika mazungumzo kuhusu suala hilo miaka nenda miaka rudi bila natija. Umoja wa Afrika umekuwa ukisisitiza kuwa, lazima nchi za Kiafrika zipatiwe nafasi mbili za kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.