Jan 05, 2024 02:32 UTC
  • OIC yataka kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala Somalia

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa mwito wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Somalia, kufuatia kusainiwa mapatano baina ya Ethiopia na Somaliland yatakayoiwezesha Ethiopia kutumia Bandari ya Berbera ya Somalia iliyoko katika eneo hilo la Somaliland.

Taarifa ya jana Alkhamisi ya jumuiya hiyo yenye nchi wanachama 57 imepinga hatua yoyote inayohujumu na kukiuka mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Somalia.

OIC imesema: Sekritarieti Kuu inatangaza tena mshikamano na Serikali ya Federali ya Somalia, na inasisitizia haja ya kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala nchi hiyo; na kulindwa usalama, amani na uthabiti katika eneo.

Kadhalika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Umoja wa Afrika (AU) zimelaani makubaliano hayo ambayo Ethiopia, isiyokuwa na bahari, itatumia bandari iliyoko katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Somaliland.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland, Muse Bihi Abdi wakiwa Addis Ababa 

Aidha Somalia imelaani vikali makubaliano hayo yaliyosainiwa baina ya Ethiopia na Somaliland mnamo Januari Mosi na kuitaja hatua hiyo kuwa ni kitendo cha "uchokozi".

Serikali ya Somalia imemwita balozi wake nchini Ethiopia kama hatua ya awali ya kulalamikia mapatano hayo ikisisitiza kuwa, Somaliland ni sehemu ya ardhi yake na hivyo eneo hilo halina haki ya kusaini mikataba ya kigeni.

Eneo la Somaliland lilijitenga na Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini halitambuliki kimataifa. Ethiopia inasisitiza kuwa, haijakiuka sheria yoyote kwa kufunga mkataba na Somaliland kuhusu utumizi wa bandari ya eneo hilo la Somalia.

Tags