Wavuvi 20 wa Kenya wauawa na wanamgambo wa Dassanech mpakani na Ethiopia
(last modified Sun, 23 Feb 2025 12:26:12 GMT )
Feb 23, 2025 12:26 UTC
  • Wavuvi 20 wa Kenya wauawa na wanamgambo wa Dassanech mpakani na Ethiopia

Zaidi ya wavuvi 20 wameuawa katika eneo la mpaka la Todonyang, kaskazini mwa Kenya, pambizoni mwa Ziwa Turkana katika shambulio la watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Dassanech kutoka nchi jirani ya Ethiopia.

Vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, shambulio hilo lilitokea jana Jumamosi saa kumi na moja jioni, katikati ya maeneo ya Lopeimukat na Natira karibu na mpaka wa Kenya na Ethiopia karibu na Mto Omo.

Duru za usalama zimeripoti kwamba, makumi ya wanamgambo wa Dassanech wa Ethiopia waliokuwa na silaha nzito waliwavizia wavuvi walipokuwa wakivua samaki katika Ziwa Turkana na kuwamiminia risasi kiholela.

Askari wa akiba katika eneo hilo amethibitisha kwamba, yumkini hujuma hiyo ilikuwa ya kulipiza kisasi baada ya jangili sugu anayetafutwa na vyombo vya usalama kwa tuhuma za kuhusika na wimbi la mauaji kando ya Ziwa Turkana, kuwapiga risasi wavuvi watatu wa genge la Dassanech katika ziwa hilo Jumamosi asubuhi.

Mvuvi akiwa kazini katika maji ya Ziwa Turkana

Askari huyo wa akiba katika eneo la mpaka la Todonyang, kaskazini mwa Kenya amesema wameona angalau miili 20 ikiwa imetapakaa ardhini, huku utambulisho wa idadi kubwa ya waliouawa katika shambulio hilo ukiwa haujajulikana.

Ripoti zinaonyesha kuwa, idadi ya waliofariki dunia inaweza kuongezeka, kwa kuwa maiti za baadhi ya wavuvi walioripotiwa kutoweka, zinaendelea kupatikana katika eneo la tukio. Kwa mujibu wa manusura, boti tano za wavuvi raia wa Kenya waliokuwa katika msafara huo zilishambuliwa, huku wote waliokuwemo wakiripotiwa kuuawa katika shambulizi la kuvizia kwenye Ziwa Turkana.