Jan 17, 2024 07:40 UTC
  • Wahajiri 40 wahofiwa kufa maji wakielekea Italia

Makumi ya wahajiri wanahofiwa kupoteza maisha wakiwa katika safari ya baharini wakielekea Italia.

Gadi ya Pwani ya Tunisia iliripoti habari hiyo jana Jumanne na kueleza kuwa, takriban wahamiaji 40 hawajulikana waliko baada ya boti iliyokuwa imewabeba kuelekea pwani ya Italia.

Shirika la habari la Reuters limeonesha kanda ya video ya Gadi ya Pwani ya Tunisia ikionesha meli za gadi hiyo zikisaka miili ya wahamiaji hao waliotoweka kwenye mkasa huo. 

Haya yanajiri siku chache baada ya Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kutiliana saini na Tunisia ili kuisaidia nchi hiyo kuendesha mageuzi makubwa ya kiusalama na kudhibiti uhamiaji haramu.

Aidha hayo yamekuja baada ya mamlaka za usalama nchini Tunisia kuanzisha kampeni maalumu ya usalama katika jimbo la kusini mashariki la Sfax ili kukomesha wimbi la wahamiaji haramu.

Wahamiaji wenye ndoto za kuingia Ulaya ambao wengi wao ni kutoka Afrika Magharibi wameongezeka tangu mwanzoni mwa mwaka 2023, ikilinganishwa na mwaka 2020 hadi 2022 wakati wa janga la Corona.

Hata hivyo sehemu kubwa ya wahamiaji hao haramu huwa hawafiki wanakokwenda, bali huishia kwenye mikono ya magenge ya magendo ya binadamu na kupigwa mnada masokoni kama watumwa na sehemu nyingine kubwa huzama baharini.

Tags