Félix Tshisekedi atangazwa mshindi uchaguzi wa rais Congo DR, wapinzani wapinga matokeo
(last modified Mon, 01 Jan 2024 03:06:33 GMT )
Jan 01, 2024 03:06 UTC
  • Félix Tshisekedi
    Félix Tshisekedi

Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Disemba 20, 2023 kwa kupata zaidi ya asilimia 73 ya kura.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) imetangaza kuwa Felix Tshisekedi ameshinda uchaguzi wa rais kwa kupata asilimia 73.34 ya kura, Moïse Katumbi Chapwe ameshika nafasi ya pili kwa asilimia 18.08 ya kura, na nafasi ya tatu imechukuliwa Martin Madidi Fayulu ambaye amepata asilimia 5.33 ya kura. 

Matokeo hayo ya awali ya uchaguzi wa Disemba 20 yalitangazwa jana Jumapili katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kinshasa, huku kambi ya upinzani na baadhi ya mashirika ya kiraia yakitaka uchaguzi urudiwe kutokana na matatizo makubwa ya vifaa ambayo yalitilia shaka uhalali wa matokeo yake.

Wagombea wa upinzani wanaopinga matokeo hayo wana siku mbili za kuwasilisha mashtaka yao, na Mahakama ya Katiba ya Congo DR ina siku saba za kuamua kesi hiyo. Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutolewa Januari 10, na rais ataapishwa mwishoni mwa mwezi huo.

Hata hivyo kambi ya upinzani tayari imetangaza kwamba haitambui matokeo hayo ya uchaguzi, ikisema kuwa haina nia ya kukata rufaa kwa sababu, haina imani na Mahakama ya Katiba.

Félix Tshisekedi

Baada ya kutangazwa matokeo hayo, Félix Tshisekedi, aliyetangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais ametoa wito wa kuwepo umoja wa kitaifa na ameahidi kufanya kazi kwa ajili ya Wacongo wote, wakiwemo wale ambao hawakumpigia kura. 

Tags