Maandamano Zimbabwe kulalamikia hali mbaya ya uchumi
Polisi nchini Zimbabwe wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya maelfu ya madereva waliokuwa wakiandamana kulalamikia hali inayozidi kuwa mbaya ya uchumi wa nchi hiyo.
Machafuko yaliibuka Jumatatu wakati waandamanaji walifunga barabara zote za kuelekea katikati ya mji mkuu, Harare huku wakiwarushia polisi mawe.
Wengine walioshiriki katika maandamano hayo ni vijana ambao hawawezi kupata kazi rasmi na badala yake wanalazimika kuwa makanga au kondakta katika matatu au daladala nchini humo.
Madereva wanalalamika kuwa polisi wameweka vizuizi vingi barabarani ambapo huwalazimu kutoa hongo ili waruhusiwe kuendelea na safari zao. Waandamanaji zaidi ya 70 wanaripotiwa kutiwa mbaroni kufuatia ghasia hizo mjini Harare.
Katika wiki za hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la maandamano ya Wazimbabwe wanaolalamikia hali mbaya ya uchumi na kile wanachodai ni usimamizi mbovu wa serikali ya Rais Robert Mugabe.
Wapinzani wanamtuhumu Mugabe, mwenye umri wa miaka 92, kuwa anaendesha nchi kiimla mbali na kushindwa kutatua matatizo ya kiuchumi na ukosefu mkubwa wa ajira. Mugabe ameitawala Zimbabwe tangu nchi hiyo ilipojinyakulia uhuru mwaka 1980 na ameahidi kuwa atagombea tena urais mwaka 2018. Rais huyo wa Zimbabwe anazilaumu nchi za Magharibi kuwa ndizo chanzo cha matatizo ya nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.