Nov 25, 2023 13:36 UTC
  • Rais William Ruto wa Kenya
    Rais William Ruto wa Kenya

Rais William Ruto wa Kenya amesema serikali yake imeweka mipango ya kuwasaidia raia ambao wameathirika na mafuriko yanayoendelea kuripotiwa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha kwenye kanda ya Afrika Mashariki.

Rais Ruto ambaye leo Jumamosi amekutana na maafisa wa idara mbalimbali zinazohusika na kukabiliana na majanga katika Ikulu ya Nairobi amethibitisha kuwa karibia watu 70 wamefariki dunia katika mafuriko hayo wakati wengine elfu 36 wakipoteza makazi yao baada ya nyumba zao kufurika maji.

Rais wa Kenya ameonya kuwa mvua itaendelea kunyesha na kwamba maandalizi zaidi yanahitajika kukabiliana na dharura zinazoweza kutokea.

Kikao cha Rais William Ruto na maafisa husika kimejadili mbinu muafaka zinazohitajika kukabiliana na athari zinazotokana na mafuriko ambayo yameendelea kuwa changamoto kwa raia katika taifa hilo la Afrika.

Rais Ruto vilevile amesema kuwa wanajeshi watasaidia katika kupeleka misaada kwenye maeneo yaliyombali na ambayo yamekumbwa na mafuriko.

Ikulu ya Nairobi

Nchi za Pembe ya Afrika zinaendelea kusumbuliwa na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hilo.

Shirika la "Save the Children" limesema kwenye ripoti yake kwamba makumi ya watu wamefariki dunia na mamia ya wengine wamelazimika kuyahama maeneo yao kutokana na mafuriko katika nchi za Pembe ya Afrika.

Taarifa ya shirika hilo imeongeza kuwa, hali ya hewa ya El Nino imezidisha mvua katika eneo la Pembe ya Afrika na kuziathiri vibaya nchi mbalimbali hasa Somalia, Ethiopia na Kenya.

Tags