Dec 05, 2023 06:04 UTC
  • Idadi ya wahanga wa mafuriko, maporomoko Tanzania yakaribia 70

Majanga ya kimaumbile yaliyoitikisa Tanzania yamemfanya Rais Samia Suluhu Hassan wa nchi hiyo kukatisha safari yake ya Umoja wa Falme za Kiarabu; huku idadi ya wahanga wa mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyotokea katika mkoa wa Manyara kaskazini mwa Tanzania ikiongezeka na kufikia watu 68.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema kufikia jana jioni, idadi ya wahanga wa mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyotokea katika mkoa huo wa kaskazini mwa Tanzania ilikuwa imefikia watu 68, na kwamba shughuli za uokoaji na kusaka maiti zinaendelea.

Maporomoko hayo ya udongo katika Wilaya ya Hanang yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali za watu, yamemfanya Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa Dubai, Imarati kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) arejee nchini  kushughulikia kwa ukaribu janga hilo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu) Zuhura Yunus ambaye ameeleza kuwa, Rais Samia ameamua kufupisha safari yake na kurejea nchini Tanzania haraka iwezekanavyo ili kushughulikia kwa ukaribu janga hilo.

Rais Samia amesema amesikitishwa na vifo hivyo na kuagiza "nguvu kubwa ya serikali ielekezwe katika Wilaya ya Hanang ili kuwasaidia wananchi."

Rais Samia ameguswa na janga la Haning

Kulingana na mamlaka za serikali nchini Tanzania, mvua kubwa zilianza kunyesha majira ya saa 11:00 alfajiri ya Jumapili na zikasababisha mafuriko yaliyoporomosha tope kutoka Mlima Hanang, mlima wa Volkano ulio na urefu wa mita 3,418 juu ya usawa wa bahari.

Vifo zaidi viliripotiwa kutokea katika maeneo ya Katesh na Gendabi katika wilaya hiyo ya Hanang, maeneo ambayo yapo karibu na mlima huo.

Mbali na vifo na majeruhi, kumeripotiwa pia uharibufu wa makaazi, vyombo vya usafiri pamoja na miundombinu ya barabara katika eneo hilo.

Hapo jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema idadi ya watu waliofariki dunia katika mafuriko na maporomoko ya udongo Wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara, imeongezeka na kufikia 63 (wanaume 23 na wanawake ni 40) na majeruhi 116.

Tags