Jan 15, 2024 08:04 UTC
  • Somalia yaionya Ethiopia: Msikiuke mamlaka ya ardhi yetu

Waziri Mkuu wa Somalia ametaka kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya nchi hiyo, wiki mbili baada ya kusainiwa mapatano baina ya Ethiopia na Somaliland yatakayoiwezesha Ethiopia kutumia Bandari ya Berbera ya Somalia iliyoko katika eneo hilo la Somaliland.

Hamza Abdi Barre alionya jana Jumapili kuwa, Ethiopia inaingilia mamlaka ya kujitawala Somalia na inapasa kuwa tayari kubeba dhima ya matokeo mabaya ya hatua yake.

Waziri Mkuu wa Somalia ameeleza bayana kuwa, makubaliano ambayo Ethiopia, isiyokuwa na bahari, ilitia saini hivi karibuni na eneo la Somalia lililotangaza kujitenga la Somaliland kuhusu utumizi wa bandari hiyo hayana itibari wala uhalali wa kisheria.

Ametoa onyo kali kwa kusema: Ethiopia haiwezi kukiuka ardhi ya Somalia. Wakijaribu kufanya hivyo, wataondoka huku wamebeba maiti zao. Maeneo ya Somalia hayawezi kutwaliwa kupitia nyimbo na vitisho. 

Ethiopia na Somalia kwa sasa ziko katika mzozo wa kidiplomasia kufuatia hatua hiyo ya Addis Ababa kutia saini mkataba wa ushirikiano na Somaliland, jimbo lililojitenga la Somalia ambalo halitambuliki kimataifa.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi Abdi mjini Addis Ababa

Mapatano hayo yalitiwa saini na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi Abdi huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia Januari Mosi, na yataiwezesha Ethiopia kutumia Bandari ya Berbera iliyoko katika eneo hilo la Somaliland.

Serikali ya Mogadishu inasisitiza kwamba, Somaliland ni sehemu ya ardhi yake na hivyo eneo hilo halina haki ya kusaini mikataba ya kigeni. Somalia imetaja hatua ya kusainiwa mapatano hayo kuwa ni kitendo cha "uchokozi".

Aidha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Umoja wa Afrika (AU) zimelaani makubaliano hayo na kutaka kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Somalia.

Tags