Juhudi za Israel za kutaka kuwa na ushawishi barani Afrika
Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni jana usiku aliwasili Kenya katika ziara ya kiserikali.
Gazeti la Star linalochapishwa nchini Kenya limeashiria safari ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni nchini Kenya na kuandika kuwa: Netanyahu anataka kufanya mashauriano ya kibiashara na kisiasa na viongozi wa Kenya ili kuimarisha uhusiano kati ya Israel na Kenya. Mikataba ya masuala ya usalama, ulinzi na kilimo imepangwa kusainiwa na pande mbili katika ziara hiyo ya Netanyahu huko Kenya. Aidha kuanzishwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tel Aviv na Nairobi ni masuala mengine yatakayofikiwa makubaliano na pande mbili za Kenya na Israel.
Hii ni ziara ya kwanza ya kiongozi wa Kizayuni barani Afrika tangu Yitzhak Rabin Waziri Mkuu wa Tano wa utawala wa Kizayuni afanye ziara nchini Morocco mwaka 1994. Utawala wa Kizayuni mbali ya kufuatilia maslahi ya kiuchumi barani Afrika, unataka pia kuungwa mkono na kuidhinishwa na nchi za Kiafrika katika taasisi za kimataifa. Hii ni katika hali ambayo hisia dhidi ya Uzayuni zingali zimetawala barani Afrika licha Israel kufanya juhudi za kuimarisha uhusiano wake na nchi za bara hilo.
Hivi karibuni washiriki katika semina ya Quds iliyofanyika mjini Dar es Salaam tanzania walitaka kuchukuliwa misimamo dhidi ya Uzayuni na kuitaka serikali ya Tanzania iisusie Israel. Katika semina hiyo kuliwasilishwa azimio lenye vipengee 11 ambalo limekosoa vikali hitilafu za kimitamo zilizopo na kushindwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti hususan Umoja wa Mataifa ili kusitisha jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Palestina wasio na hatia.
Azimio hilo limesisitiza pia juu ya udharura wa kuendelezwa hatua chanya za jamii ya kimataifa katika uwanja huo; na vilevile kuyaunga mkono mkono kwa pande zote mapambano ya wananchi wa Palestina hadi pale raia hao watakarejeshewa haki zao za kisheria. Kipengee kingine cha azimio hilo lililotolewa kwenye semina ya Siku ya Kimataifa ya Quds mjini Dar es Salaam Tanzania kinaeleza kuwa, upo udharura wa kususiwa ushirikiano wowote wa kiuchumi na uwekezaji kati ya Tanzania na Israel.
Wananchi wa Tanzania pia walishiriki katika maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds huko Dar es Salaam na kutangaza mshikamano wao kwa mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Palestina.
Hisia dhidi ya Uzayuni huko Afrika Kusini nchi ambayo inahesabika kuwa yenye uchumi mkubwa barani Afrika pia zimeongezeka na kuakisiwa pakubwa. Katika miaka ya hivi karibuni chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC kiliidhinisha taarifa na kuunga mkono rasmi juhudi za wananchi madhlumu wa Palestina kwa minajili ya kuijiainishia mustkakbali wao. Viongozi wa chama cha ANC pia waliwataka wananchi wa Afrika Kusini kuunga mkono harakati yoyote inayouweka chini ya mashinikizo utawala ghasibu wa Israel.
Ni muda sasa ambapo wapinzani wa Israel nchini Afrika Kusini wamekuwa wakitaka kukatwa uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hiyo na Wazayuni kwa kutumia nara na shaari kama "kususia na kutowekeza vitega uchumi." Baada ya kuchaguliwa Nelson Mandela kuwa Rais wa Afrika Kusini mwaka 1994 uhusiano kati ya nchi hiyo na Wazayuni ulizidi kuvurugika. Mandela alifuta mikataba yote ya ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hiyo na Israel baada ya kumalizika muda wake na badala yake alielekeza ushirikiano na uungaji mkono wake kwa Wapalestina. Weledi wa mambo wanasema kuwa misimamo inayoonyeshwa na Afrika Kusini, ikiwa ni nchi yenye uchumi unaostawi kwa kasi barani Afrika, ina nafasi muhimu katika kudhoofisha nafasi ya utawala wa Kizayuni barani Afrika.